Katibu mwenezi mkoa wa Shinyanga ndugu Emmanuel Mlimandago |
Siku moja tu baada ya naibu waziri wa zamani wa maji nchini Anthony Diallo,ambaye sasa ni mwenyekiti wa ccm mkoa Mwanza kudai kuwa dhana inayojengwa kwamba mradi wa maji wa ziwa Victoria ulifanikishwa kwa nguvu ya aliyekuwa waziri mkuu Edward Lowassa,ni potofu na afadhali angetajwa Diallo
Moja ya magazeti ya Tanzania Raia Mwema la tarehe 24-30 Septemba 2014,lilitoka na kichwa cha habari "Diallo: Lowassa Kaleta Maji? Bora Mimi",kauli hiyo imezua kizaa.
Leo katibu wa siasa na uenezi wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Shinyanga Emmanuel Mlimandago ameibuka na kumtaka mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mwanza Dkt Antony Diallo kuacha kumtuhumu na kumtolea kashfa mbalimbali zisizothibitika na kumvujia heshima waziri mkuu mstaafu Edward Lowassa likiwemo suala la maji ya ziwa Victoria kuyatoa Ihelele mpaka Shinyanga na Kahama kwamba ni kazi yake badala ya Lowassa.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Mlimandago alisema mwenyekiti huyo wa CCM mkoa wa Mwanza amekuwa akitumia magazeti,Tv na mitandao ya kijamii kumchafua mbunge wa Monduli Edward Lowassa kitendo alichosema kinatokana na Diallo kutumika na mahasimu wa kisiasa wa Edward Lowassa.
Alisema hata suala la maji ya ziwa Victoria kuyatoa Ihelele mpaka Shinyanga na Kahama kama anavyodai yeye Diallo kuwa ni kazi yake aliyoifanya kipindi akiwa naibu waziri wa wizara ya Maji,chini ya waziri wa wizara hiyo wakati huo ikiongozwa na Lowassa,ni kuudanganya umma, kwani naibu waziri hana uwezo huo.
“Mimi kama mtanzania na kama kiongozi wa ChamaTumechoka kumvumilia,leo namuonya aache,maneno aliyoyasema ni dhahiri kuwa ameonesha udhaifu wa hali ya juu sana na hasa msomi kama yeye mwenye elimu ya PHD,amewadhalilisha wasomi kwani naibu waziri huwa ana madaraka pasipo mamlaka,namuomba aache kudanganya na kupotosha umma”,alisema Mlimandago.
“Watanzania wanajua naibu waziri haiingii kwenye baraza la mawaziri labda iwe leo,na tunajua naibu waziri hupangiwa kazi na waziri wake mwenye dhamana ya wizara na hata bungeni hujibu maswali kwa niaba ya waziri,sasa tunashangaa huo uwezo naibu waziri Diallo aliupata wapi,wakati alikuwa chini ya waziri Lowassa?”,alihoji Mlimandago.
Aidha alimtaka Diallo kuacha,chuki binafsi,fitina,majungu,siasa za majitaka, uongo na upotoshaji na kutaka kujitafutia umaarufu na heshima asizostahili kupitia mgongo wa Mheshimiwa Edward Lowassa.
“Diallo amechelewa kuyazungumzia maji ya Ziwa Victoria kwani Wana Kahama na Shinyanga wote kwa ujumla,wanajua kazi nzuri ya kupatiwa maji imefanywa na aliyekuwa waziri mwenye dhamana ya wizara ya maji Mheshimiwa Edward Lowassa”,aliongeza.
Katika hatua nyingine alimtaka kuacha kuudhihirishia umma wa Watanzania kuwa kumbe anatumika kuchamfua Lowassa huku akimwomba ayaseme mapungufu yake kama vile kueleza kwanini wananchi wa jimbo la Ilemela waliacha kumchagua nafasi ya ubunge mwaka 2010 na aleezee elimu yake na PHD alivyoipata.
“Tunaomba auleze umma,kitu gani kilimfanya aukose ubunge mwaka 2010,na ni kwa kiasi gani alichangia na kusababisha jimbo la Nyamagana na kuanguka kwa Mheshimiwa Laurence Masha na jimbo kuchukuliwa na upinzani kutokana na siasa zake za chuki na visasi na kuendeleza siasa za bora tukose wote”,alifafanua Mlimandago.
Katika hatua nyingine alimshauri mwenyekiti huyo wa CCM mkoa wa Mwanza kutumia muda wake kushughulika na kupanga mikakati wa jinsi ya kupambana na mauaji ya akina mama vikongwe na albino ikizingatiwa kuwa mkoa huo unaongoza kwa mauaji hayo nchini.
Aliongeza kuwa ni vyema sasa Diallo akajikita kushughulika kuokoa majimbo yake yaliyochukuliwa na upinzani mfano jimbo la Ilemela,Nyamagana na Ukerewe kuliko kuendeleza malumbano na kugombania nafasi zisizokuwa na tija na kwamba kutokana na kuwa yeye ni kiongozi wa chama apeleke hoja zake kwenye vikao vya chama badala ya kuzungumza nje ya vikao
Na Kadama Malunde- Shinyanga
BOFYA HAPA KUSOMA TAMKO LA KATIBU MWENEZI WA CCM MKOA WA SHINYANGA,PIA UONE HABARI ILIYOZUA BALAA YA DIALLO KUMLIPUA LOWASSA
BOFYA HAPA KUSOMA TAMKO LA KATIBU MWENEZI WA CCM MKOA WA SHINYANGA,PIA UONE HABARI ILIYOZUA BALAA YA DIALLO KUMLIPUA LOWASSA