MKUU wa Wilaya ya KahamaBenson Mpesya amewataka watumishi katika hospitali ya Halmashauri ya mji wa Kahama kufanya kazi kwa weledi bila kujali mgawanyo wa kiutawala uliofanywa wakati wa kuigawa wilaya hiyo.
Kauli hiyo ameitoa juzi mjini Kahama wakati akipokea msaada wa vitanda 27 vya kisasa vya wagonjwa katika hospitali hiyo vilivyotolewa na Kampuni ya African Barrick Gold Mine kupitia Mgodi wake wa Buzwagi.
|
Katika makabidhiano hayo Mpesya amesema ameshangazwa na mgawanyo wa kiutawala wa wilaya ya Kahama iliyogawanywa kwenye halmashauri tatu za Mji,Ushetu na Msalala mgawo huo umeathiri huduma za afya.
Aidha Mpesya amesema mgawo huo pia umekwenda sambamba na hospitali ya wilaya ambayo nayo imegawanywa katika Halmashauri tatu hali iliyodhoofisha utendaji kazi kwa kuwagawa madaktari katika halmashauri tatu,badala ya kuimarisha moja ya wilaya.
Alipendekeza Madiwani hao wangeweza kutumia busara wakaacha kuigawa hospitali hiyo ambayo imesimama kama ya Rufaa kwa kutoa huduma kwa wagonjwa wanaotoka katika Halmashauri zao,badala ya kuwapeleka Madaktari kwenye zahanati za vijiji,huku wilaya kukiwa na mapungufu.
Naye Meneja Uendelevu wa Mgodi wa Buzwagi George Mkanza amesema vitanda hivyo vimetolewa na Madaktari rafiki wa Kampuni hiyo kutoka nchini Austaria na vimegharimu Shilingi Milioni 54.