Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MTOTO LOWASSA AKATWA VIDOLE 9 NA BOMU HUKO ARUSHA


Mtoto Lowassa Kivuyo (14), amelazwa katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center, baada ya kulipukiwa na kitu kinachodhaniwa kuwa bomu na kumkata vidole tisa vya mikono yake.
Akizungumza kwa tabu katika hospitali hiyo, mtoto huyo  alisema tukio hilo lilitokea Jumapili Septemba 7, mwaka huu saa tisa mchana akiwa na wenzake watatu walipokuwa wakichunga ng’ombe.
Alisema waliona kitu kama kifuniko cha mpira ambacho kilikuwa kimefungwa na kuanza kurushiana na wenzake, Charles Ngine, Baraka Silonga na Long’otuti Petro na ghafla kililipuka.
Alisema mwenzake, Petro alijeruhiwa kichwani huku ng’ombe watatu pia wakijeruhiwa na kitu hicho.
Kaka wa Lowassa, ambaye anamtunza hospitalini hapo, Maige Kivuyo alisema tukio hilo lilitokea eneo la Elperera, Kata ya Sepeko wilayani Monduli.
“Alikuwa na wenzake wanachezea kwa kurushiana kitu ambacho tunadhani ni bomu na ndipo kililipuka,” alisema.`
Kivuyo alisema eneo hilo ni la Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) lakini huwa wanaruhusiwa kuingiza mifugo yao mara baada ya mazoezi kumalizika.
Muuguzi wa zamu wa wodi namba mbili, kitengo cha mifupa, alipolazwa Lowassa, Deodata Mahela alisema mtoto huyo amekatika vidole tisa na amebaki na kimoja cha mkono wa kushoto.
“Hivi sasa anaendelea vizuri baada ya kupata matibabu, kwani pia alikuwa amepata majeraha mengine kidogo pembeni ya kifua,” alisema Mahela.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa JWTZ, Luteni Kanali Erick Komba alisema jeshi halina taarifa za tukio hilo.
“Tutachunguza mara moja na kupata ukweli wa taarifa hiyo,” alisema.
Na Mussa Juma, Mwananchi
TUNAPENDA TUKUTUMIE HABARI ZETU MARA TU ZINAPOTOKEA, LIKE PAGE YETU SASA HIVI UENDE NA WAKATI. BONYEZA HAYA MANENO

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com