Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limetaka jeshi la polisi kufumuliwa na kuundwa upya kwa madai ya kushindwa kufanyakazi kwa kufuata maadili.
Tamko hilo limekuja siku moja baada ya waandishi wa habari kupigwa na polisi wakati wakitekeleza majukumu yao juzi jijini Dar es Salaam.Waandishi hao walikuwa wakifuatilia tukio la kuhojiwa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, Makao Makuu ya Jeshi la Polisi nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa TEF, Absalom Kibanda, alisema kuwa tukio hilo limewasikitisha kwani limekuwa mwendelezo wa jeshi hilo kuwapiga waandishi wa habari wanapokuwa wakitekeleza wajibu wao.
Kibamba alisema kwa tukio la juzi imejidhihirisha kwamba polisi hawajifunzi kutokana na matukio yaliyotangulia na pengine wamekuwa wakifanya vitendo hivyo kwa makusudi wakiwalenga waandishi wa habari.
Alisema katika mazingira hayo, wanashawishika kukumbuka kauli iliyotolewa na Mbunge wa zamani wa Shinyanga Mjini (CCM), Leonard Derefa, ambaye aliwahi kusema jeshi la polisi livunjwe ili liundwe upya.
Kibanda alisema mwenendo wa polisi unawashangaza kwa kuwa polisi hao hao kila kukicha huwaita waandishi wa habari kwa lengo la kuujulisha umma kuhusu masuala mbalimbali dhidi ya usalama wa nchi kwa ujumla.
Alisema hata tangazo la Mbowe kuhusu maandamano polisi walilifahamu kupitia vyombo vya habari lakini inasikitisha polisi hao kuonekana ni maadui zao walipokwenda makao makuu ya polisi kufuatilia tukio hilo.
Kibanda alisema TEF inaamini kuwa kupigwa waandishi wa habari haikuwa bahati mbaya bali ilifanyika kwa makusudi kwa nia ya kuwapiga na kuwajeruhi.
“Tuna sema hivi kwa sababu tuna ushahidi kwamba waliopigwa walitoa na kuonyesha vitambulisho vyao mapema kwa hiyo polisi walifahamu kwamba hao walikuwa waandishi wa habari hivyo waliwalenga,” alisema.
Aidha, alisema tukio la kifo cha mwandishi Mwangosi lilifanyika mbele ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, "baada ya kufanya kazi yake vizuri kwa maono ya jeshi la polisi alipandishwa cheo na kuhamishiwa makao makuu ya polisi.”
Kibanda alisema pengine polisi waliohusika katika tukio la juzi nao wanatafuta kupandishwa cheo kama Afande Kamuhanda.
Alisema ili polisi kujinasua katika tuhuma hizo inapaswa kuchukua hatua za wazi dhidi ya polisi waliohusika kuwashambulia waandishi watatu wa habari, ukimya wao utajidhihirisha walikusudia kuwapiga na kuwajeruhi.
Kibanda alisema TEF itaandika barua ya malalamiko kwa IGP kumuomba achukue hatua dhidi ya askari waliohusika kuwashambulia waandishi wa habari.
Alisema wataendelea kutumia kalamu zao kulaani matukio haya ya polisi dhidi ya waandishi wa habari pamoja na athari zake kwa umma ili itoe hukumu inayostahili kwa jeshi hilo.
Hata hivyo, alisema serikali inatakiwa kuchunguza kwa kina matukio hayo ya polisi kuwashambulia waandishi wa habari, kujua hasira za polisi zinatokana na nini na wanataka kuficha nini na watathmini athari zake katika mfumo nzima utoaji na upatikanaji wa habari nchini.
MCT YANENA
Baraza la Habari Tanzania (MCT), limelaani kitendo hicho ambacho waandishi wa habari lengo lao lilikuwa ni kufuatilia habari za Mbowe aliyeitwa kuhojiwa dhidi ya kauli ya Chadema ya kuitisha maandamano na migomo nchini.
Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Kajubi Mukajanga, imesema kuwa, MCT inaamini mashambulizi hayo hayakuwa bahati mbaya kwa kuwa ni mfululizo wa Jeshi hilo kuwanyanyasa waandishi wakati wakiwa katika kazi.
Aidha, Baraza hilo limeeleza kuwa mashambulizi hayo siyo tu yamelenga kuficha ukatili uliokusudiwa kufanywa, bali unaibua chuki baina ya taasisi hiyo na vyombo vya habari bila sababu za msingi.
“Unyanyasaji huu wa polisi ulifanyika mbele ya viongozi wakuu wa Jeshi akiwamo Kamishna wa Opereseheni na Mafunzo, MCT tunalishauri jeshi la polisi kuacha waandishi wa habari kufanya kazi zao badala ya kutumia nguvu kupita kiasi ikiwa ni pamoja na kuharibu vitendea kazi vyao,” ilisema taarifa hiyo.
Aidha, Baraza hilo limetoa pole kwa waandishi walioshambuliwa na kuumizwa ambao ni Josephat Isango (Tanzania Daima), Shamin Aus (Hoja) Yusuf Badi (Mpiga picha wa Magazeti ya Serikali, Tanzania Standard Newspapers.
Pia limesema kuwa, vitendo vya kikatili vya namna hiyo vinavyofifisha uhuru wa habari na kujieleza, ni vya aibu na vinashusha hadhi ya nchi na kumdhalilisha Rais wa nchi machoni pa mataifa kwa kuwa ni muumini na mchangiaji wa dhati wa makubaliano ya kuendesha serikali kwa uwazi.
UPTC YALAANI POLISI KIPIGO CHA WANAHABARI
Klabu za waandishi habari nchini (UTPC), imetoa tamko la kulaani kitendo cha polisi wa jijini Dar es Salaam kuwapiga baadhi ya waandishi wa habari waliokuwa wakisubiri kufanya mahojiano na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Akizungumza na wanahabari jijini Mwanza jana, Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC, Abubakar Kassan, alisema kitendo cha polisi kurudia vitendo vile vile vya kuwanyanyasa waandishi wa habari wanapokuwa kazini, hakina budi kulaaniwa.
Alisema inawezekana kitendo cha polisi kuwafukuza wafuasi wa Chadema kilikuwa sahihi, lakini wanapaswa kukumbuka wanahabari walikuwa kazini kutoa taarifa kwa jamii kuhusu mahojiano ya polisi na Mbowe.
WAFUASI WA CHADEMA MBARONI
Wafuasi wa Chadema wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kuingia Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kinyume na utaratibu.
Wafuasi hao ni Ngaiza Kamugisha (28) dereva, mkazi wa Vingunguti, Benito Mwapinga (30) Fundi nguo mkazi wa Mtoni kwa Azzi Ally na Eliasante Bugeji (51) Mhasibu wa CCBRT mkazi wa Komakoma Kinondoni, Dar es Salaam.
Wakili wa Serikali Mkuu, Benard Kongola akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka na George Barasa, walidai kuwa wafuasi hao wanakabiliwa na mashtaka matatu.
Kongola alidai mbele ya Hakimu Mkazi Frank Moshi kuwa washitakiwa waliingia kwa nguvu Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, kukaidi amri halali na kutoa lugha ya matusi.
Alidai Septemba 18 maeneo hayo washtakiwa walikataa kutii amri ya halali ya kutawanyika eneo la makao hayo iliyotolewa na Mkaguzi wa Jeshi la Polisi, Inspeta Zuhura, ambaye alitoa amri hiyo baada ya kuruhusiwa na viongozi wake.
Katika shtaka la tatu linalomkabili Bugeji peke yake, inadaiwa Septemba 18, akiwa katika mazingira ya Makao Makuu ya Jeshi la Polisi alitoa lugha ya matusi kwa Maofisa wa Polisi.
Wakili wa wafuasi hao Peter Kibatala alidai mashtaka yanayowakabili washtakiwa yanadhaminika, hivyo wanaomba mahakama iwapatie masharti na fuu kwa mujibu wa sheria.
Moshi alisema ili washtakiwa wawe nje kwa dhamana, wanatakiwa wawe na wadhamini wawili wa kuaminika wakiwamo watumishi wa serikali au watumishi kutoka katika Taasisi inayotambulika wakiwa na barua za waajiri wao na vitambulisho vya kazi na wadhamini watasaini bondi ya Sh. 500,000 kwa kila mmoja. Washtakiwa hao walipata dhamana. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 24, washtakiwa watakaposomewa maelezo ya awali.
Nje ya mahakama Mratibu wa Chadema Kanda ya Pwani, Nickson Tugala alikuwa aking'ang'ania kuingia mahabusu kuwaona washtakiwa jambo ambalo lilisababisha fujo katika eneo hilo.
Tugala alionekana kubishana na Insepta wa Jeshi la Polisi Mussa Mkini mpaka kufikia hatua ya kusogelea kwa karibu hali iliyowatia hofu watu waliyokuwa katika eneo hilo kuwa watu hao wanataka kupigana.
Ambapo, Mkini ilimbidi aombe nguvu kutoka Jeshi la Polisi, ilipofika saa 6:10 mchana ziliingia gari mbili za polisi namba PT 1846 na PT 1145 zikiwa na askari wenye silaha za moto.
Mkini alitoa amri ya Tugala kuchukuliwa na kupelekwa kituo cha polisi cha Kati kutokana na fujo lakini bado alikuwa akiwagomea askari hao.
Baadaye alikubali kuondoka nao, ambapo askari wawili walipanda kwenye gari ambalo alikuwa akiendesha la M4C namba T 351 CAY. Askari mmoja alipanda ndani ya gari na mwingine alipanda nyuma ya gari hilo wakiongoza kwenda ‘Central’.
CHADEMA YAMTAKA DK. BILAL KUTOA TAMKO
Chadema kimemtaka Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, ajitokeze hadharani na atoe kauli kama alitoa maelekezo mengine kwa vyombo vya dola dhidi ya vyombo vya habari mara baada ya kukutana na wahariri.
Pia Chadema kimemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, atoe kauli mbele ya umma ni hatua gani watachukua dhidi ya askari waliofanya tukio hilo baada ya kupata maelekezo kutoka kwa Kamishna wa Polisi Operesheni na Mafunzo, Paulo Chagonja.
“Chagonja alisimamia operesheni mbele ya jeshi na kuhakikisha kupigwa kwa waandishi wa habari, licha ya waandishi kuonyesha vitendea kazi vyao vikiwamo kamera lakini waliumizwa,” alisema.
KIPENGELE CHA KUTETEA WANAHABARI
SIKU moja baada ya Polisi kuwapiga waandishi wa habari katika ofisi za makao makuu ya Jeshi hilo Jijini Dar es Salaam, baadhi ya wadau wameomba Bunge litakapofanya marekebisho ya Katiba ya mwaka 1977 ambayo yamepangwa kufanyika kwa ajili ya kuelekea kwenye uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, haki za wanahabari pia ziingizwe ili kuwawezesha kufanya vema kazi zao wakati mchakato wa Katiba mpya utakapokuwa umesimama.
Pia wabunge wa Bunge Maalum la Katiba wameombwa kupitisha ibara mbili zinazohusu haki na Uhuru wa Habari kwenye Rasimu ya Katiba kama zilivyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ili kukomesha kabisa vitendo vya wanahabari kuzuiwa kufanya kazi wao na vyombo vya dola.
Maombi hayo yametolewa na wanahabari wa vyombo mbalimbali waliokutana jana mjini Dodoma kwa ajili ya kuhamasisha wabunge wakubali kupitisha Ibara ya 30 na 31 za Rasimu ya Katiba mpya kama zilivyopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba, pamoja na marekebisho madogo yaliyofanywa kwenye ibara hizo.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mhariri mtendaji wa Gazeti la Jamhuri, Deodatus Balile, alisema kuwa umefika wakati ambao vitendo vya udhalimu kwa wanahabari kupigwa ama kunyang’anywa zana zao za kazi vikomeshwa kwa haki za wanahabari kutambulika kikatiba.
Alisema kuwa wanahabari wanapigwa kutokana na kutotambulika kikatiba huku sheria iliyopo ikiwa haitoi fursa nzuri kwa wandishi wa habari kufanya kazi zao kwa uhuru kwa kuwa ilitungwa kwa malengo ya kudhibiti habari badala ya kuwezesha upatikanaji wa habari.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba alisema kuwa wanasiasa wamekuwa ni watu wenye kujali maslahi yao pekee na ndiyo sababu kwenye makubaliano baina ya Rais Kikwete na Kituo cha Demokrasia nchini (TCD) wameazimia kuifanyia mabadiliko Katiba ya mwaka 1977 katika mambo manne tu yanayohusu siasa ili kuwawezesha kuingia kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Kibamba alipendekeza kuwa katika mabadiliko hayo Ibara ya 30 na 31 za Rasimu ya Katiba zichukuliwe kama zilivyo na kuingizwa kwenye Katiba ya mwaka 1977 kuchukua nafasi ya Ibara ya 18 ya Katiba hiyo ili kuwafanya wanahabari nao wawe na haki ya kupata habari bila vikwazo taifa linapoelekea kwenye uchaguzi.
Mwanasheria wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Godfrey Pandikizi alisema kuwa endapo mabadiliko hayo yatafanyika yatasaidia wanahabari kuwa na uwezo, uhuru na haki ya kikatiba ya kufanya shughuli zao mahali popote na kuwa huwenda vitendo viovu vya kupigwa na kuporwa zana zao wanavyofanyiwa na Jeshi la Polisi vikapungua kwa kiasi kikubwa.
Na Beatrice Shayo, Dar es Salaam, Cynthia Mwilolezi, Arusha, Rose Jacob, Mwanza, na Emmanuel Lengwa, Dodoma-Nipashe