|
Wakazi wa mji wa vitongoji vya Bukombe mkoani Geita na maeneo jirani wakiwa katika kituo cha Polisi Bukombe kuaga miili ya askari wawili waliouawa kwa bomu juzi usiku baada ya majambazi kuvamia kituo hicho na kuwashambulia kisha kupora silaha. Picha na Ernest Magashi
Siku moja baada ya kituo cha polisi cha Wilaya ya Bukombe mkoani Geita kuvamiwa na majambazi wakiwa na silaha na kuua polisi wawili, Jeshi la Polisi limemtia mbaroni mtu mmoja akidaiwa kuhusika katika tukio hilo.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu, mtu huyo alikamatwa juzi usiku mkoani Geita akiwa na silaha mbalimbali yakiwamo mabomu ya machozi.
Alizitaja silaha zilizokamatwa kuwa ni pamoja na bunduki sita aina ya SMG, pump action tatu na mabomu 11 ya machozi.
Hata hivyo, Mangu alisema baada ya uchunguzi wa kina kutokana na tukio walimtia nguvuni jambazi huyo ambaye hata hivyo hakumtaja jina.
Alisema walipomkamata aliwaonyesha mahali silaha zilipo, hatua ambayo moja kwa moja inaonyesha alihusika kwenye tukio la uvamizi wa kituo cha polisi Bukombe.
“Jitihada za kumkamata mtu huyo zilifanywa na polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama,” alisema Mangu na kuongeza:
“Kutokana na uchunguzi walioufanya, majambazi wako kwenye misitu mikubwa wanajificha kwenye mgongo wa ufugaji.
Mangu alisema, “Naomba wafugaji wote mtoke kwenye mapori, kwani chanzo cha uhalifu ni huko, sasa sitakuwa na mzaha kwenye jambo hili, nitahakikisha nawaondoa wote, lakini hii itakuwa kwa sababu za kiusalama zaidi.”
Katika tukio hilo askari wawili walipoteza maisha na wengine wawili kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili.
|
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com