Naibu katibu mkuu Taifa,katibu wa tawi la tamico mgodi wa dhahabu ya Geita Thomas Sabai
Baada ya muda mrefu chama cha wafanyakazi wa migodi,nishati,ujenzi na kazi nyinginezo(TAMICO) kutokuwa na naibu katibu mkuu Taifa,katibu wa tawi la tamico mgodi wa dhahabu ya Geita Thomas Sabai amepata nafasi hiyo kutokana na juhudi zake za kutetea maslahi ya wafanyakazi.
Mfanyakazi huyo mwenye umri wa miaka 44,ni mwanaharakati wa vyama vya wafanyakazi (trade unionist)aliyesababisha wafanyakazi na wanachama wa mgodi wa Geita gold mine LTD kunufaika naye baada ya kufunga mikataba ya hali bora mahali pa kazi huku matawi ya kanda ya magharibi Shinyanga yakilala kutokuwa na mikataba hiyo.
Kutokana na utendaji wake makini na juhudi za kuwaunganisha wafanyakazi wa mgodi huo,baraza kuu la Taifa la chama hicho lililidhia kumteua kwenye nafasi hiyo baada ya kuonyesha nia ili aweze kusaidia wafanyakazi wa kanda zingine ambao wanafanyakazi katika mazingira magumu.
Kikao cha baraza kuu la Taifa la chama hicho cha mei 30 mwaka huu huko morogoro,kililizia mapendekezo ya kamati tendaji ya Tamico Taifa na kuagiza kuajiriwa kwa barua ya tarehe 04 juni 2014 iliyosainiwa na katibu mkuu wa chama hicho Hassan Ameir .
Sabai mwenye elimu ya uhasibu na biashara kutoka katika chuo kikuu cha Daystar University Nairobi Kenya amesoma kozi nyingi za kutetea wafanyakazi ndani na nje ya nchi.
“nilijitahidi kuwaunganisha wafanyakazi wa mgodini kwangu,na kusababisha wanichaguwe katika nafasi mbalimbali za uongozi wa chama hiki cha wafanyakazi,ikiwa ni pamoja na mjumbe wa kamati tendaji ya wilaya,kanda ya ziwa,mjumbe wa mkutano mkuu Taifa,mjumbe wa bodi ya wadhamini na mjumbe wa Anglo Gold Ashanti Shaft Steward Council Continental Africa” alibainisha Sabai
Akiwa katibu wa tawi katika mgodi wa dhahabu wa Geita Gold Mine, alisababisha kufungwa mkataba ya hali bora kwa wafanyakazi na mwaka huu alikuwa akiendelea na mazungumzo na mwajiri kwa ajiri ya kukamilisha baadhi vipengele kwenye mkataba wa hali bora vyenye manufaa kwa wanachama na wafanyakazi wa mgodini hapo.
Kupata nafasi hiyo,itakuwa ni furaha kwa wafanyakazi wa chama hicho wa kanda ya magharibi Shinyanga ambapo kamati tendaji ya TAMICO kanda hiyo iliamua kuutuhumu uongozi wa juu kuwa haujajishughulisha na uwekaji wa mikataba ya hali bora kwa wafanyakazi waliopo katika matawi ya kanda ya magharibi Shinyanga na kama ipo ni duni na haiwasaidii.
Kikao cha kamati tendaji cha kanda ya magharibi Shinyanga cha juni 21 ,2014 kilichofanyika Liga hoteli mjini Shinyanga, chini ya mwenyekiti wake Antony Masonda kilitoa tamko lililokuwa likiutaka uongozi wa juu wa chama hicho Taifa kuondoka madarakani kwa sababu mbalimbali zikiwemo za kutumia vibaya rasilimali za chama na kutosimamia katiba ili kufikia malengo na dira ya chama ya kuwasaidia wafanyakazi kupata maslahi bora na kutetea haki zao mahala pa kazi.
Kamati tendaji ya kanda ya magharibi Shinyanga katika kikao chake kilieleza kwamba tangu chama kilipoanzishwa hadi leo viongozi wake wa ngazi ya Kitaifa wameshindwa kutimiza malengo ya kufunga mikataba ya hali bora mahali pa kazi na kwamba karibu matawi yote ya kanda ya magharibi Shinyanga hayana mikataba ya hali bora hata kama baadhi yanayo mikataba hiyo ni duni na dhaifu,na haikidhi matarajio ya wafanyakazi.
Hata hivyo katibu mkuu wa Tamico Taifa Hassan Ameir alipinga madai ya kamati tendaji ya kanda ya magharibi na kuiagiza izingatie maelekezo ya katiba ya chama hicho na kuwataka kufanyakazi kwa faida ya wanachama na wafanyakazi wa TAMICO.
Kuajiriwa kwa Thomas Sabai itakuwa ni furaha kwa wafanyakazi na wanachama wa chama cha wafanyakazi wa migodi,nishati,ujenzi na kazi nyinginezo hapa nchini kutokana na umakini na uchapa kazi alioufanya katika mgodi wa dhahabu wa Geita Gold Mine LTD kwa kuwaunganisha wafanyakazi na kuweka mkataba wa hali bora.
Ni wazi kwamba migogoro ya wanachama na viongozi wake itapungua kama siyo kuisha kabisa endapo utakuwepo ushirikiano kati ya Naibu katibu mkuu huyo na matawi yote ya kanda ya magharibi Shinyanga wafanyakazi wake watakuwa na mikataba ya hali bora na imara ambayo itakidhi matarajio ya wafanyakazi wa chama hicho.
Stephen Kidoyayi-Shinyanga
TAFADHALI BOFYA HAPA U LIKE PAGE YETU TUKUTUMIE "HABARI" MOJA KWA MOJA KILA ZINAPOTOKEA
TAFADHALI BOFYA HAPA U LIKE PAGE YETU TUKUTUMIE "HABARI" MOJA KWA MOJA KILA ZINAPOTOKEA