Kulia ni katibu tawala wa mkoa wa Shinyanga Dkt Anselm Tarimo akikabidhi mashine 20 za kufyatulia matofali kwa viongozi kutoka halmashauri za wilaya mkoa wa Shinyanga katikati ya wiki hii nje ya ofisi ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga-Picha na Kadama Malunde KUTAZAMA PICHA ZINGINE BONYEZA HAPA |
Shirika la nyumba la taifa limekabidhi mashine 20 za kufyatulia tofali kwa vijana mkoa wa Shinyanga kuwasaidia kuondokana na tatizo sugu la ajira sambamba na kuinua uchumi kwa vijana 200.
Akizungumza wiki hii wakati wa hafla fupi ya kukabidhi mashine hizo kwa uongozi wa mkoa wa Shinyanga,meneja wa shirika la nyumba taifa mkoa wa Shinyanga(NHC) Ramadhan Macha alisema lengo la kutoa mashine hizo ni kusaidia makundi ya vijana katika halmashauri zote nchini.
Macha alisema tukio hilo kimsingi ni matokeo ya utekelezaji wa mpango mkakati wa shirika wa miaka mitano(2011/2011-2014/2015) ambapo pamoja na kulenga kupunguza tatizo la makazi nchini kwa kujenga nyumba 15,000 nchi nzima ifikapo mwaka 2015.
Alisema mbali na lengo hilo pia walijiwekea malengo ya kusaidiana na serikali katika kupunguza tatizo la ajira kwa vijana na tayari shirika limetoa mafunzo kwa wakufunzi watakaotoa mafunzo kwa vikundi vya vijana watakaopewa mashine hizo ili zitumike kwa tija na kudumu kwa muda mrefu zaidi.
“Tayari katibu tawala wa mkoa alishafahamishwa kuhusu suala hili na taarifa hizo kunakiliwa na kusambazwa kwa wakuu wa wilaya,wakurugenzi wa halmashauri zote,wakiombwa kuandaa vikundi kila kimoja vijana 40,kuwa na uongozi,usajili na akaunti ya benki na jambo hili limeshatekelezwa na halmashauri zote”,aliongeza Macha.
“Mashine tunazokabidhi leo ni 20 zenye thamani ya shilingi milioni 9,zina gharama nafuu,rahisi kuzitumia,zimetengenezwa hapa nchini kwa kutumia teknolojia rahisi,kila halmashauri itapewa mashine 4,isipokuwa halmashauri ya Ushetu itayaokabidhiwa kipindi kijacho”,alisema.
Katika hatua nyingine alisema bidhaa inayozalishwa kutokana na mashine hizo ni rafiki wa mazingira kutokana na kwamba hutumia saruji kidogo na udongo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi mashine hizo kwa viongozi wa halmashauri za wilaya katibu tawala wa mkoa wa Shinyanga Dkt Anselm Tarimo aliwataka maafisawa vijana katika kila halmashauri kusimamia vikundi hivyo vya vijana na taarifa za utekelezaji zitolewe kila baada ya miezi mitatu.
Katika hatua nyingine alitoa angalizo kwa vikundi hivyo kutoingiza siasa ili viwe endelevu na kuomba wananchi kujitokeza kununua matofali yanayotengenezwa na vijana hao kwani wakipata soko wataweza kujiendeleza zaidi.
Mashine hizo 20 zitakabidhiwa kwa vijana lengwa 200,kutoka halmashauri ya Msalala,Kahama mji,Shinyanga,Manispaa ya Shinyanga na Kishapu wataopewa shilingi 500,000/= kila kundi kama mtaji wa kuanzia baada ya kupatiwa mafunzo juu ya mashine hizo.
KUTAZAMA PICHA ZINGINE BONYEZA HAPA |
Na Kadama Malunde-Shinyanga