BAADA TU YA KATIBA MPYA KUPITA KWA KUPATA THELUTHI MBILI ZA TANZANIA BARA NA ZANZIBAR, SASA SAMWEL SITTA AVIZIWA MTAANI.
Saturday, October 04, 2014
Samuel Sitta.PICHA|MAKTABA. Dar es Salaam. Baada ya
Bunge la Katiba juzi kufanikiwa kupata theluthi mbili ya wajumbe wa
pande zote mbili za Muungano na kupitisha Katiba inayopendekezwa, sasa
msuguano kuhusu Katiba unaonekana kuhamia uraiani.
Msuguano
kuhusu Katiba hiyo unatarajiwa kuendelea mitaani, ndani ya vyama vya
siasa na kwenye majukwaa kutokana na tofauti ya mitizamo iliyoibuka
kuhusu Rasimu ya Katiba iliyopitishwa.
Ingawa matokeo ya
kura za ushindi yalipokewa kwa furaha na wajumbe waliokuwapo bungeni kwa
kucheza na kurusha vijembe kwa wapinzani, huenda kibarua kitakuwa
kigumu kwa CCM itakapolazimika kupambana na wananchi, wanasiasa,
wanaharakati na viongozi wa dini ‘waliojeruhiwa’ na mwenendo wa Bunge.
Bunge
hilo liliendeshwa kwa upinzani mkali kutoka kwa makundi mbalimbali ya
watu waliokuwa wakitaka lisimamishwe kwa madai kuwa limechakachua maoni
yao kama yalivyopendekezwa kwenye Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa
bungeni na Tume ya Jaji Joseph Warioba.
CCM na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar CCM
iliingia doa baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar (SMZ), Othman Masoud Othman kuzua kizaazaa bungeni Jumatano
wiki iliyopita kwa kupiga kura ya hapana katika ibara 22 kwenye Rasimu
ya Katiba iliyopendekezwa.
Mwanasheria huyo ambaye awali
alijiondoa kwenye Kamati ya Uandishi kwa kutoridhishwa na mambo
yalivyokuwa yanakwenda, alizomewa na baadhi ya wajumbe na kulazimika
kutolewa ukumbini akiwa chini ya ulinzi wa askari wa Bunge.
Akizungumza
na gazeti hili, Othman alisema kuwa alichofanya kilikuwa ni utashi wake
kwa kuwa Serikali ilitamka kwenye Baraza la Wawakilishi na hata nje ya
Baraza kuwa haikuwa na msimamo.
“Kwa hiyo kama Serikali
haikuwa na msimamo kwa maana ya upande, maana yake ni ipi pengine
unisadie… nilipiga kura kwa kuzingatia utashi wangu na maoni yangu,”
alinukuliwa Othman.
Ingawa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba,
Samuel Sitta alimtetea Othmani kwa kusema wajumbe hawakupiga kura kwa
kutumia vyeo vyao, kwa namna wajumbe walivyoonyesha jazba imeonyesha
kuwa CCM itapaswa kusafishwa taswira iliyochafuka.
Sitta na viongozi wa dini Kwa
upande mwingine, Sitta amejikuta akiingia kwenye ‘vita’ na viongozi wa
dini, baada ya kuwataka waumini wa madhehebu mbalimbali kuupuza nyaraka
zilizotolewa na viongozi hao kwa kuwa hazina utukufu wowote wa Mwenyezi
Mungu.
Sitta alisema baadhi ya viongozi wa dini wanalenga
kuliingiza taifa kwenye machafuko na kwamba yeye hatakuwa tayari
kuvumilia hali hiyo.
Waraka huo ulitolewa kwa pamoja na
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Jumuiya ya Kikristo Tanzania
(CCT), Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (FPCT) na Kanisa la
Waadventista Wasabato (SDA).
Huku akiwa na waraka huo
mkononi, Sitta alisema kuwa lugha iliyotumika haina staha na haikupaswa
kutumiwa na watu wanaohubiri dini duniani.
Akizungumzia
kauli ya Sitta, Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius
Kilaini alisema kauli ya Sitta inaonyesha kuwa amechoshwa na mwenendo wa
Bunge la Katiba.
“Sikutarajia kiongozi kama huyo kutoa
kauli mbaya kama hiyo kwa Taifa zima. Sikutegemea mheshimiwa kama huyo
kusema maneno kama hayo… Huenda ana stress (msongo wa mawazo). Hata
ikiwa hivyo, hakupaswa kutoa kauli nzito kama hiyo. Anatakiwa kufahamu
kuwa waraka huo umetoka kwa Wakristo wote hapa nchini,” alisema Askofu
Kilaini.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Bara, John Mnyika jana
alisema kitendo cha Sitta na wenzake kushindwa hata kuelewa waraka wa
viongozi wa dini na kuuita kuwa “hauna utukufu wa Mungu na wa kipuuzi”,
ni wazi wamelewa madaraka wasaidiwe kwa kupumzishwa.
Hata
hivyo, jana Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC) Father
Raymond Saba, amesema bado wanaendelea kutafakari kauli ya Sitta na
kwamba kwa sasa hawajatoa taarifa yoyote.
Akizungumzia kauli
ya Sitta, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Hamad Salim
alisema kauli ya kiongozi huyo imeongeza mpasuko wa dini nchini hasa
kuhusu mahakama ya kadhi.
“Viongozi wa dini wameipokea kauli
ya Serikali kwa kuwa tu alisema ni kiongozi wa Serikali, lakini
itatokea shida kama ahadi yao haitatekelezwa,” alisema Salim.
Sitta na Jaji Warioba Sitta amejikuta kwenye vita ya maneno na Jaji Warioba huku kila mmoja akisisitiza kuwa anafanya kazi aliyotumwa na wananchi.
Akizungumza
katika maadhimisho ya miaka 19 tangu kuanzishwa kwa Kituo cha Sheria na
Haki za Binadamu (LHRC) hivi karibuni, Jaji Warioba alisema ataingia
mitaani kuitetea Rasimu ya Katiba iliyokuwa imebeba maoni ya wananchi.
Alisema kuwa Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba imeondoa mambo manne muhimu.
Hata
hivyo, akizungumza jana na gazeti hili alisema kuwa Katiba hiyo imeacha
maswali mengi kuliko majibu hasa kwa upande wa Zanzibar.
Sitta alalamikia kutukanwa Sitta
atakuwa na kibarua kingine cha kujisafisha mbele ya wananchi ambao
alikaririwa akisema kuwa wamekuwa wakimtumia meseji za matusi za ya 50
kila siku.
Kwa nyakati tofauti wananchi wasiojulikana
wamekuwa wakiandika meseji za matusi kwenye mitandano na simu kwa kile
wanachosema kuwa Sitta amelazimisha maoni ya CCM yatawale Bunge.
Wananchi wasubiri waelezo zaidi Baadhi
ya wananchi waliohojiwa kuhusu mwenendo wa Bunge hilo, waliwalaumu
wajumbe wa Bunge waliokuwa wakisema walipiga kuwa kwa niaba ya wananchi
kwenye majimbo yao.
Walihoji ni lini wajumbe hao ambao ni
wabunge wao walikwenda kuwauliza iwapo wanataka kupiga kura ya hapana au
ndiyo dhidi ya Katiba iliyopendekezwa?
‘Mimi nimesikia tu
mbunge wetu (anamtaja) amesema wananchi wake wamechagua kura ya ndiyo.
Ni nani alimtuma kwenda kuwa tunataka Katiba hiyo wakati maoni yetu
tulitoa tofauti, “ Yohana Change mkazi wa Vwawa, Mbozi.
Mwanaidi
Suleiman alisema haelewi nini kilichotokea bungeni, kwa kuwa matarajio
aliyokuwa nayo kuhusu Katiba yameyeyuka baada ya kusikia mambo mengi
yamekataliwa.
“Nafuu kama wangeondoa mambo mengine, lakini
siyo serikali tatu na uraia wa nchi mbili. Mimi hayo niliyaona makubwa
sana, kama hayapo sasa Katiba itahusu nini?” alihoji Mwanaidi.
Chadema na wanachama wake. Hali
ya hewa ndani ya Chadema ilichafuka baada ya Sitta kusema kuwa kuna
wajumbe wawili wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutoka Zanzibar
walikubali kupiga kura kinyume na msimamo wa vyama vyao.
Sitta alisema kuwa kati ya wajumbe hao, mmoja alikubali kupiga kura na kusema yuko tayari hata kufukuzwa na chama chake.
“Sasa
wale wanaotumia mbinu za ovyoovyo ili mchakato huu usikamilike
wanapoteza muda, maana ukizuia maji huku, yanaelekea kwenye mkondo
mwingine,” alisema Sitta.
Taarifa hizo zilionekana kuwalenga
wabunge wa Viti Maalumu, Maryam Msabaha na Mwanamrisho Abama ambao kwa
nyakati tofauti walithibitishwa kutafutwa ili apige kura.
“Kweli
nimesumbuliwa sana na watu ambao siwezi kuwataja na wananitaka nipige
kura na wengine walifika mpaka nyumbani lakini mimi siwezi kushiriki
maana nikifanya hivyo dhamiri yangu itanishtaki,” alisema Msabaha.
Naye
Abama alisema kuwa alikuwa amepewa ilani na viongozi wake kwamba
anatafutwa ili akapige kura, hivyo aliamua kukaa ndani kukwepa mtego
huo.
Kauli hizo mbili tofauti zinauachia Ukawa maswali
magumu yanayohitaji majibu ili kubaini iwapo kuna usaliti wowote
umefanyika au la.
Wabunge wengine ambao wanaweza kukukumbana
na matatizo ndani ya chama hicho ni Mbunge John Shibuda (Maswa
Mashariki), Said Arfi (Mpanda Mjini) ambao walikiuka uamuzi wa Ukawa
kutoshiriki Bunge hilo.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod
Slaa jana alisema kuwa suala la wasaliti wa chama linatarajiwa
kuzungumzwa kwenye vikao vya ndani.
“Siwezi kulitolea uamuzi
suala hilo, baada ya kumaliza uchanguzi sasa litazungumzwa ndani ya
vikao vya chama na kutolewa uamuzi,” alisema Dk Slaa.
Aliyekuwa
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro alisema kuwa Sitta alipaswa
kuwataja wajumbe kutoka Ukawa waliokubali kupiga kura, lakini hakufanya
hivyo.
“Juzi amechukua kura zao na hawataji ni kina nani
wala walipiga kura kwa njia gani. Hata akijiongezea hizo kula mbili feki
bado BMK upande wa Zanzibar wanabakiwa na kura 145 tu na siyo 146,”
alisema Mtatilo.
Wanananchi waikataa rasimu Naye
Joseph Lyimo kutoka Manyara, amesema kuwa baadhi ya wakazi wa mkoani
humo, wamesema Bunge la Katiba limepitisha rasimu ya Katiba bila
maridhiano kwa baadhi ya wajumbe hivyo kusababisha hofu ya kupatikana
kwa katiba mpya itakayokidhi matakwa ya wananchi.
Wakizungumza
jana na mwandishi wa habari hizi, wananchi hao walidai kuwa rasimu hiyo
iliyopitishwa bungeni juzi haikukidhi maoni yaliyotolewa kwenye tume ya
Warioba kwani ibara 28 zimefutwa na kuwapo ibara mpya 42.
Mkazi
wa mji mdogo wa Mirerani, Abdalah Mtengeti alisema kwenye Tume ya
Warioba wananchi walipendekeza mbunge awe na ukomo wa madarakani kwa
miaka 15, lakini sasa wabunge hao wameridhia asiwe na mwisho wa utawala.
“Wananchi hawawezi tena kumwajibisha mbunge waliyemchagua
wao wenyewe kama walivyopendekeza awali pia hakuna ukomo wa mbunge tena
hivyo atatawala hadi mwenyewe aseme sigombei tena,” alisema Mtengeti.
Mwenyekiti
wa Bavicha Mkoa wa Manyara, Frank Oleleshwa alisema rasimu hiyo ya
wabunge haikujali maoni ya wananchi kwani walipendekeza kufutwa kwa vyeo
vya wakuu wa mikoa na wilaya lakini, wabunge wameridhia.
“Pia
wananchi walipendekeza kuwepo na Serikali tatu ikiwamo kurudisha
Tanganyika ili kuwapo na usawa wa nchi, lakini wabunge wamegoma hilo na
kuridhia Rais wa Zanzibar awe makamu wa pili wa Rais,” alisema
Oleleshwa.
CCM, CUF Zanzibar Naibu Katibu Mkuu
wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai
Ali Vuai walipozungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti visiwani
humo, Mazrui alisema kwamba mambo yaliyopitishwa na Bunge la Katiba
katika rasimu hiyo yanagongana na Katiba ya Zanzibar iliyofanyiwa
marekebisho mwaka 2010 ikiwamo suala la mamlaka ya ugawaji mikoa
aliyopewa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kushauriana na Rais wa
Zanzibar.
Alisema Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano
utekelezaji wake utakuwa mgumu kwa baadhi ya mambo Zanzibar mpaka Katiba
ya Zanzibar ifanyiwe tena marekebisho na kabla ya kufanyika hivyo
lazima kuitishwe kura ya maoni kwa wananchi.
Kwa upande wake
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema kwamba kama
viongozi wote watafanya kazi kwa kuzingatia sheria na katiba, Serikali
ya Umoja wa Kitaifa(SUK) haitoyumba kwa sababu hakuna mshindi wala
mshindwa baada ya rasimu ya katiba kupitishwa.
“Matokeo ya
kura ya rasimu ya katiba, ni ushindi wa wazanzibari wote na watanzania
kwa ujumla, na hakuna mshindi wala mshindwa” alisema Vuai ambaye pia
alikuwa mjumbe wa bunge maalum la katiba.MWANANCHI
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin