Kushoto ni mfanyabiashara Giluti Makula akishikana mkono na mwenyekiti wa kamati ya shule ya msingi Mapinduzi A Silvester Senga(kulia) baada ya kukabidhi madawati 22 kutokana na kuguswa na hali ngumu ya wanafunzi hao japokuwa iko mjini-Picha na Marco Maduhu-Malunde1 blog
Kushoto ni mfanyabiashara Giluti Makula akishikana mkono na Mwalimu mkuu wa shule hiyo Savera Rwabuyogo ambaye alisema wakati wa mitihani hulazimika kuazima madawati shule za jirani ili kutoa fursa za wanafunzi kufanya mitihani wakiwa wamekaa kwenye madawati.
Pamoja na jitihada zinazofanywa na serikali hapa nchini katika kuboresha elimu lakini shule nyingi bado zinakabiliwa na changamoto kadha wa kadha bila kujalisha kama ziko mjini au kijijini ,Hapa mjini Shinyanga wanafunzi wa shule ya msingi mapinduzi A iliyopo mjini Shinyanga wanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa madawati hali ambayo imetajwa kuwafanya wanafunzi kuumia migongo, kuwa na miandiko mibaya na wengine kuamua kuwa watoro shuleni.
Hali hiyo imebainikwa wiki hii baada ya shule hiyo kukabidhiwa madawati 22, yenye thamani ya shilingi milioni 2 na elfu tisini kutoka kwa mfanyabiashara wa usafirishaji abiria mjini Shinyanga, Giluti Makula.
Wakitoa shukrani kwa niaba ya wanafunzi wenzao, wanafunzi Real Shome na Emmanuel Sayi walisema uhaba wa madawati ndiyo kero kubwa shuleni hapo ambapo madarasa mengine hayana madawati kabisa huku wanafunzi wakikaa chini na kuumia migongo, na baadhi yao huamua kulala ili wapunguze maumivu.
“Kwa kweli tunaomba kuletewa madawati,hatuna madawati ndiyo maana miandiko yetu inakuwa mibaya ,tunaumia migongo, na baadhi yetu kuwa watoro na kushindwa kuhudhuria shuleni kutokana na kupata maumivu ya migongo”, walisema wanafunzi hao.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo Savera Rwabuyogo, alikiri wanafunzi hao kuumia migongo na kuwa watoro shuleni kutokana na uhaba huo wa madawati kuongeza kuwa wakati wa mitihani hulazimika kuazima madawati shule za jirani ili kutoa fursa za wanafunzi kufanya mitihani wakiwa wamekaa kwenye madawati.
Rwabuyogo alisema, shule hiyo hapo awali ilikuwa na madawati 147 kabla ya kuongezewa hayo 22, huku wanafunzi wakiwa 837 kuanzia darasa la kwanza hadi la saba, wasichana 433, wavulana 404, na wanafunzi.
Alisema kati ya wanafunzi hao 837 ambao hutumia madawati hayo ni Darasa la Saba ,na la nne huku wengine wakikaa chini.
Naye mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo ,Silvester Senga, alisema wazazi na walezi katika shule hiyo wamekuwa wagumu kuchangia miradi ya maendeleo na wanapoitwa kwenye vikao vya shule, wamekuwa hawa hudhurii na wanapowafautaili wamekuwa wakidai wanahali ngumu ya maisha.
Akizungumza baada ya kukabidhi madawati hayo mfanyabiashara Giluti Makula, alisema katika mawazo yake alikuwa anajua kuwa shule za mjini hazina tatizo la madawati, na mara baada ya kusikia risala iliyosomwa katika mahafari ya shule hiyo ya kuwaaga darasa la Saba Septemba 19,mwaka huu kuwa wanakabiliwa na changamoto ya madawati.
Makula alisema, siku ya mahafari hayo ya kuwaaga wahitimu wa darasa la saba, katika shule hiyo ambapo alikuwa mgeni rasmi alishanghaa kusikia shule ya Mpinduzi A, ambayo ipo mjini Shinyanga kuwa wanafunzi wanakaa chini na hivyo kuguswa na kutoa msaada huo wa madawati 22, ili kupunguza changamoto zinazowakabili wanafunzi hao.
Na Kadama Malunde-Shinyanga