WAJUKUU wa marehemu Sabina Ngalu(77),ambaye ni mama wa mwandishi wa habari wa kujitegemea Salum Maige anayeandikia magazeti ya Mwananchi,The Citizen na Radio Free Africa(RFA) ya jijini Mwanza wamejikuta wakicharazwa bakora eneo la makaburi muda mfupi kabla ya mazishi.
Kaburi la marehemu |
Tukio hilo la aina yake limetokea mwishoni mwa wiki iliyopita saa 5 asubuhi katika Kitongoji cha Nyamwanza kata ya Sima Wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza muda mfupi baada ya mwili wa marehemu kuwasili eneo la mazishi kwenye shamba lake ukitokea kanisa la Roman Catholic Parokia ya Yesu Kirsto Mfalme la mjini Sengerema.
Chanzo cha wajukuu hao zaidi ya 10 kuchacharazwa bakora ni utovu wa nidhamu waliouonyesha wa kung’ang’ania ndani ya kaburi lililokuwa limeandaliwa rasmi kwa ajili ya kuuhifadhi mwili wa marehemu Ngalu(77).
Sababu za wajukuu hao kung’ang’ania ndani ya kaburi hilo walitaka wapewe Ng’ombe mmoja au pesa taslimu Tshs 100,000,kwa mjibu wa mila na desturi za kabila la Kisukuma jambo ambalo lilipingwa na baadhi ya wanandugu waliodai mila hizo zilikwishapitwa na wakati na kuwataka watoke kaburini ili taratibu za mazishi ziendelee.
Baadhi ya wajukuu walioonja joto la jiwe ni pamoja na Andrea Mabula,Sabina Bukuru,Johari Bukuru,Asha Bukuru,Faida Bukuru,Yuves Petro,Semen pamoja na koiongozi wao Enos Ntilaga.
Hata hivyo wajukuu hao waligoma kutoka ndani ya kaburi hilo huku wakisisitiza kuwa wapo tayari kufa lakini si kutoka ndani ya kaburi hilo bila kupatiwa ng’ombe mmoja au kiasi hicho cha pesa.
Kitendo cha wajukuu hao kugoma kutoka ndani ya kaburi hilo,kilimchefua Padre Nicodemus Mayala ambaye pia ni Paroko wa Parokia ya Yesu Kristo Mfalme Sengerema Mwanza ambaye aliamua kuondoka eneo la maziko huku akitaarifu polisi kuhusiana na vurugu hizo.
Kufuatia hali hiyo,kaka wa marehemu Enosi Ngalu,aliyeonekana kukerwa na kitendo hicho alitafuta mkwaju(fimbo) ndefu kisha kutinga eneo lilipochimbwa kaburi hilo na kuanza kutembeza mkong’oto wa nguvu kwa wajukuu hao waliokuwa ndani ya kaburi hilo.
Kitendo ambacho kilizidisha hasira kwa wajukuu hao ambao wakiwa ndani ya kaburi walianza kujibu mapigo kwa kumrushia mchanga mjomba wao huyo ambaye alizidiwa ujanja na kuamua kusitisha zoezi lake la kutembeza bakora mithili ya katuni maarufu ya mzee kifimbo cheza wa gazeti la Sani na kutimua mbio.
WAOMBOLEZAJI WAKUBALI YAISHE
Kufuatia hali hiyo,mmoja wa waombolezaji aliamua kukubali yaishe baada ya kuona wajukuu hao walikuwa hawabipu kisha kuzama mfukoni na kutoa kiasi cha pesa walichohitaji wajukuu hao na kuwapa na ndipo walipokubali kutoka ndani ya kaburi hilo ili mazishi yaendelee.
PADRE AGOMA KUONGOZA IBAADA YA MAZISHI.
Ili kuonyesha alikerwa na kitendo hicho,Padre Mayara ambaye kwa wakati huo alikuwa amewekwa kitimoto na baadhi ya wanandugu wakimsihi kutosusia mazishi hayo mita 200 kutoka eneo la kaburi aligoma kurejea kaburini kuongoza ibada ya mazishi hayo.
‘’Hata kama wameshatoka ndani ya kaburi mie siwezi kurudi tena huko kuongoza ibada ya mazishi maana hili jambo limefanywa kinyume na taratibu za sisi wakristo maana haya ni mambo ya kipagani yalipaswa yafanywe kipagani’’alisikika Padre Mayala akitia ngumu.
BABA WA WATOTO AZIDI KUMWANGUKIA PADRE
‘’Ni kweli hili limeshafanyika tunaomba utusamehe baba paroko na sisi kama wazazi tunajua jinsi ya kuwawajibisha hawa watoto hawawezi kutushinda,cha msingi hapa ni wewe kusamehe hili lililotokea turudi kaburini ukaongoze misa ya mazishi tumsitili ndugu yetu maana saaa 2 zimepita jeneza linapigwa jua tunakuwa hatumtendei haki marehemu ambaye anapaswa kupumzika’’alisikika mmoja wa wanafamilia ya marehemu akimshauri Padre bila mafanikio.
PADRE ALEGEZA MASHARTI
Baada ya vuta nikuvute hatimaye Padre Mayala aliwataka wajukuu hao kurudisha pesa waliyochukua na kuwataka radhi wanamtaa huo na ndipo anaweza kurudi eneo la kaburi kuongoza ibada ya mazishi kinyume na hivyo alisisitiza asingeweza kufanya hivyo kwani kitendo hicho kimekiuka misingi ya dini nyao.
WAJUKUU WAKUBALI KWA SHINGO UPANDE KURUDISHA PESA
Kutokana na hali hiyo wajukuu hao waliitwa mbele ya Padre na mbele ya wanamtaa huo kisha waliomba samahani ikiwa ni pamoja na kurudisha pesa hiyo kwa aliyekuwa ameitoa na ndipo Padre aliporejea eneo la kaburi na kuongoza ibada ya mazishi.
POLISI WATINGA MAKABURINI
Majira ya saa 6:30 polisi zaidi ya wane kutoka kituo cha Sengerema wakiwa na bunduki aina ya SMG,na zile za mabomu ya machozi walifika eneo hilo kufuatia simu iliyokuwa imepigwa na Padre Mayala wakati vurugu hizo zikiwa zimepamba moto.
Baada ya polisi kufika eneo hilo walimkuta Padre Mayala akiendelea na ibada ya mazishi na wao wakaweka kambi kwa muda huku wakizungukazunguka eneo hilo na baadaye waliondoka baada ya kuona hali iko shwari eneo la mazishi.
TIMBWILI LAHAMIA NYUMBANI KWA MAREHEMU
Majira ya saa 7:15 baadaa ya kutoka makaburini wajukuu wale waliwahi nyumbani kwa marehemu Mtaa wa Mlimani Kata ya Nyatukala Wilayani Sengerema kisha kuanzisha timbwili jingine kwa kuficha chakula na vyombo vya kupakulia wakidai warudishiwe pesa yao waliyokuwa wameirejesha makaburini kwa shinikizo la baba paroko.
‘’Leo hali mtu hapa,mmetucharaza bakora na pesa yetu mkatunyang’anya sasa tuko tayari kupigwa mpaka mtuuwe lakini chakula hakitoki hapa au la sivyo mturudishie pesa yetu’’alisikika Enos Ntilaga mjukuu wa marehemu akichimba biti huku akiwa anahamisha masufuria ya chakula kwa kushirikiana na wenzake na kwenda kuyaficha.
MMOJA WA WAOMBOLEZAJI AOKOA JAHAZI
Baada ya timbwili hilo kukolea kama moto kwenye majani makavu,mmoja wa wafiwa alizama mfukoni kisha kutoa kiasi cha fedha kilichotakiwa na kuwakabidhi wajukuu hao ambao walirudisha chakula jikoni na taratibu za ndugu za jamaa na marafiki wa wafiwa kupata chakula ziliendelea huku baadhi ya wafiwa wakiwa tayari wameamua kuondoka na kwenda kutafuta chakula mahotelini akiwemo Maige ambaye ni mtoto wa marehemu na waandishi wengine wa habari waliofika kumlaki likiwemo0 gazreti hili .
YABAINIKA WENGINE WALIKUWA WAJUKUU FEKI
Mtoto wa marehemu, Maige ambaye ni mwandishi wa habari akizungumzia tukio hilo alidai kuwa,si wote walioanzisha timbwili hilo ni wajukuu wa marehemu mama yake bali na vijana wa kihuni waliingilia sakata hilo.
‘’Kama huyo unayemuona pale(huku akimuonyesha mwandishi wa habari)si mwanafamilia wala si mjukuu wa marehemu mama ni mhuni tu na sijui hata alikotokea naona atakuwa mzamiaji wa chakula’’alisema Maige kwa masikitiko.
KAKA WA MAREHEMU AAHIDI KUWASHUGHULIKIA
Kwa upande wake kaka wa marehemu aliyewacharaza bakora wajukuu hao,alidai kuwa wanasubilia siku arobaini ziishe waitishe kikao cha ukoo kwa lengo la kuwawajibisha wale wote waliozua tafrani msibani.
MWENYEKITI WA ENEO APIGWA BUTWAA
Mwenyekiti wa mtaa huo wa Mlimani aliyekuwa eneo hilo,Joseph Numbuyamwana alishangazwa na hatua hiyo huku akiwasihi wale wote wanaokusudia kufanya vitendo hivyo nyuma ya pazia la kimila wafanye kwa kuangalifu kuepuka kuwakwaza viongozi wa dini kama ilivyotokea kwenye msiba huo.
Na Victor Bariety-Malunde1 blog Sengerema
Social Plugin