Wananchi Mkoani Geita wametakiwa kuacha mara moja tabia ya kuwaua vikongwe kwa imani za kishirikina na kuacha kujichukulia sheria mikononi kwani kufanya hivyo wana kwenda kinyume na mapenzi ya Mungu.
Kauli hiyo imetolewa jana na Askofu wa kanisa la Habari Njema Tryphone Siku wakati wa kufungua mkutano wa siku tano katika viwanja vya shule ya msingi Kalangala vilivyoko mjini Geita lengo likiwa ni kuwaombea watu kuacha dhambi na kumrudia mwenyezi Mungu.
Askofu Siku alisema watu wa mkoa huo wamekuwa wakiwaua vikongwe kwa imani za kishirikina na kujichukulia sheria mikononi kwa kuwaua wahalifu hivyo kuwaomba kuacha mara moja kwani wanakwenda kinyume na mapenzi ya Mungu na kuwataka, waganga wanaopiga ramli chonganishi nao kuacha.
Alisema viongozi wa serikali wa mkoa wa Geita kwa kushirikiana na mkuu wa mkoa huo Said Magalula wamekuwa wakijitahidi sana kuwaelimisha wananchi kuacha tabia hizo kwa kushirikiana na makanisa likiwemo kanisa lake.
"Jamani acheni kuwaua vikongwe kwa imani za kishilrkina na kujichukulia sheria mikononi na nyinyi waganga acheni kuwachonganisha watu kwa kuwapigia ramli za uwongo"alisema Siku.
Naye Mchungaji wa kanisa hilo Alex Mshindi kutoka nchini Rwanda alishukuru wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye mkutano huo lakini akawaomba wakazi wa mkoa wa Geita kwa ujumla kumrudia aliyewaumba na kuacha matendo maovu.
"Nimeshangazwa na mauaji ya vikongwe na kujiochukulia sheria mikononi ninavyosikia hapa Mkoani kwenu, jamani acheni tabia hizo lakini tushirikiane kuwaombea wanaofanya hivi waache na wamrudie muumba wenu",alisema mchungaji Alex.
Na Valence Robert-Malunde1 blog-Geita