MBONA majanga! Mrembo aliyejitambulisha kwa jina la Latifa Abdallah (19), mkazi wa Kinondoni –Mkwajuni, Dar amesimulia alivyotekwa na watu aliodai ni wachuna ngozi wakiwa na mwanamke aliyevalia kininja ndani ya gari jeusi.
Akizungumza na waandishi wa habari hizi jijini Dar, juzi, Latifa alidai Oktoba 19, mwaka
huu akiwa anatoka kumsindikiza dada yake aliyekuwa akienda Kibaha, Pwani
ghafla msichana aliyevalia kininja akajigonga kwenye mwamvuli
alioushika na kumwambia alimgonga kwa makusudi.
“Nilimwomba msamaha na kumwambia ni bahati mbaya lakini alinikamata na
kuniingiza ndani ya gari jeusi lililopaki kando ya barabara ambapo kuna
mtu alifungua mlango yule mwanamke akanisukumia ndani,” alisema Latifa.
Akizidi kusimulia, binti huyo alisema kuwa, ndani ya gari hilo alimkuta
msichana mmoja kama yeye na mtoto kama wa miaka miwili wakiwa wamefungwa
vitambaa vyeusi machoni na yeye akafungwa kama wenzake.
“Tulikwenda kushushwa kwenye nyumba moja sijui ni wapi, tukaingizwa
katika chumba kidogo na kufunguliwa vitambaa. Ndipo nilipogundua kuwa,
watekaji wote walivaa kininja. Mmoja alikuwa mwanaume, mwingine ndiyo
yule aliyenisukumia ndani ya gari pale kwenye Kituo cha Daladala cha
Vijana Kinondoni (Dar).
“Yule mwanaume alisema lazima tufanye naye mapenzi la sivyo atatufanya
kama watakavyomfanyia yule mtoto.
Wakamchukua yule mtoto na kumchoma
sindano, alilia sana kisha akanyamza ghafla huku ngozi yake ikiumuka
kama puto. Yule mwanaume alitoa kisu na kuanza kumchuna ngozi yule mtoto
akianzia shingoni.
“Nikiwa katika hali ya kutetemeka kwa woga, yule mwanamke alisema
tujiandae na kifo kama cha yule mtoto. Nilimwomba Mungu sana atuepushie
kifo hicho.
“Siku ya Jumanne asubuhi wale watu walikuja kutuangalia kidogo na
kuondoka. Baadaye jioni walirudi na kutupa maji ambayo hatukuelewa ndani
yake yalikuwa na nini, walitunywesha na kutuambia kesho yake
wangeturudisha makwetu, wakachukua namba za simu za ndugu zetu,
sikuamini nikawatajia namba ya mwalimu wangu wa cherehani ambaye
waliniambia akipokea nimwambie kuwa mimi ni mzima nitafika nyumbani
kesho kutokea Kawe jambo ambalo nililifanya.
“Kuanzia hapo yule mwanamke akawa anachati naye. Wakati huo yule
mwenzangu kwao ni Mbezi naye aliwataarifu ndugu zake na tukawa
tunasubiri kesho ifike. Kweli, kesho yake wakatuchukua, mimi nikashushwa
pale Kituo cha Daladala Kinondoni–Studio (Dar), wakanipa shilingi 1,000
wakasema nipande bodaboda nirudi nyumbani,” alisema Latifa.
Mwalimu wa cherehani wa Latifa, Celestine ‘Baba Mkanji’ alisema tangu
Latifa atoweke nyumbani amekuwa akipigiwa simu na kutumiwa meseji
zinazoonesha Latifa alikuwa kwenye hali ya hatari jambo lililomshtua na
kuwashirikisha ndugu zake nao wakaripoti Kituo cha Polisi cha
Mzambarauni, baadaye Kituo cha Polisi cha Oysterbay jijini Dar.
Baada ya kurudishwa nyumbani, Latifa alipelekwa Oysterbay Polisi kwa
ajili ya kupata PF3 na baadaye kwenda Hospitali ya Mwananyamala kwa
ajili ya vipimo zaidi.
Naye mama mzazi wa Latifa, Habiba Saidi (56) alisema amesikitishwa na kitendo alichofanyiwa mwanaye na kuomba watu wa haki za binadamu na wanasheria wamsaidie ili waliomfanyia mambo hayo mwanaye wakamatwe.
Na Chande Abdallah na Deogratius Mongela