HOFU YA EBOLA YATANDA HUKO SENGEREMA,BINTI AZIKWA KI EBOLA EBOLA




Watu sita wakiwamo wahudumu watatu wa afya wa hospitali teule ya Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, wamewekwa chini ya uangalizi maalum baada ya kumhudumia mgonjwa aliyefariki akiwa na dalili za ugonjwa wa ebola.

Mtu aliyefariki alitajwa kuwa ni Salome Richard (17), anayetoka katika kijiji cha Kahunda wilayani Sengerema mkoani Mwanza.

Akithibitisha kuwapo kwa hali hiyo Mganga Mfawidhi wa Hospitali Teule ya Wilaya ya Sengerema, Dk. Mary Jose, alisema mgonjwa huyo alifikishwa katika hospitali hiyo na ndugu zake watatu akiwa na homa kali huku akitokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili wake.Alisema vipimo vya mgonjwa huyo vimepelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa uchunguzi zaidi.

“Tulimpokea juzi saa 7 mchana kutoka katika kijiji cha Kahunda wilayani hapa akiwa na homa kali akitokwa damu mwilini, lakini kwa tahadhari tulimweka wodi maalum peke yake akipatiwa matibabu na ilipotimu saa 8 usiku alifariki dunia,” alisema

Alisema kutokana na tahadhari ya ugonjwa huo, watumishi watatu wa idara ya afya na ndugu watatu wa marehemu huyo, wamezuiliwa kwa kuwekwa katika uangalizi maalum hadi matokeo ya vipimo vilivyochukuliwa vitakaporejeshwa toka Muhimbili.

Akizungumzia tukio hilo, muuguzi Mfawidhi wa hospitali hiyo, Daniel Mihayo, alisema timu maalum ya watalaam na viongozi wa mkoa walienda hospitalini hapo juzi na kuondoka na vipimo vya mgonjwa huyo kabla hajafariki dunia kwa kuzingatia maelekezo ya serikali ya kuchukua tahadhari linapotokea tukio kama hilo.

“Kwa sasa jamii inatakiwa kuepukana na uzushi uliozagaa kila kona kuhusu mgonjwa huyo kufariki kwa ebola…tunawamba wasiwe na wasiwasi kwani hatua stahiki zinachukuliwa kwa wagonjwa wa aina hiyo kama tahadhari,” alisema Mihayo.

Mhudumu aliyempokea mgonjwa huyo katika hospitali hiyo, Fungameza Majula, alisema ndugu watatu walimpeleka mgonjwa huyo kwa taksi lakini alipobaini dalili hizo aliujulisha uongozi wa hospitali na mara moja hatua za tahadhari zilichukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwazuia ndugu kurudi nyumbani.

Hata hivyo, juhudi za kumpata mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Careen Yunusu, kuzungumzia tukio hilo hazikufanikiwa.

Akizungumzia tukio hilo, Mganga mkuu wa mkoa wa Mwanza, Bw.Valentino Bangi, alisema alipokea taarifa za mgonjwa huyo kufariki kwa homa inayofanana na ugonjwa wa ebola au maburgh.

Bw.Bangi alisema ofisi yake imetuma timu ya wataalam wa afya katika Hospitali ya Wilaya Sengerema na kuchukua sampuli ya vipimo vya mgonjwa na kupeleka Muhimbili kwa uchunguzi zaidi.


Bw.Bangi alisema ili kukabiliana na mlipuko wa magonjwa hayo, tayari taifa, uongozi wa mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na ofisi yake, wameweka vituo vya kupima magonjwa katika mipaka ya Sirari, Mutukula na uwanja wa Ndege wa Mwanza

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post