Imani potofu imetajwa kuwa ni chanzo cha baadhi ya wananchi kushindwa kutumia vyandarua vya kuzuia malaria vinavyotolewa na serikali kupitia wizara ya afya na ustawi wa jamii,kutokana na madai kuwa vimeletwa ili kupanga uzazi na kupunguza idadi ya watu.
Hayo yalisemwa wiki hii na mwenyekiti wa bodi ya hospitali ya rufaa mkoa wa Shinyanga Wilson Majiji kwenye kikao cha kuhamasisha chanjo ya surua rubella na malaria,ambapo alisema elimu zaidi inahitajika kuendelea kutolewa ili kubadili mtazamo uliojengeka miongoni mwa watu huku wengine wakidai zinapunguza nguvu za uzazi.
Aliwataka wananchi kuupuuza uvumi huo kwani serikali ya Tanzania ina nia nzuri na wananchi wake, katika kutaka kutokomeza ugonjwa huu wa malaria pamoja na kupunguza vifo vya wajawazito na watoto vitokanavyo na malaria.
“Hii ni changamoto kubwa na inabidi wataalam wajipange katika kutoa elimu kwani watu wengine wanasema wakipewa chanjo wanapunguza kizazi badala ya kuzaa watoto watano wanaweza kuishia wawili pia baadhi yao wanaamini huu ni mkakati wa serikali wa kupunguza idadi ya watu kupitia vyandarua hivyo na chanjo ”alisema Majiji.
Naye mratibu wa zoezi la ugawaji wa vyandarua katika kaya nchini kutoka wizara ya afya na ustawi wa jamii Yusufu Mwita,alisema zaidi ya asilimia 93 ya wananchi wanaishi kwenye maeneo yenye maambukizi ya malaria. Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 za Afrika na sehemu kubwa ya watu wake wapo hatarini kuambukizwa malaria.
Hata hivyo aliongeza kuwa katika kukabiliana na ugonjwa wa malaria wizara ya afya inatarajia kugawa vyandarua million 22.3 katika mikoa 22 ya Tanzania bara na kwamba utekelezaji utafanyika kwa kutumia mifumo ya serikali iliyopo kwa kushirikiana na wadau ambapo lengo ifikapo mwaka 2020 asilimia 85 wawe wanatumia vyandarua vyenye viuatilifu vya kudumu ili kujikinga na malaria.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Shinyanga Ally Rufunga aliwataka wananchi watakaopatiwa vyandarua hivyo kuvitumiakwa matumizi yaliyokusudiwa, ili kukabiliana na ugonjwa hatari wa malaria hususani kwa akina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano badala ya kuvitumia kufugia kuku na kuvulia samaki.
Kampeni ya kitaifa ya chanjo ya surua na rubella itazinduliwa rasmi Oktoba 18 hadi 24 mwaka huu kitaifa mkoani Dodoma,ambapo ugonjwa huo wa rubella ni hatari na dalili zake zinafanana na za surua na kwamba chanjo yake inaitwa surua rubella itakayotumika kukinga magonjwa mawili.
Na Kadama Malunde-Shinyanga