Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

INATISHA!! WANAFUNZI WATAFUNWA NA MAMBA WAKIOGA MTONI HUKO TARIME

WANAFUNZI wawili wa shule za msingi za Nyabisara (Murito) na Kerende Kata ya Kemambo wilayani Tarime, Mara wameumwa hadi kuondolewa nyama zao za miguu na mamba walipokwenda kuoga maji ya mto kwa nyakati tofauti.

Wanafunzi hao ni Penina Joseph Mangure  (11) wa darasa la nne Shule ya Msingi Nyabisara katika Kijiji cha Murito ambaye ni mtoto wa mwenyekiti wa kijiji hicho, Joseph Mangure na Stephano Stephano (11) pia wa darasa la nne Shule ya Msingi  Kerende.

Taarifa za wanafunzi hao kukutwa na mkasa huo zilifikishwa katika Kituo cha Polisi Nyangoto (Nyamongo) na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Tarime na Rorya, Lazaro Mambosasa.
Akizungumza hivi karibuni, baba  wa Penina alisema mwanaye  aliokolewa na wananchi baada ya kupiga kelele wakati akiwa ameshikilia nyasi zilizomsaidia kushindwa kutumbukizwa majini na mamba huyo ambaye alikwenda na kipande cha nyama ya mguu wa kushoto.

Kwa upande wake mtoto Stephano alidaiwa kukutwa na tukio hilo alipokuwa akioga maji ya mto huo wakati akichunga ng’ombe wa nyumbani kwao.

Mtoto huyo alifanikiwa kuokolewa na wasamaria wema alipokamatwa na mamba huyo baada ya kupiga kelele na kufanikiwa kumtoa mguu katika mdomo wa mamba lakini akiwa ameshamnyofoa kipande cha nyama mguu  wa kushoto pia.

Mwenyekiti huyo alisema tangu Januari hadi Oktoba mwaka huu, watu watano wa kijiji chake wameshapoteza maisha baada ya kuliwa na mamba kwa nyakati tofauti huku wengine takribani 100 wakijeruhiwa.
Pia mwenyekiti huyo alisema mto huo kupita katika makazi ya watu ni tatizo na kwamba kila mara wananchi wanapopatwa na adha hizo huwasilisha taarifa katika Halmashauri ya Wilayani Tarime kupitia kitengo cha wanyama pori kwa ajili ya kusubiri hatua zaidi.

Alimuomba Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyarandu kuhakikisha inawafidia wote waliojeruhiwa au kupotezewa maisha na mamba hao.
  Watoto hao bado wanasota majumbani mwao baada ya tiba ya awali huku wazazi wao wakitafuta fedha ili wapelekwe Hospitali ya Bugando, Mwanza

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com