Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Shinyanga Khamis Mgeja(pichani) amesema kitendo cha Umoja wa katiba ya Wananchi (UKAWA) kutangaza kusimamisha mgombea mmoja kuanzia ngazi ya mitaa hadi uchaguzi mkuu ili kuiangusha CCM ni ndoto za mchana na kwamba hiyo ni dalili za kufirisika kisera na kuchanganya wananchi.
Mgeja aliyasema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa harambee kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya wazazi katika kituo cha Afya kata ya Kambarage manispaa ya Shinyanga ambapo mgeni rasmi alikuwa naibu waziri wa nishati na madini Stephen Masele ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Shinyanga mjini kupitia CCM.
Alisema kitendo cha vyama vya siasa vya upinzani nchini kuungana kusimamisha mgombea mmoja ili kuiangusha CCM ni dalili za vyama hivyo kupoteza mwelekeo wa ki sera na kuwachanganya wananchi washindwe kuelewa ni ilani au sera ipi itakuja kutekelezwa na vyama hivyo.
“Hii ni dalili ya watu hawa kufirisika ki sera,tunaweza kusema kuwa arobaini yao ni safari hii kwamba sasa wametoka kwenye biashara ya jumla sasa wanaelekea kufanya biashara ya reja reja,wananchi watashindwa kuelewa kwamba wanafuata sera ya chama kipi,ili watakapokosea wananchi wawasute”,alisema Mgeja.
“Mimi nafikiria mwisho wao umeshafika,wanatudhihirishia kuwa wameishiwa,wamefirisika ndiyo maana wameamua wakusanye nguvu kuliangusha gogo kitu ambacho hakitawezekana,Kwa kweli sasa Chadema,Cuf,NCCR Mageuzi Kushnei!! Kwisha kabisa!!”,aliongeza Mgeja.
Alisema CCM imefanya mambo makubwa chini ya rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuwaletea maendeleo wananchi katika sekta mbalimbali badala ya wapinzani ambao wao ajenda yao ni matusi na kubeza mafanikio yaliyofikiwa na CCM.
“Tunahitaji kuzungumza maendeleo,tusigeuze Shinyanga kama kituo cha watu kuja kutukana,atakuja hapa Freeman Mbowe,atakuja Dr Wilbroad Slaa,atakuja Tundu Lisu na matusi yao,hawaleti hata mfuko mmoja wa saruji,lakini Wanashinyanga tutakesha tunashabikia oooh! Unaona bwana hili jembe,sisi hata majembe ya matusi yanapongezwa”,alisema Mgeja.
Katika hatua nyingine alimpongeza diwani wa kata ya Kambarage kupitia Chadema Nyangaki Shilungushela kwa kuendesha siasa za kistaarabu bila matusi huku akiwataka viongozi wengine wa Chadema kuiga mfano wake kwani kinachotakiwa ni ushirikiano kuwaletea maendeleo wananchi.
“Kituo hiki cha afya kiko katika kata inayoongozwa na Chadema,lakini ndugu yangu Shilungushela siasa zake za kistaarabu sana,angekuwa mwingine matusi yangetawala,lakini kakubali kushirikiana na mbunge kuwaletea maendeleo wananchi,kwani kituo hiki kinatumiwa na watu wote bila kujali huyu ni wa CCM,CUF au Chadema”,alieleza Mgeja.
Katika harambee ya kuchangia ujenzi wa wodi ya wazazi kituo cha afya cha Kambarage CCM mkoa wa Shinyanga walichangia mifuko 20 ya saruji,huku mbunge wa jimbo la Shinyanga mjini Stephen Masele na rafiki zake wakichangia shilingi milioni 45.
Wadau mbalimbali wajitokeza wakiongozwa na mbunge Masele aliyekuwa mgeni rasmi katika changizo hilo na kufanikiwa kukusanya shilingi milioni 115 ikiwa ni zaidi ya asilimia 100 ya pesa zilizokuwa zinahitajika shilingi milioni 105.
Na Kadama Malunde-Shinyanga