Watu saba wameuawa kwa kuchomwa moto ndani ya nyumba katika tukio ambalo nyumba 18 ziliteketezwa na mbili kubomolewa na wananchi waliodai wanawaua wachawi katika Kijiji cha Murufiti, Kasulu, mkoani Kigoma.
Polisi wameeleza kuwa tayari watu 17 wamekamatwa kwa kuhusika kwenye tukio hilo.
Miongoni mwa waliouawa katika tukio hilo lililotokea Jumatatu iliyopita ni John Mavumba (68) na mkewe Elizabeth Kaje 55 ambao pamoja na wenzao walikuwa wakituhumiwa kuwa ni washirikina.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Josephat John ambaye ni mtoto wa Mavumba, alisema wazazi wake walichomwa moto na kundi la vijana waliokuwa wakiwatuhumu kuwa ni wachawi.
Alisema vijana walikuwa wamebeba mapanga, marungu na kupita katika nyumba mbalimbali wakifanya mauaji wakisema maneno kwa kurudiarudia kwamba watawamaliza wachawi kwa kuwaua, ndipo yeye na wenzake walikimbia usiku huo wakihofia kuuawa.
“Niliporudi alfajiri niliukuta mwili wa mama ukiwa umbali wa mita 10 kutoka ilipo nyumba yetu ukiwa umeungua na mwili wa baba ukiwa umeungua ndani ya nyumba,” alisema John.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Jafari Mohamed alisema mauaji hayo yalitokea Oktoba 6 kuanzia saa 4:00 usiku katika kijiji hicho.
John alisema baada ya tukio hilo wanaume wengi wameyakimbia makazi yao wakihofia kuuawa na kundi la vijana hao. “Kijiji kimebaki na wanawake tu, wanaume wamezikimbia nyumba zao wanahofia kuuawa,” alisema.
Mohamed alisema mauaji hayo yametokana na imani za kishirikina.
Aliwataja waliouawa kuwa ni John Muvumba (68), Elizabeth Kaje (55), Dyaba Kitwe (55), Vincent Ntiyaba (42), Herman Ndabiloye (78), Redempta Mdogo (60) na Ramadhan Kalaliza (70) wote wakazi wa kijiji hicho.
Alisema nyumba zilizochomwa moto ni 18, mbili zilibomolewa na kufanya jumla ya nyumba 20 zilizoharibika kabisa.
Wakazi wa kijiji hicho, Zablon Andrew na Eveline Enock walisema kwa nyakati tofauti kuwa chanzo cha mauaji hayo ni mganga wa jadi aliyefika kijijini hapo na kupiga ramli akiwataja watu waliouawa kuwa ni wachawi.
Andrew alisema baada ya mganga huyo kuwataja, vijana walikusanyana na kuanza kuwateketeza watu bila huruma.
“Kitendo hiki kimeturudisha nyuma kimaendeleo kwa sababu nyumba zetu zimechomwa moto na mazao yetu yameharibiwa,” alisema Andrew.
Hali ilivyo kijijini
Mmoja wa watu aliyechomewa nyumba, Evelyne Msilu alisema sasa kijiji hicho kina askari wengi wanaofanya doria.
“Hali inasikitisha, tumepoteza ndugu zetu waliouawa, wanaume wengi wamekikimbia kijiji kwa hofu ya kuuawa na vijana wengine wamekimbia wakiogopa kukamatwa,” alisema.
Kwa nini ipigwe ramli?
Akisimulia, Enock alisema kuna kijana mmoja katika kijiji hicho ambaye kazi yake ni kufyatua matofali aliwaomba vijana wanzake kuwa siku inayofuata wamsaidie kuyapanga katika tanuru.
Alisema jambo la ajabu ni kwamba walipoamka asubuhi walikuta matofali yamekwishapangwa na haikujulikana aliyefanya kazi hiyo.
Alisema kijana huyo na wenzake waliamini kwamba waliofanya kazi hiyo ni wachawi.
Akisimulia kisa kingine, Enock alisema siku chache zilizopita kuna msiba ulitokea kijijini hapo na baada ya mazishi, siku iliyofuata walikuta msalaba umeng’olewa na haujulikani ulipo, jambo ambalo pia lilihusishwa na ushirikina.
Ofisa mtendaji wa kijiji hicho, Ogen Gasper aliyeomba Serikali kujenga kituo cha polisi kijijini hapo, alisema baada ya kupata taarifa za tukio hilo alifanya jitihada kubwa kuwapata askari, lakini hawakufika kwa kilichodaiwa ni kukosa usafiri.
Gasper alisema hilo ni tukio la tatu kwa watu kuuawa kwa kutuhumiwa kuwa ni wachawi, la kwanza likiwa limetokea mwaka 1996.
via>>Mwananchi
Social Plugin