Mtoto wa kike wa miaka 13 aliyenajisiwa na mwajiri wake, ameeleza kuwa alimtaarifu mke wa mtuhumiwa kuhusu vitendo hivyo, lakini wawili wakasameheana na kumtaka asiwaambie watu.
Inadaiwa kuwa mtoto huyo aliyekuwa akifanya kazi za ndani maeneo ya Bunju B, jijini Dar es salaam alibakwa zaidi ya mara tatu na mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 35.
Mtoto huyo, ambaye kwa sasa amelazwa Hospitali ya Mwanayamala, alichukuliwa kutoka Bukoba alikokuwa akiishi na baba yake.
Akihojiwa na Rose Temu, ofisa wa Ustawi wa Jamii wa Hospitali ya Mwananyamala, mtoto huyo alisema mwajiri huyo alikuwa akimtendea vitendo hivyo kwa nyakati tofauti, mara ya mwisho ni Jumapili iliyopita.
Alisema alifika Dar es Salaam Novemba mwaka jana akitokea Bukoba baada ya kuacha shule akiwa darasa la tano na kuchukuliwa na mtu huyo kwa makubaliano na baba yake ya kuja kufanya kazi za ndani.
“Baada ya kuishi kwa muda, siku moja usiku alinivizia na kuniingilia kinguvu, kisha akaniambia nisiseme. Lakini nilimwambia mkewe na alipomuuliza, bosi alikataa na kusema mimi muongo,” alisema.
Mara ya pili aliponifanyia mama alitukuta, akamuuliza ‘unamfanya nini mtoto wa watu’, akajibu ‘namchezea’.
Wakaingia ndani baadaye mama akasema ameomba msamaha na hatarudia tena hivyo nisiwaambie watu,” alisimulia.
Mtoto huyo alisema anataka kurudi kwa baba yake kuendelea na shule, lakini atafanya hivyo baada ya kulipwa Sh160,000 anazomdai za malimbikizo ya mshahara.
Ofisa huyo alisema wamempokea mtoto huyo kutoka kwa polisi Jumanne na tayari ameshafanyiwa vipimo mbalimbali.
Alisema atakuwa chini yao hadi watakapowasiliana na wazazi wake.
Alisema atakuwa chini yao hadi watakapowasiliana na wazazi wake.
Mjumbe wa Mtaa wa Bunju B, Josephat Rutayuka alisema Jumapili ya saa 12:00 asubuhi, mtoto alikwenda kumlalamika kuhusu vitendo viovu.
Na Daria Erasto-Dar es salaam