Kuna mjadala wa muda mrefu kuhusu suala la nyama nyekundu, ambapo makundi mawili tofauti yamekuwa yakitoleana hoja kuhusu faida na madhara ya kula nyama, hasa ile nyama iliyowekwa katika kundi la ‘nyama nyekundu’ (red meat).
Wakati wakereketwa wa masuala ya afya wanasema kuwa nyama nyekundu huchangia hatari ya mtu kupata ugonjwa wa moyo na saratani ya tumbo, wadau wa nyama wanadai kuwa hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya saratani, ugonjwa wa moyo na nyama nyekundu.
Wakereketwa wa masuala ya afya wanaeleza kuwa ukweli uko wazi kwamba nyama nyekundu inaweza kusababisha ugonjwa wa moyo kwa mtumiaji, kwani baadhi ya nyama nyekundu huwa na kiwango kikubwa mafuta (saturated fat) ambayo huongeza kolestro mwilini na mtu mwenye kiwango kikubwa cha kolestro huwa hatarini kupatwa na ugonjwa wa moyo.
Kwa upande wa saratani, watafiti wanasema kuwa bado hakujawa na ushahidi wa moja kwa moja kuwa nyama nyekundu inaweza kusababisha saratani ya tumbo. Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na Taasisi ya Afya ya Taifa nchini Marekani, umebaini kuwa watu wanaopenda kula kwa wingi nyama nyekundu, hufa mapema kuliko wale wanaokula kiasi kidogo cha nyama hiyo.
Wapenda nyama ambao wako kwenye hatari kubwa ya kupatwa na saratani na ugonjwa wa moyo ni wale wanaokula kuanzia kiasi cha gramu 112 za nyama (karibu robo kilo) kila siku, lakini wanaokula kiwango kidogo (nusu ya robo kilo) hawako hatarini na badala yake watapata virutubisho muhimu vinavyopatikana kwenye nyama.
Ulaji wa nyama nyekundu wenye faida kwa mwili wa binadamu ni ule unaozingatia kiasi na aina ya nyama. Nyama inayopendekezwa ni steki isiyo na chembe ya mafuta (lean meat) na itakayoliwa kwa kiasi kidogo.
Nyama inahitajika kiafya kwasababu ina madini ya chuma ambayo ni muhimu kwa wasichana na wanawake wanaotarajia kuzaa. Pia nyama ina Vitamini B12 ambayo husaidia utengenezaji wa DNA na hujenga mishipa na seli za damu. Halikadhalika kuna madini ya zinki ambayo husaidia kuimarisha ufanyaji kazi wa kinga ya mwili. Bila kusahau nyama ina protini ambayo ni muhimu kwa ujenzi wa mifupa na misuli.
JE, NGURUWE NI NYAMA NYEKUNDU?
Kumezuka swali pia kama nyama ya nguruwe nayo iko kwenye kundi la nyama nyekundu, kwani kimuonekano ni nyeupe.
Jibu ni kwamba nyama ya nguruwe nayo ni nyekundu.
Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo ya Marekani, kiwango cha protini aina ya ‘myoglobin’ kilichomo kwenye misuli ya nyama yoyote ndicho kinachoonesha aina ya nyama. Nyama ya nguruwe inahesabika kuwa ni nyekundu kwa sababu kiwango chake cha ‘myoglobin’ ni kikubwa kuliko kile kilichomo kwenye nyama nyeupe za kuku na samaki.
Kwa ujumla, nyama nyekundu ni muhimu kwa afya ya binadamu, lakini itakuwa muhimu kama itatumiwa kwa kiwango na kiasi kinachotakiwa. Siku zote epuka kula nyama yenye mafuta na badala yake pendelea kula steki isiyokuwa na mafuta ili upate virutubisho vyake muhimu kwa afya yako.
Kula nyama kinyume na mwongozo huu, ni sawa na kuamua kujiweka katika hatari ya kupatwa na ugonjwa wa moyo na matatizo mengine ya kiafya, ikiwemo ugonjwa wa miguu au kansa ya tumbo. Jiepushe na hayo kwa kuzingatia masharti ya ulaji sahihi.
Bonyeza Maneno haya Tukutumie Habari zetu zote moja kwa moja hapo ulipo
Bonyeza Maneno haya Tukutumie Habari zetu zote moja kwa moja hapo ulipo
Social Plugin