Madiwani katika manispaa ya Shinyanga wametakiwa
kutimiza wajibu wao kwa kusimamia ipasavyo miradi mbalimbali ya maendeleo
badala ya kuogopa kupoteza nyadhifa zao katika chaguzi zijazo endapo
watasimamia kikamilifu kuhimiza wananchi kutoa michango.
Akizungumza juzi katika kikao cha Baraza la madiwani wa
manispaa ya Shinyanga mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni naibu meya wa
manispaa hiyo David Nkulila alisema kuna baadhi ya madiwani hivi sasa
hawawajibiki wakihofia kunyimwa kura katika chaguzi zijazo.
Nkulila alisema wapo madiwani ambao wanashindwa
kuwahamasisha wananchi kuchangia miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa
maabara katika shule kwa kile kinachodaiwa kuogopa kuwachosha kwa michango
wapiga kura wao.
“Najua wengi wetu tuna hofu kubwa na chaguzi zijazo,naomba
muwe wajasiri kuelimisha wananchi kwa
kusema yaliyo kweli,simamieni miradi ya maendeleo,kama ni kurudi kwenye nafasi
zenu mungu ndiyo anajua,tendeni haki kwa wananchi,uoga haufai”,aliongeza
Nkulila.
Akitangaza maeneo mapya ya uchaguzi wa serikali za
mitaa mwaka huu,mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga Festo Kang'ombe alisema tayari kanuni za
uchaguzi huo zimeshatoka na kilichobaki ni kupokea vifaa kwa ajili ya kupigia
kura tarehe 14,Desemba mwaka huu.
Kang’ombe alisema uchaguzi utafanyika katika kata 17
ikihusishwa mitaa 55 badala ya 25 ya chaguzi zilizopita,vijiji 19 badala ya 17
na vitongoji 85.
“Tayari tumeshatoa tangazo kuhusu maeneo mapya ya uchaguzi wa serikali za
mitaa,matangazo yapo katika ofisi za kata na manispaa ya Shinyanga”,alisema Kang'ombe
Kwa upande wake diwani wa kata ya Ndala kupitia Chama
Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) George Sungura alieleza kusikitishwa na
madiwani katika manispaa hiyo kukosa ushirikiano wa dhati katika shughuli za
maendeleo huku akiwataka kubadilika ili kuwaletea maendeleo wananchi.
Na Kadama Malunde-Shinyanga
Social Plugin