Mtoto mwenye umri wa siku nane, ameibwa baada ya mama yake kunyweshwa juisi inayosadikiwa kuwa na dawa za kulevya.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma, Dk. Nassoro Mzee, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mwanamke huyo, Teddy Bishaliza (19), alilazwa katika Wodi 17 kufuatia afya yake kuathiriwa na dawa hizo, huku mtoto wake wa kike ikidaiwa kuwa aliibwa katika tukio lililotokea juzi mtaa wa Chidachi, Manispaa ya Dodoma.
Akizungumza kwa tabu wodini hapo, Bishaliza alisema alijifungua mtoto huyo Jumatano ya wiki iliyopita hospitalini hapo kwenye Wodi Namba Tatu na kuruhusiwa kurejea nyumbani na mtoto wake siku iliyofuata.
“Nikitoka wodini, nilikutana na dada ambaye sikuwahi kumuona, akanisaidia kubeba mizigo michache niliyokuwa nayo na tulipokaa kwenye benchi akaniambia anikodie bajaj inipeleke nyumbani, tulipofika hakuteremka kwenye bajaj akaahidi kuja tena kututembelea,” alisimulia Bishaliza.
Alisema juzi jioni, dada huyo alifika nyumbani kwao akiwa amevaa dera na kujitanda kikoi kizito chenye rangi ya kijani na chungwa bivu, baadaye mama yake Bishaliza, alimpelekea chakula kisha akamuacha na mdogo wake, Rahel Leganga (12), mtoto na mgeni wao huyo.
Rahel alilieleza kwamba wakati wakila chakula, mgeni ambaye baada ya mama Teddy kuondoka alijifungua ushungi aliokuwa amejifunika sehemu kubwa ya uso wake na kumwagiza ampe vikombe ili awawekee juisi.
“Alitoa juisi ya boksi ile inayouzwa Shilingi 3,000, akanimiminia dada kikombe cha nusu lita na mimi akaniwekea, nilipoonja nikahisi chungu nikaikataa, lakini dada akanywa yote,” alisimulia Rahel na kuendelea:
“Akaniambia ninywe ili niongeze damu mwilini, nikitaka nisisikie uchungu ninywe haraka haraka kama maji, nikamwambia mimi siinywi, tulipomaliza kula tu dada akasema anahisi usingizi, akalala.”
Rahel alisema hata yeye baada ya kula na kurejesha vyombo mahala pake, alilala na alipoamka saa 11:00 alfajiri ya jana, alishangaa kumkuta dada yake amelala fofofo huku mtoto na mgeni wakiwa hawamo chumbani.
Alisema baada ya dada yake kuamka, walijaribu kutoka nje, lakini ilibainika mlango ulifungwa kwa nje, majirani walisaidia kuufungua baada ya wao kupiga kelele wakiomba msaada, yeye (Rahel) alikwenda kumuita baba na mama yao wanaoishi mtaa wa pili.
Baba na Mama Teddy wakiwa nje ya wodi namba 17 alimolazwa mtoto wao huyo, walisema kati yao hakuna anayeweza kumtambua mwizi wa mjukuu wao, isipokuwa Rahel aliyesema akimuona mwanamke huyo atambua.
Baba Teddy aliyejitambulisha kwa jina la Job Leganga, alieleza
kuwa Teddy hana mume bali alipata ujauzito na kutokana na nyumba yao kuwa ndogo, waliamua kumpangishia chumba mtaa wa pili kutoka nyumbani kwao ili waendelee kumhudumia kwa mahitaji yake muhimu.
Teddy alitaja jina la baba wa mtoto wake kuwa ni Christian Francis, ambaye hata hivyo, aliondoka mjini hapa na kurejea kwao mkoani Morogoro.
MAJIRANI WASIMULIA
John Nadoo (50), Mjumbe wa Nyumba Kumi katika eneo analoishi Teddy, alisema juzi jioni alimuona mwanamke akiwa amevaa dera, amejitanda mtandio wake kiasi cha kubakiza sehemu ndogo ya sura yake, lakini hakumsalimia badala yake alionekana akiita watoto.
“Baada ya kuzungumza na watoto, niliona akiongozana na mtoto mmoja, sikuelewa kilichoendelea mpaka asubuhi nilipopata taarifa kutoka kwa majirani kuwa mtoto wa Teddy ameibwa jana (juzi) usiku,” alieleza Nandoo.
Eunice Shaibu (11), alisema: “Aliniita akaniuliza kwa Teddy wapi?” nikamwambia subiri nikuitie mwenzangu akupeleke mimi nimeachwa nilinde nyumba, nikamuita Therezia ndiye aliyempeleka.”
Terezia Michael (11), alisema alipofika nyumbani kwa Teddy, walimkuta akiwa amekaa kwenye kizingiti cha mlango wa kuingia kwenye ua wa nyumba yao akampokea mkoba.
Rosemary Ndahani (21), anayeishi chumba kilichopakana na Teddy, alisema akiwa na mpangaji mwenzao, Happy, waliona Teddy akiingia kwenye ua wa nyumba yao na dada anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 28, mrefu, mweupe mwenye unene wa wastani, alivaa dera ambalo mtandio wake aliutumia kujifunga ushungi.
Alisema hawakufahamu kilichoendelea mpaka asubuhi aliposikia Teddy na mdogo wake wakipiga kelele za kuomba msaada, kufunguliwa mlango wa chumba chao uliokuwa umefungwa kwa nje na kwamba alipotoka chumbani humo alikuwa akiweweseka mithili ya watumiaji wa dawa za kulevya.
“Alichokuwa akitamka ni kudai mtoto wake, akisema ‘wameniibia mtoto wangu, lakini alikuwa hajiwezi, akiweweseka kwa kukosa nguvu kabisa mpaka wazazi wake walipofika na kumpeleka hospitali,” alieleza Ndahani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, alipoulizwa na mwandishi wa habari hizi kuhusiana na tukio hilo, alisema analifanyia kazi na kwamba hawezi kuthibitisha kama mtoto huyo ameibwa ama la.
via>>Nipashe