MFANYAKAZI wa kiwanda cha kutengeneza nguo na vyandarua cha A to Z, kilichopo Kisongo nje kidogo ya Jiji la Arusha amekufa kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kudondokewa na mashine ya kufungia marobota.
Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas amethibitisha kuwapo kwa tukio hilo, ingawa aliahidi kutoa taarifa zaidi leo.
Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya kiwanda hicho zilizothibitishwa na Mkurugenzi wa Uzalishaji wa kiwanda hicho, Binesh Haria, zinasema aliyekufa ametambuliwa kwa jina la Erick Mathayo (25).
Inaelezwa alidondokewa chuma hicho kizito juzi saa 1:00 asubuhi alipokuwa akijaribu kuhakiki moja ya mizigo iliyokwishafungwa.
Mathayo alipasuka kichwa na ubongo kuwa wazi hali iliyoulazimu uongozi wa kiwanda kumkimbiza hospitali ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru kwa matibabu.
Taarifa kutoka Hospitali ya Mount Meru zilizothibitishwa na mhudumu wa Kitengo cha Wagonjwa walio katika Uangalizi Maalumu (ICU) ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kuwa siyo msemaji wa hospitali, zinadai kwamba Mathayo alikufa wakati akiendelea kupatiwa matibabu.
Akithibitisha kutokea kwa kifo hicho, Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Afya za Wafanyakazi na Usalama Mahali pa Kazi (OSHA), Ramadhani Msimbira alikiri kuwepo kwa mazingira anayodai ni mabovu ya utendaji wa kazi ndani ya kiwanda hicho.
Majira ya saa moja usiku juzi, mwandishi wa habari hizi alipigiwa simu na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, John Mongela akimtaka afike ofisini kwake ambapo alitii amri hiyo akiwa ameongozana na waandishi wengine wawili (majina tunayo).
Mongela aliwajulisha kuwa amepigiwa simu na Haria akimwomba awasihi waandishi wa habari kuacha kuandika habari hiyo kwani itawachafulia kwa jamii.
Hata hivyo, baada ya kupewa taarifa kamili na picha ya tukio hilo Mkuu wa Wilaya aliwaruhusu waandishi kuendelea na kazi zao kwa kusisitiza kuwa ''hakuna jinsi ni lazima habari hiyo iandikwe.''
Mwili wa Mathayo umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru na mipango ya mazishi inafanyika nyumbani kwa marehemu Sombetini jijini Arusha.
Social Plugin