Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MKALAMA KUKABIDHI VYUMBA 57 VYA MAABARA OKTOBA 15


DSC00871
Mkuu wa wilaya ya Mkalama mkoani Singida, Edward Ole Lenga.(Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu, Mkalama
WILAYA mpya ya Mkalama mkoa wa Singida, Oktoba 15 mwaka hu ,inatarajia kumkabidhi mkuu wa mkoa wa Singida, Dk.Parseko Kone, vyumba 57 vya maabara katika shule 19 za sekondari za kata ya wilayani humo zikiwa zimekamilika ujenzi wake kwa asilimia mia moja.
Akizungumza na Mwakilishi wa MOblog, mkuu wa wilaya hiyo, Edwerd Ole Lenga alisema hadi sasa ujenzi wa  vyumba 53 vya maabara katika shule hizo,umekamilika na ni sawa na aslimia 92.9 ya ujenzi huo.
Alisema ujenzi unaendelea wa vyumba vitatu vya maabara vilivyosalia upo kwenye hatua nzuri ambazo ni kuweka milango, madirisha na rangi tu.
Lenga alisema ujenzi mwigine ni wa chumba vya maabara ya shule ya sekondari ya kata ya Tumuli ambao umechelewa kuanza kutoka na shule hiyo kuhamishwa kupisha uwekaji wa umeme,upo kwenye hatua ya kupaua.
“Kwa ujumla sisi tuna uhakika wa kukamilisha ujenzi wa maabara zote mwezi huu wa Septemba mwishoni (30/9/2014). Lakini kutokana na agizo la mkuu wa mkoa, kuwa wilaya zote tano zikabidhi maabara zikiwa zimekamilika kwa aslimia mia oktoba 15 mwaka huu, basi tutafanya hivyo siku ikifika”, alifafanua mkuu huyo wa wilaya.
Lenga alisema mafanikio hayo ya kujivunia, kwa kifupi yamechangiwa na mbinu shirikishi ambapo wananchi walishirikishwa kuanzia hatua ya kwanza ya kupanga ujenzi huo.Vile vile usimamizi ulikuwa madhubuti na mkali.
Kwa upande wa vifaa vya maabara,Lenga alisema wanatarajia kunza na vifaa vya maabara ya somo la kemia kwa kila shule.
“Naomba nitumie nafasi hii, kuiomba Wizara ya elimu na mafunzo, ituunge mkono kwa kutusaidia vifaa vya maabara. Milango ipo wazi pia kwa wadau wa maendeleo ya elimu kutuunga mkono kwa kutusaidia vifaa vya maabara ili wanafunzi waweze kusoma sayansi kwa vitendo pia”,alisema Lenga.
Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa wilaya ametumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi, madiwani na watendaji kwa ushirikiano wao uliofanikisha ujenzi huo.
Akifafanua zaidi,alisema “Mafanikio hayo ya ujenzi wa maabara,yamepelekea wilaya kuongoza katika kufanya vizuri kwenye ujenzi wa maabara kati ya wilaya tano za mkoa wa Singida”

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com