Mwanamme aitwaye Mageni Buhimili(54) mkazi wa kijiji na kata ya Mwakitolyo
wilaya ya Shinyanga ameuawa kwa kukatwa panga kichwani,mikononi na tumboni
wakati akila chakula cha usiku nyumbani kwake.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga SACP Justus Kamugisha amesema tukio hilo
limetokea Oktoba 26 mwaka huu saa moja na nusu usiku.
Kamanda Kamugisha alisema mwanamme huyo mkazi wa kitongoji cha Mahiga kata ya
Mwakitolyo akiwa anakula chakula cha usiku ghafla alivamiwa na watu
wasiojulikana kisha kumuua kwa kumkata panga kichwani,mikononi na tumboni.
Alisema juhudi za kuwabaini na kuwakamata wahusika wa tukio hilo zinaendelea.
Wakati huo huo jeshi la polisi linawashikilia watu watatu wakazi wa kata ya
Idahina wilayani Kahama kwa kosa la kukutwa wakimiliki silaha aina ya bastola
na gobole kinyume cha sheria.
Kamanda Kamugisha alisema watu hao walikamatwa Oktoba 27 mwaka huu.
Aliwataja watu hao kuwa ni Magashi Magunga(21) mkazi wa Chato mkoa wa Geita na
Masumbuko Juma(27) mkazi Ushirombo ambao walikamatwa kwa kupatikana na silaha
aina ya bastola.
Alisema silaha hiyo imetengenezwa kienyeji isiyokuwa na namba za usajili
wakimiliki kinyume cha sheria na kwamba wanahojiwa ili kubaini matukio ya
kihalifu waliyokuwa wakiyafanya.
Alimtaja mtuhumiwa wa tatu kuwa ni mwanamke aitwaye Kashindye Mgaiwa(38)
aliyekamatwa kwa kosa la kupatikana na silaha aina ya gobole lililotengenezwa
kienyeji na halina namba.
Kamanda huyo aliongeza kuwa mtuhumiwa alikuwa akilimiliki bila kibali na
inasadikiwa alikuwa akilitumia kutenda uhalifu.
Na Kadama Malunde-Shinyanga