Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga SACP Justus Kamugisha |
Mwanamke mmoja aitwaye Frola Kakiziba(47) aliyekuwa
katibu muhtasi wa ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa ya Shinyanga
mkazi wa Majengo Mapya mjini Shinyanga amefariki dunia baada ya pikipiki
aliyokuwa anasafiria kugongana na pikipiki nyingine katika barabara kuu ya
Shinyanga-Mwanza.
Tukio hilo limetokea jana saa moja asubuhi katika eneo
la Ushirika,kata ya Ngokolo barabara ya Shinyanga Mwanza ambapo pikipiki yenye
namba za usajili T.317 BWW aina ya SUNLG iligonga ubavuni pikipiki nyingine
ikiendeshwa na dereva asiyefahamika iliyokuwa imembeba abiria aitwaye Frola
Kakiziba.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha
alisema pikipiki yenye namba za usajili usajili T.317 BWW ikiendeshwa na Khamis
Nkelege(52) ambaye ni afisa ardhi Shinyanga mkazi wa Mwasele iliigonga pikipiki
aliyokuwa amepanda Frola Kakiziba ambaye alianguka chini na kupata majeraha
kichwani na kupelekwa katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga na kufariki dunia
muda mfupi wakati akipatiwa matibabu.
Amesema dereva wa pikipiki iliyokuwa imembeba marehemu
alikimbia baada ya ajali.
Hata hivyo amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa
madereva wa pikipiki zote mbili.
Kamanda Kamugisha amewataka watumiaji wa
magari,pikipiki na watumiaji wengine wa barabara kufuata sheria za usalama
barabarani ili kuepuka ajali zisizo za lazima.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog
Social Plugin