Uchaguzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA,wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga umeingia dosari,baada ya mmoja wa madiwani wa chama hicho kuhusishwa na rushwa na vitendo vya usaliti ndani ya chama kutoka CCM.
Pia katika uchaguzi huo baadhi ya wagombea wamechapana makonde baada ya kuenguliwa kwa baadhi ya majina ya wagombea katika uchaguzi wa Baraza la Vijana wa chama hicho (BAVICHA),huku Red Brigade wakihusika katika vurugu hizo.
Hali hiyo ilitokea juzi mjini Kahama katika ukumbi wa Mamba Hall, baada mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa Chama hicho wilayani Kahama Leonard Mayala ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nyasubi, alienguliwa kuwania nafasi hiyo baada ya kubainika kutumia rushwa kuomba achaguliwe katika nafasi hiyo.
Mgombea huyo alituhumiwa kutumia shilingi milioni mbili kuwahonga baadhi ya wanachama,fedha ambazo zinadaiwa zilitolewa na baadhi ya makada wa Chama cha Mapinduzi kwa njia ya mtandao wa (Mpesa)ili kuhakisha ananyakuwa nafasi hiyo.
Tuhuma hizo zimekuja baada ya wanachama kutokuwa na imani naye kutokana na mwenendo wa diwani huyo wa kuwa karibu na makada wa CCM wilayani hapa na hivyo kusababisha viongozi na wasimamizi wa uchaguzi huo kuengua jina lake baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na kuwekewa pingamizi.
Aidha katika uchaguzi huo baadhi ya wagombea na wanachama walichapana makonde wakipinga kuenguliwa majina ya baadhi majina ya wagombea katika uchaguzi wa Baraza la Vijana wa Chadema (BAVICHA).
Ugomvi huo ulitokea baada ya wagombea waliopitishwa katika nafasi ya Uenyekiti wa Bavicha kuanza kujinadi kwa wananchama ndipo mgombea Thomas Masanja aliyeenguliwa katika kinyang’anyiro hicho kutokana na kukosa sifa ikiwemo kadi yake ya uanachana kutotambulika alijitokeza na kuzuia uchaguzi.
Kufuatia kuenguliwa kwa mgombea huyo ndipo badhi ya wafuasi wake wakiwemo Red Brigade walipojitokeza na kuanza kufanya fujo kwa lengo la kuzuia uchaguzi huo kuendelea wakidai kwamba mgombea wao kutotendewa haki kwa kuenguliwa kinyemela kugombea nafasi hiyo.
Hali hiyo ilikwenda mbali zaidi kwani wafuasi hao walianza kuwashambulia baadhi ya viongozi na wasimamizi ambapo Mwenyekiti wa Chadema wa Halmashauri ya Msalala Emmanuel Bombeda alipigwa ngumi na Red brigade waliokuwa wakimuunga mkono mgombea aliyeenguliwa.
Utulivu na amani urejea ukumbini humo baada ya msimamizi wa uchaguzi wa Chama hicho kanda ya Ziwa Mashairiki,Madata Sande kuingilia kati na kuwataka wanachama kuwa wavumilivu ili kufanikisha uchaguzi huo kwani wagombea walioenguliewa katika kinyang’anyiro hicho walienguliwa kihalali bila upendeleo wowote kwa kuzingatia katiba ya chama hicho.
Katika uchaguzi huo wajumbe walimchagua Juma Protas,kuwa Mwenyekiti wa Chadema wa wilaya hiyo,naye Mshibu Peter akiteuliwa kushika nafasi ya Ukatibu wa chama hicho,nafasi ya Ukatibu Uenezi ikimwangukia Anord Peter na Mweka Hazina alichaguliwa,Elias Mayunga.
Nalo Baraza la Vijana BAVICHA lilimchagua Samwel Peter kuwa Mwenyekiti wake na ndani ya uchaguzi huo wajumbe walichagua viongozi mbali mbali wa yakiwemo mabaraza ya Wazee,Wanawanake na wajumbe wa mkutano mkuu taifa wa chama hicho.
via>>mohabmatukio blog