Baadhi ya wagonjwa waliofika kupata huduma katika Hospitali ya Wilaya ya Geita wameutaka uongozi kumtimua daktari mmoja (jina tunalihifadhi), kwa madai ya kufanya kazi za kitabibu akiwa amelewa.
Mbali na madai hayo, pia wagonjwa hao wamelalamika kutolewa lugha chafu na daktari huyo.
Tukio hilo linadaiwa kutokea juzi baada ya daktari huyo kufika hospitalini hapo na kukuta wagonjwa wakiwa kwenye foleni na baadaye kuwaporomoshea matusi.
Hata hivyo, madai hayo yalipingwa na daktari huyo aliyekuwa mkali wakati alipoombwa kuzungumzia madai dhidi yake.
Alisema: “Sasa unataka niseme nini hapo. Mimi siyo msemaji, kamuulize bosi wangu.”
Mmoja wa wagonjwa anayedai kukutana na kadhia hiyo, Joyce Makoye, mkazi wa Nzera, alisema mara nyingi anapokwenda hospitalini hapo ni kawaida kumkuta daktari huyo akiwa amelewa.
“Alikuja hapa akiwa na dalili zote za kulewa; hakuwa kwenye hali ya kawaida. Alitoa lugha chafu kwa wagonjwa kiasi cha kuwafanya wengine kuondoka bila kutibiwa,” alisema Makoye.
Alisema kitendo cha daktari huyo kuja kazini akiwa amelewa, kimeidhalilisha taaluma ya udaktari na yeye mwenyewe.
Mkazi mwingine, Martine John alisema mbali na tuhuma hizo, pia daktari huyo ana tabia ya kutumia muda mwingi kufanya mambo binafsi na siyo kuhudumia wagonjwa.
Alisema wanapinga daktari huyo kuendelea kufanya kazi kwenye hospitali hiyo kwa vile tayari wananchi wameshapoteza imani naye.
“Tungependa mganga mkuu wa hospitali afanye utaratibu wa kumtoa kwenye kituo hiki. Hatumhitaji kwa sababu hana upendo kwa wagonjwa,” alisema John.
“Analipwa mshahara wa bure ndiyo maana muda mwingi anautumia kwenye pombe na mambo yake binafsi.”
Mganga mkuu, Dk Adam Sijaona alisema hana taarifa na tukio hilo, wala hajapata malalamiko kuhusu tabia ya ulevi inayolalamikiwa na wagonjwa.
“Sina taarifa ya tukio wala kupokea malalamiko. Ninachofahamu, mtumishi wa afya hatakiwi hata kuonja pombe anapokuwa kazini,” alisema Dk Sijaona.
Na Jackline Masinde, Mwananchi
Social Plugin