Kwako, Hashim Lundenga.
Ni
matumaini yangu kwamba hunifahamu licha ya kwamba majina yetu
yanashabihiana. Najua jinsi jasho linavyoendelea kukutoka kutokana na
changamoto kubwa unazokutana nazo, tangu ulipomtangaza Sitti Mtemvu kuwa
Miss wa Tanzania 2014.
Mimi
si Mkurugenzi wa Lino International Agency, kampuni inayoendesha
mashindano ya Miss Tanzania kwa mwaka wa 18 sasa mfululizo. Mimi
sijawahi kwenda Wizara ya Elimu na Utamaduni (kipindi hicho) kuomba
kibali cha kuyaanzisha tena mashindano ya Miss Tanzania baada ya kuwa
yamepigwa marufuku kwa zaidi ya miaka 24 (yalipigwa marufuku mwaka 1968
kutokana na sababu za kimaadili).
Sikushirikiana
na Prashant Patel kumtafuta mkurugenzi wa utamaduni kipindi hicho, Baya
Senkemwa na kumuomba ‘chondechonde’, aangalie kama kuna namna
tunayoweza kuruhusiwa kuirudisha Miss Tanzania.
Mimi
ni mlalahoi tu ambaye sina ubavu wa kufanya kama wewe uliyoyafanya.
Nakuhakikishia, tangu kipindi hicho, mimi nisingekuwa na ubavu wa
kuendelea kusimamia mashindano hayo na kutoa warembo kedekede kwa zaidi
ya miaka 18 kama wewe, ningeanzia wapi?
Hata
hivyo, hayo yote hayanizuii kukufikishia ujumbe wangu kwako, anko
wahenga wanasema, nguo ikimvuka muungwana huchutama.
Jahazi la Miss
Tanzania linazama anko, ng’atuka ili uendelee kutunza heshima yako.
Kwa uzoefu na uelewa
wako, najua unajua fika kwamba mwaka huu ‘umebugi’ kumtangaza Sitti
Mtemvu kuwa Miss Tanzania. Sijui kama ni urafiki wa kawaida kati yako na
baba yake, mheshimiwa Abbas Mtemvu uliokusukuma kumpa ushindi au ni
vigezo alivyokuwa navyo msichana huyo, sitaki kuzungumzia huko, ishu
kubwa hapa ni suala la umri.
Yawezekana
awali hukujua kama umeingizwa chaka na Sitti kwa kukuletea cheti chenye
utata kuhusu umri wake halisi. Huenda wewe na kamati yako mlijiridhisha
kwamba kweli Sitti alizaliwa mwaka 1991. Katika hili mnaweza kusamehewa
kwamba ‘huenda’ hamkuujua ukweli mapema.
Hata
hivyo, kama kweli mliingizwa chaka, iweje hata uthibitisho mwingine
ulipopatikana wa hati ya kusafiria ya Sitti yenye namba AB201696
kuonesha kwamba mrembo huyo alizaliwa Mei 31, 1989 na siyo 1991 kama
alivyowaaminisha, kwa nini mnaendelea kuwa wagumu na kushikilia msimamo
wa awali?
Hapa
naanza kupata shaka Lundenga, nilitegemea kwamba kwa sababu umepata
uzoefu wa kutosha wa kuongoza Miss Tanzania kwa miaka 18, ungeweza
kung’amua haraka kwamba kelele anazopigiwa Sitti kuhusu kudanganya umri
zina hoja ndani yake.
Badala
ya kuendelea kutetea ubatili wa Sitti, ungesimamia kwenye ukweli na
kuwaeleza Watanzania kwamba mlighafirika na kumpa ushindi mtu asiyefaa
kwa sababu aliwadanganya.
Badala
yake, umeendelea kumtetea huku ukishindwa hata kugundua kwamba
kujikanyaga kwa mrembo huyo wakati akihojiwa na waandishi wa habari,
ilikuwa ni kwa sababu kuna jambo analificha.
Hapana
Lundenga, hapa umechemka na kwa kuwa unaendelea kutetea uovu, unazidi
kutupa shaka zaidi. Nikwambie tu, inaonekana unafahamu kila kitu kuhusu
mchezo unaoendelea na hiyo pekee inatosha kukuondolea sifa za kuwa hapo
ulipo.
Kwa
bahati mbaya mimi nitabaki kuwa mimi na sitaweza kuwa wewe lakini kama
ningekuwa mimi kwenye nafasi yako, kwa hili la Miss Tanzania 2014,
narudia tena kusema bila kumung’unya maneno kwamba ningeng’atuka na
kuwaachia wengine wenye uwezo zaidi yangu waongoze Miss Tanzania.
Social Plugin