Shirika la Ujasusi la Israel Mossad limetoa tangazo fulani la kazi kwa njia ya video. Kwenye video hiyo wanaonyesha ndege isiyo na rubani (drone) inavyomfuatilia mtu na kumpiga picha kwa matumizi yake.
Kwa Marekani siyo mara moja wala mara mbili, dunia imeshuhudia ndege hizo zikitumika kuwashambulia wale ambao nchi hiyo inawaita magaidi. Yanatokea haya Pakistan, Afghanistan, Somalia na maeneo mengine duniani.
Pia ni kawaida kusikia drone ya Israel imetunguliwa nchini Iran ilipokuwa katika shughuli za ujasusi. Kimsingi matumizi ya ndege hizo yamekuwa makubwa siku za karibuni.
Drone maarufu kwa kifupi cha ARV ni ndege zinazoendeshwa au kuelekezwa na watu waliopo ardhini katika vituo maalumu.
Drone inaweza kuwa India lakini rubani akawa Dodoma nchini Tanzania, au drone inaweza kuagizwa kufanya shuguli fulani sehemu yoyote duniani kwa kupewa miongozo kutokana na programu inayotumia.
Wanazielekeza ndege hizo kufanya shughuli mbalimbali hasa za kiulinzi na kiusalama. Wakati mwingine ndege hizo hazihitaji mtu wa kuziongoza moja kwa moja, inaweza kutengenezewa programu maalumu na kujiendesha yenyewe.
Awali, ndege hizi hazikujulikana hadi mwaka 2007 baada ya jeshi la Marekani kutuhumiwa kuuwa watoto kwenye harusi moja katika mpaka wa Pakistan na Afghanistan. Kuanzia hapo dunia ikatambua kuwa ndege hizo ni silaha tena za maangamizi.
Kuna aina mbalimbali za drones lakini zote zinaweza kugawanywa katika makundi mawili. Mosi, zile zinazotumika kwenye shughuli za upelelezi na pili, zinazotumika katika shughuli za kivita.
Katika siku za karibuni, ndege hizo zimekuwa zikitumika kama vyombo vya kusafirishia bidhaa ndogondogo, hasa zinazonunuliwa kwa mtandao. Tayari kampuni za Google na Amazon zimeshaanza majaribio ya ndege hizo.
Barani Afrika hatuko nyuma katika biashara ya drones au vyombo vinavyofanana na ndege hiyo. Afrika Kusini kuna kampuni imeanza kutengeneza drones na inapanga kuanza kukodisha kwa mataifa mengine kwa ajili ya shughuli mbalimbali.
Hapa Tanzania hasa kwenye hifadhi za wanyama, Serikali imeamua kutumia drone kwa ajili ya kupeleleza na kuchukua picha za maeneo mbalimbali ya hifadhi, pamoja na kulinda wanyama dhidi ya majangili na majanga mengine yanayoweza kutokea maeneo hayo.
Hivi sasa kuna mijadala inaendelea kuhusu matumizi ya drones sehemu mbalimbali duniani hasa kwenye shughuli za kijeshi na nyingine ambazo siyo za kibiashara.
Wanauliza kuhusu sheria na mikataba mingine ya kimataifa kuhusu anga na ukuaji wa kasi wa drones hasa pale zinapotumika kushambulia maadui na kufanya uharibifu mkubwa wa mali na watu.
Pamoja na changamoto hizo hapo juu, kuna faida nyingi za kutumia drone kwenye suala zima la usafirishaji, ikiwa kutakuwapo na sheria nzuri na usimamizi mzuri wa sheria husika.
Katika nchi maskini, drones zinaweza kurahisisha usafiri kwa kiasi kikubwa.
Hivi sasa duniani kuna aina nyingi za drone zinazoweza kufanya shughuli mbalimbali kutegemea na mazingira na mahitaji ya jamii husika na hata nyingine zinaendelea kutengenezwa na kuboreshwa zaidi .
via>>Mwananchi
Social Plugin