Sisi Mashirika
yapatayo 50 yanayotetea Usawa wa Kijinsia, Haki za Binadamu, Demokrasia,
Utawala bora, Maendeleo na Ukombozi wa Mwanamke Kimapinduzi (FEMACT) tumekuwa
tukifuatilia kwa karibu mchakato wa katiba unavyokwenda tangu ulipoanza pamoja
na changamoto zinazojitokeza bado kuna fursa ambazo wananchi wameweza
kushirikishwa na kutia matumaini ya kupata katiba mpya.
Jambo
la kusikitisha ni kwamba wakati mchakato ukikaribia mwisho kumeanza kujitokeza matukio ya aibu naya kusikitisha ambayo yanaweza kuuchafua kabisa au kuharibu
kazi nzuri ambayo ilikuwa imeanza kufanyika.
Mdahalo huo
uliokuwa ukirushwa moja kwamoja na redio na televisheni ulivurugika kutokana na
kundi la vijana kuanza kumzomea aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Jaji Joseph Warioba, alipokuwa akiwasilisha hoja zake.
Zomeazomea hiyo
ilifuatiwa na vurugu ambazo zilisababisha mtafaruku na bugdha kubwa kwa
washiriki wa mjadala huo.
Hali hii ni tishio
kwa uhuru na haki kwa wananchi kujieleza, kutoa maoni na kujumuika katika
kujadili masuala muhimu yanayohusu mustakabali wa nchi yao. FEMACT kama
muungano wa mashirika na asasi mbalimbali za kiraiya, inalaani vikali vurugu
hizo kwani zinaweza kusababisha machafuko nchini hasa katika kipindi hiki cha
kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na mchakato wa kura ya maoni ya katiba
pendekezwa.
Vurugu kama hizo zinaweza kuwa tishio kwa wananchi
hasa makundi yaliyoko pemebezoni, wakiwemo wanawake, wazee, walemavu na makundi
mengineyo.
Ni dhahiri kuwa, makundi hayo na watanzania kwa ujumla watakuwa na
hofu ya kushiriki katika kujadili katiba pendekezwa ambayo ni mustakabali wa
nchi yao.
Hii inaweza kusababisha watu au makundi yanayopenda kushiriki katika
kujadili katiba pendekezwa kutojitokeza tena kwa hofu ya kufanyiwa fujo.
Aidha, kuhusu kufanyiwa fujo kwa aliyekuwa
Mwenyekiti wa Tume ya Katiba Jani mstaafu Joseph Warioba, na watu wengine
akiwemo mwanamke na mlemavu wa macho waliokuwa wanashiriki katika mjadala huo,
kitendo hicho ni cha kidhalilishaji kinacholenga kufifisha maoni ya wananchi.
FEMACT kama watetezi wa haki za kijamii inaamini kuwa mtu yeyoye ana uhuru wa
kutoa maoni yake na kusikilizwa na watu wengine bila kufanyiwa vurugu,
kudhalilishwa au kudhuriwa kwa namna yoyote.
Hofu yetu ni kwamba matukio kama haya yanawatisha
wanawake na walemavu kushiriki hatua
zinazofuata kama uchaguzi wa serikali za mitaa, kura za maoni na uchaguzi mkuu
2015 kikamilifu kwasababu watahofia kufanyiwa vurugu.
Kwa takribani miaka 10 iliyopita tumeshuhudia
idadi ya wapiga kura nchini ikizidi kushuka badala ya kuongezeka licha ya kuwa
idadi ya watu nchini kuongezeka, sababu
kama hizi za kuvuruga mikusanyiko ya wananchi, mikutano ambayo wananchi
wanapashana taarifa inafifisha ari ya wananchi kujitokeza.
Ili kuhakikisha mchakato huu unafanyika katika
hali stahiki, na wananchi kushiriki kikamilifu chaguzi zinazokuja FEMACT
inapendekeza yafuatayo;
1.
Uhuru
wa kujieleza na kutoa maoni uheshimiwe katika kujadili mambo yanayohusu
mustakabali wan chi yao ikiwemo katiba pendekezwa na makundi yote yakiwemo
yaliyoko pembezoni yapewe nafasi na kuhakikishiwa usalama.
2.
Vyombo
vya usalama kuhakikisha kuwa, usalama unakuwepo kwa wananchi wakati
wanaposhiriki katika mchakato wa kujadili na kupiga kura ya maoni ya katiba
pendekezwa pamoja na chaguzi zijazo.
3.
Vijana
ambao ni zaidi ya asilimia 65% ya idadi ya watu nchini, waepuke kutumiwa na
watu binafsi, vyama vya siasa au makundi fulani katika jamii ili kuepukana na
kuharibika kwa hali ya usalama katika nchi yetu.
4.
Vyama
vya siasa au makundi yoyote kuacha mara moja kushiriki katika vitendo vya
kiuchochezi au vinavyoweza kusababisha vurugu katika nchi yetu.
5.
Wananchi
waachwe wajadili kwa mapana maudhui ya Katiba
Pendekezi bila kuwekewa mipaka au ukomo ili waielewe kabla ya kushiriki upigaji
kura kama ilivyopendekezwa.
Imetolewa na
Lilian Liundi
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji -TGNP Mtandao
Kny Sekretarieti ya
FemAct
Social Plugin