Wakati Watanzania wakizidi kupoteza maisha yao kutokana na ajali za mara kwa mara abiria waliokuwa wanasafiri na gari ya kampuni ya AFRICA ONE kutoka mkoani Mwanza na kuelekea Kagera wameiomba Mamlaka ya usafirishaji wa maji na nchi kavu (SUMATRA) kuifungia mara moja kampuni hiyo kutokana na dereva anayendesha gari lenye namba T. 444 B CW kulewa kupindukia wakati akiendesha.
Wakizungumza na waandishi wa habari abiria hao waliokwama zaidi ya saa tano katika mtaa wa Mbugani wilayani Geita Mkoani Geita baada ya gari kuharibika kisha dereva na konda kutoweka na kwenda baa ya jirani na kuanza kunywa pombe na huku wakijua kuwa wanabeba roho za watanzania.
Mmoja wa abiria aliyejitambulisha kwa jina la Makoye Lugata alisema tangu walipoanza safari hiyo pamoja na abiria hao kulalamikia mwendo kasi wake lakini hawakuweza kusikilizwa kutokana na dereva huyo kuendesha huku anakunywa viroba aina ya konyagi anavyotembea navyo mfukoni mwake.
"Jamani tangu tunatoka Mwanza ni matatizo makubwa sana, na tumelipa nauli zetu dereva na kondakta wake wanatembea wakinywa viroba, mimi naomba mamlaka husika iifungie kampuni hii kwani tunaweza kupoteza watanzania wengi kama utaratibu ni huu",alisema Makoye.
"Sijui kama tutafika tunakokwenda, gari ni bovu, inaharibika kila wakati dereva na konda wake wanakunywa viroba tu, tukisema tunaambiwa "kama hutaki kuendelea na safari tushuke" mimi nina watoto tunakwenda msibani Bukoba na sasa hivi hawaonekani wametoweka hatujui hatima yetu" alisema abiria mwingine aitwaye Koleta.
Dereva wa gari hilo ambaye hakutambulika jina lake mara moja alipohojiwa na waandishi wa habari kuhusu malalamiko hayo kwa abiria wake na kuendesha huku akinywa viroba barabarani alikataa kuzungumza na kuamua kukaa kimya.
Akiongea na waandishi wa habari kwa njia ya simu mkurugenzi wa kampuni hiyo Zamiru Idd a alisema kuwa yeye yuko Dar-es-salaam na hajui kama kuna mambo kama hayo.
"Katika barabara hiyo kuna maaskari wengi, hiyo gari ilipitaje ikiwa na mwendo kasi?",alihoji
Kuhusu kulewa kwa dereva wake, alisema hata huyo dereva hamjui na hajawahi kumuona wakuulizwa ni meneja wake.
Meneja wa kampuni hiyo anayeishi Mkoani Mwanza alipopigiwa simu,simu yake iliita bila kupokelewa na alipotumiwa ujumbe wa maandishi akujibu.
Naye Kamanda wa usalama barabarani Mkoa wa GeitaaJohn Mfinanga alipoulizwa juu ya hilo aliseama hana taarifa ya gari hilo na kuahidi kufuatilia kwa karibu suala hilo.
Na Valence Robert-Malunde1 blog Geita