Licha ya kutoa ajira kwa maelfu ya vijana wa Kitanzania na pia kupunguza tatizo la usafiri mijini litokanalo na foleni, usafiri wa pikipiki maarufu kama 'bodaboda' umeendelea kuua watu kimyakimya na kuwasababishia ulemavu wa kudumu maelfu ya manusura wa ajali za vyombo hivyo kila uchao.
Uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa mbali na vifo na ulemavu, bodaboda zimeathiri pia utoaji wa huduma katika hospitali zinazopokea majeruhi wa vyombo hivyo, kwani wodi zimefurika kupita kiasi na kusababisha wagonjwa wengi kulala chini.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohamed Mpinga, amesema katika kipindi cha mwaka 2013 peke yake, pikipiki 8,241 zilihusika katika ajali 6,831 na kusababisha vifo vya watu 1,098 na kuwajeruhi wengine 6,578; huku baadhi yao wakiishia kupata ulemavu wa kudumu. Idadi hiyo ni sawa na wastani wa vifo vya watu watatu kila uchao na majeruhi 18.
DAR, MORO, PWANI VINARA
Akieleza zaidi, Kamanda Mpinga anasema kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Agosti mwaka huu, pikipiki 3,998 zilihusika kwenye ajali 3,777 na kusababisha vifo vya watu 608 na majeruhi 2,883.
Aidha, takwimu za mikoa zinaonyesha kuwa jiji la Dar es Salaam ndilo linaloongoza kwa kuwa na matukio ya ajali za bodaboda. Mwaka jana, bodaboda 3,970 zilihusika katika ajali 3,405 jijini Dar es Salaam na kusababisha vifo vya watu 172 na majeruhi 3,541.
Kadhalika, katika kipindi cha Januari hadi Agosti mwaka huu, jiji la Dar es Salaam lilikuwa na ajali 1,687 zilizohusisha pikipiki 2,280 na kusababisha vifo vya watu 113 na majeruhi 1,539.
Kamanda Mpinga anasema mkoa unaoshika nafasi ya pili kwa ajali za bodaboda ni Morogoro; uliokuwa na ajali 657 na kuhusisha pikipiki 866 zilizosababisha vifo 73 na majeruhi 557 kwa mwaka 2013
Mwaka huu, kwa kipindi cha Januari hadi Agosti, Morogoro kulikuwa na ajali 191 zilizohusisha pikipiki 264 na kusababisha vifo vya watu 41 na majeruhi 202.
Mpinga anautaja mkoa unaoshika nafasi ya tatu kuwa ni Pwani, wenye matukio 428 ya ajali zilizohusisha pikipiki 589, vifo vya watu 84 na majeruhi 466 kwa mwaka 2013, huku kwa kipindi cha Januari hadi Agosti mwaka huu mkoa huo ukiwa na matukio 121 yaliyohusisha pikipiki 164 na kusababisha vifo vya watu 40 na majeruhi 172.
Kilimanjaro unashikilia nafasi ya nne katika janga hilo. Ulikuwa na ajali 372 zilizohusisha pikipiki 409 na kusababisha vifo vya watu 74 na majeruhi 343 kwa mwaka 2013. Kuanzia Januari hadi Agosti mwaka huu, mkoa huo ulikuwa na ajali 104 zilizohusisha pikipiki 121 na kusababisha vifo vya watu 22 na majeruhi 88.
Mikoa mingine na idadi ya ajali za bodaboda katika kipindi cha mwaka 2013 kwenye mabano ni Ruvuma (213), Katavi (190), Arusha (180), Manyara (154), Tabora (128), Dodoma (123), Rukwa (110), Mwanza (96), Mbeya (90), Kigoma ( 82), Shinyanga (81) na Kanda Maalum ya Tarime/Rorya ajali 80.
Mingine ni Mtwara (77), Lindi (59), Singida (54), Geita (50), Kagera (43), Mara (42), Tanga (35), Njombe (27) na Simiyu ikiwa na matukio machache zaidi ya ajali za bodaboda yaliyoripotiwa Polisi baada ya kukumbwa na ajali 18 katika kipindi chote cha mwaka 2013.
Akielezea kuhusu hatua zitakazosaidia kupunguza zaidi ajali za bodaboda nchini, Mpinga anasema elimu ndiyo nguzo ya kumaliza ajali za bodaboda na kwamba tangu mwaka 2010, wamekuwa wakitoa elimu na wanaamini kuwa walau kiwango cha ajali za bodaboda kimekuwa kikipungua.
Kamanda Mpinga anasema katika utafiti wao, wamebaini vyanzo vya ajali nyingi ni makosa ya kibinadamu ambayo ni pamoja na kutoheshimu sheria, mwendo wa kasi, ulevi wa madereva (ukiwamo wa unywaji wa viroba kabla ya kuendesha), pikipiki kupakiza abiria wengi zaidi ya uwezo wake maarufu kama mishkaki na madereva kutokuwa na leseni zinazothibitisha kuwa na uwezo wa kutumia vyombo hivyo vya moto.
Anataja vyanzo vingine kuwa ni ubovu wa miundombinu kama mashimo, utelezi na kona kali barabarani na watumiaji kutovaa kofia ngumu (helmet) huchangia kuongeza idadi ya vifo vitokanavyo na ajali za pikipiki.
REKODI YAWEKWA MOI
Uchunguzi umebaini kuwa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi) peke yake hupokea wastani wa majeruhi 77 kwa wiki wanaotokana na ajali za bodaboda, hiyo ikiwa ni sawa na wastani wa majeruhi 11 kwa siku.
Dk. Mwanga Joseph wa Moi anasema asilimia 55 ya majeruhi wote wanaofikishwa kwao kutokana na matukio ya ajali jijini Dar es Salaam huwa ni kutokana na bodaboda.
Anasema wingi huo wa majeruhi wa bodaboda husababisha mrundikano wa wagonjwa wodini kiasi cha kuzidi idadi ya vitanda na hivyo wengi hulazimika kulala chini.Anasema licha ya changamoto zilizopo sasa, wao wanaendelea kutekeleza wajibu wao wa kutoa huduma na wanaamini kuwa ufumbuzi wa tatizo la mrundikano uliopo sasa Muhimbili ni kuwa na matawi zaidi ya Moi kuanzia ngazi ya mkoa na wilaya ili kupunguza idadi ya wagonjwa wanaofikishwa hapo kila uchao.
Msemaji wa Moi, Patrick Mvungi, anasema kwa mwezi mmoja, wagonjwa wa ajali ni 600 na kati yao, 330 sawa na asilimia 55, ni wa ajali za bodaboda.
Mvungi anasema kuwa licha ya majeruhi wa pikipiki kuwa wengi kiasi cha kuzidi uwezo wa wodi zao, bado wanapowapokea huwachukulia kuwa ni sawa na majeruhi wengine na wala hawawatengi kwenye wodi maalum kama ambavyo imekuwa ikivumishwa na baadhi ya watu.
" Kuna uvumi kuwa (Moi) tumetenga wodi kwa ajili ya majeruhi wa ajali za pikipiki... (hili) siyo kweli. Hata viongozi wa waendesha pikipiki wa Temeke kupitia umoja wao walishafika kuuliza hilo, tukawahakikishia kwamba majeruhi wote wanalazwa kwenye wodi moja bila kubaguliwa na hivyo hakuna sehemu maalum kwa ajili yao," alisema.
Akieleza zaidi, Mvungi anasema kuwa kwa ujumla hali siyo nzuri kutokana na msongamano wa wagonjwa unaotokana na ajali nyingi za bodaboda.
"Wodi ina uwezo wa kulaza wagonjwa 33 kwa maana ya vitanda vilivyopo, lakini wagonjwa huongezeka na kufikia 90. Hali hii siyo nzuri. Tunalazimika kuweka magodoro chini na kuwapa huduma kwa sababu sisi ni hospitali ya umma, hatuwezi kumkataa mgonjwa anapofikishwa (kwetu) akiwa katika hali yoyote ile," anasema.
Mvungi anasema kuwa mbali na mipango mingine kadhaa waliyo nayo, lakini njia mojawapo ya kukabiliana na changamoto ya mrundikano wa wagonjwa kwenye wodi zao ni kukamilika kwa jengo la ghorofa saba hivi karibuni litakalokuwa na vitanda 380 na vifaa vingine vingi vya kisasa.
"Licha ya hali ngumu iliyopo sasa, (sisi) tunaendelea kuwa taasisi bora inayotoa huduma kwa wagonjwa," anasema.
"Ndani ya jengo hilo tutaboresha zaidi kwa kuwa tunatumia mfumo wa kompyuta na kuachana na mafaili (ya makaratasi) katika kuhifadhi taarifa za mgonjwa. Madaktari watakuwa na uwezo wa kuwasiliana na wenzao waliopo nje katika uboreshaji wa huduma za afya," anasema na kuongeza kuwa taasisi yao imetunukiwa cheti cha ubora Afrika Mashariki.
GHARAMA BADO NAFUU
Mvungi anasema gharama za upasuaji ni Sh. 200,000 na za kupokewa kwa huduma za awali ni Sh. 50,000, hiyo ikiwa ni nusu ya gharama halisi.
Anasema katika ajali nyingi za bodaboda, majeruhi huvunjika mfupa mrefu wa mguu ambao hutakiwa kuwekwa vifaa maalum vinavyouzwa nje ya nchi kwa dola 300 za Marekani (Sh. 480,000).
Anasema kwa ujumla, gharama anazolipa mgonjwa ni ndogo kwa kuwa serikali hutoa ruzuku na kwamba, kwa kawaida huwa kuna wagonjwa wa aina mbili; ambao ni wanaolipiwa na Moi baada ya kushindwa kumudu na wengine wanaojilipia wenyewe.
MAJERUHI KUTELEKEZWA WODINI
Anaongeza kuwa majeruhi wengi wa bodaboda hawana uwezo wa kumudu gharama za matibabu na kwamba umoja wao (waendesha bodaboda) huonekana siku wanayoletwa hospitalini, lakini baadaye wenzao wote hupotea na mgonjwa kukosa wa kumhudumia, labda itokee bahati mbaya kwamba mgonjwa apoteze maisha na ndipo hapo waliomleta na kumsaidia katika siku za awali huonekana tena.
"Wengi wa vijana hawa ni wale ambao wanategemea bodaboda kwa ajili ya kujipatia kipato. Wengine ni za kwao na wengine za matajiri... hawa, wengi hutelekezwa na Moi hulazimika kuwagharimia," anasema Mvungi.
Mvungi anaelezea changamoto nyingine kuwa ni kutelekezwa hospitali kwa majeruhi wa bodaboda. Anasema kundi la waendesha pikipiki au watembea kwa miguu huokotwa kama wagonjwa wasiofahamika na kwamba wanapofikishwa kwao, hutibiwa kwa matarajio kuwa wakizinduka ndugu zao watajitokeza au wakipona watalipia gharama wenyewe; lakini kwa baadhi yao hali huwa tofauti kwani hushindwa kulipia kutokana na vipato vyao kuwa duni.
"Ni mzigo kwa taasisi kumlisha mgonjwa, kumtunza na kumuwekea vifaa maalum ili arejee katika hali yake ya kawaida. Lakini kupitia sera ya msamaha wa matibabu, wagonjwa wa aina hii huwa wanasamehewa," anasema na kuwashauri madereva wa bodaboda kujiunga na bima ya afya ili wanapopata ajali au kuugua iwe rahisi zaidi kwao kupata matibabu.
MTAALAM WA USAFIRISHAJI ANENA
Mkufunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Injinia Hans Mwaipopo, anasema vyanzo vya ajali ni vitatu ambavyo ni binadamu anayechangia kwa asilimia 76, chombo anachotumia asilimia 16 na mazingira asilimia nane.
Anasema binadamu anachangi kwa asilimia hiyo kutokana na ukosefu wa elimu ya usalama barabarani kwa vile wengi hawajui sheria zinazowaongoza wawapo barabarani.
Mwaipopo anasema pia tabia ya kupuuza sheria kwa wanaofahamu huchangia ongezeko la ajali; kuporomoka kwa maadili kwani sasa ni rahisi mtu kupata cheti kwamba amesomea na kukionyesha hata kama hajawahi kusomea udereva.
Aidha, Mwaipopo anaongeza kuwa lipo pia tatizo la watu kupewa vyombo vya moto bila kujihakikishia kuwa ni wazima kiakili kwani upo uwezekano kwa watu wenye matatizo ya akili kuendesha vyombo vya moto kama pikipiki na hivyo kuhatarisha maisha ya watu wasio na hatia.
Mkufunzi huyo anasema katika nchi nyingi zilizoendelea, kabla ya mtu kukabidhiwa leseni anapimwa akili na hilo pia linapaswa kuzingatiwa ili kupunguza ajali.
Mwaipopo anasema sheria namba 30 ya 1973 na marekebisho yake inasema dereva mwenye leseni halali anatakiwa kuwa na sifa kuu tatu, ambazo ni pamoja na kusomea udereva katika chuo kilichosajiliwa na chenye walimu na macho yake yawe yanaona vizuri.
Sifa nyingine ni kutokuwa na ulemavu unaoweza kuathiri chombo cha moto anachoendesha, kuwa na akili timamu, awe na afya njema na asiwe na maradhi yenye kuathiri chombo anachoendesha kama ugonjwa wa moyo, sukari na kifafa.
" Leo hii wapo madereva wana matatizo ya kifafa. Tukifanya ukaguzi, tutabaini kwamba wapo wengi wana matatizo ya macho, kifafa, moyo na sukari lakini wanaendesha vyombo vya moto. Hii ni hatari," anasema.
Anasema chombo kinachangia kwa asilimia 16 kwa maana ya matumizi mabaya, ikiwa ni pamoja na chombo kwisha muda wake wa matumizi, lakini bado kinaendelea kubaki barabarani.
Anasema mazingira yanachangia kwa asilimia nane, ikitokana na miundombinu mibovu na kukosekana kwa alama muhimu katika barabara na pia barabara kulazimishwa kona pasipostahili na nyingi kujengwa chini ya kiwango.
Anasema changamoto iliyopo kwa watu wa bodaboda, ni tabia ya wengi wao kufundishana wao kwa wao. Hawajifunzi sheria za usalama barabarani na hivyo hujiona wenye haki kuliko watumiaji wengine.
"Mara kwa mara huwa tunawaona... mtu anatakiwa kupita kushoto, yeye anapita kulia na hawana kofia ngumu... katika hili hatuwezi kutafuta mchawi, ni lazima ajali zitaendelea kutokea na vifo na majeruhi kuongezeka," anasema.
AJIRA NA FOLENI
Bodaboda zimekuwa zikisaidia kupunguza tatizo la usafiri katika maeneo mengi nchini. Katika maeneo ya mijini kama Dar es Salaam ambako tatizo la foleni limekosa suluhu ya haraka, bodaboda ndiyo kimbilio.
Kwenye maeneo yasiyofikika kirahisi kwa usafiri wa gari, hasa vijijini, bodaboda pia zimetwaa nafasi. Vyombo hivi ni mkombozi pia wa Watanzania, hasa vijana wanaokabiliwa na tatizo la ajira.
Dereva Sudi Hassan wa Mbagala Charambe anasema kuwa kwa wastani, kila siku huwa hakosi kuingiza Sh. 20,000, sawa na Sh. 600,000 kwa mwezi na kiasi hiki ni kikubwa mno kulinganisha na wastani wa pato la Mtanzania kwa mwaka (2013) ambalo ni Sh. 1,186,424, sawa na Sh. 98, 868.67 kwa mwezi, au Sh. 3,295.62 kwa siku; hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa taarifa ya serikali iliyotolewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwenye Mkutano Mkuu wa 30 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) uliofanyika jijini Tanga Mei 14, 2014.
Hata hivyo, vifo vya ajali za vyombo hivi vinavyosababisha kuongezeka kwa idadi ya wajane na watoto yatima nchini huhalalisha hisia kwamba pamoja na faida zake, bodaboda ni "muuaji wa kimyakimya".
Ajali za bodaboda zimekuwa zikichangia ongezeko la yatima. Takwimu zilizowahi kutolewa mwaka 2011 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, zilionyesha kuwa Tanzania ilikuwa na watoto yatima milioni 2.4 hadi kufikia mwaka 2011; kati yao wasichana wakiwa 1,055,000 na wavulana 1,345,000.
Aidha, ajali za bodaboda zinaathiri uchumi wa watu mmoja mmoja na taifa. Kwa mujibu wa Kamanda Mpinga, idadi ya pikipiki zilizohusika katika ajali mwaka 2013 peke yake ni 8,241. Hivyo, ikiwa kila pikipiki hununuliwa kwa wastani wa Sh. milioni 2 na kisha kuharibika kabisa baada ya kupata ajali, maana yake jumla ya Sh. bilioni 16.48 zilipotea katika kipindi cha mwaka 2013.
Kadhalika, vipato vya watu wanaotegemea pikipiki hizo kwa shughuli za kibiashara viliathirika kwa kiasi kikubwa kwani, kama kila dereva wa bodaboda alitarajia kuingiza wastani wa Sh. 600,000 kwa mwezi (kama ilivyo kwa dereva Hassan wa Mbagala Charambe), maana yake ni kwamba pato la jumla ya Sh. 7,200,000 lilipotea kwa kila pikipiki kwa mwaka 2013. Hivyo, kwa taifa zima (pikipiki 8,242), kiasi kilichopotea kutokana na bodaboda zilizohusika katika ajali ni Sh. bilioni 4.94. Kwa makadirio ya jumla, hasara iliyotokana na gharama za kuharibika kwa pikipiki hizo pamoja na kipato kilichopotea kwa kutokuwapo barabarani kwa pikipiki hizo kwa mwaka wa 2013 ni takriban Sh. bilioni 21.
UZOEFU WA UGANDA
Changamoto zitokanazo na ajali za bodaboda zipo pia katika nchi nyingine za Afrika, Mashariki. Kwa mfano, nchini Uganda, mwaka 2011 pekee, madereva wa bodaboda 570 walifariki dunia. Wodi ya dharura katika Hospitali ya Rufaa ya Mulago jijini Kampala imepachikwa jina la "bodaboda" kutokana na kuwa na majeruhi wengi wa ajali za bodaboda. Hospitali hii peke yake, kwa mwaka hupokea wastani wa majeruhi 7,280, sawa na majeruhi 20 kwa siku.
KAULI ZA MADEREVA
Frank Chungu aliyefanya kazi ya kuendesha pikipiki kwa miaka mitano katika kijiwe cha Mwenge jijini Dar es Salaam anasema chanzo cha ajali nyingi za bodaboda ni matumizi ya vilevi kama bangi na pombe kali za kwenye vipakiti ambayo hutumiwa na waendesha pikipiki wengi.
Anasema wengine hujifunza kwa muda mfupi na kuingia barabarani kama madereva kamili na matokeo yake, wengi kati ya hao hawafuati sheria za usalama barabarani na kujiweka katika hatari kubwa ya kupata ajali.
"Wengi hawaheshimu taa za barabarani, Wanapita upande ambao siyo sahihi. Hawako makini, wanatumia pombe … na kuvuta bangi. Kwa hali kama hii ni lazima kutakuwa na ongezeko la ajali," anasema.
Chungu anasema hivi sasa walau kuna mabadiliko kidogo ukilinganisha na miaka michache iliyopita hasa kutokana na wengi wa madereva kuingiwa woga baada ya kushuhudia wenzao wengi wanavyojeruhiwa na kupata ulemavu wa kudumu na wengine kupoteza maisha huku wakiacha wake na watoto zao.
Kuhusu leseni, anasema kwa sasa wengi wao wana leseni, lakini tatizo ni kwamba, hawajifunzi kwa umakini kwani wapo wanaokwenda kujifunza uwanjani siku ya kwanza na ya pili yake wanaingia barabarani kupakia abiria.
Anasema wengine huendesha kwa kasi kubwa kwa sababu tu ya kutaka wasifiwe kuwa wao ni mahiri na kwa bahati mbaya, kadri pikipiki inavyozidishwa mwendo ndivyo inavyokuwa nyepesi kuiendesha na hivyo dereva kusahau kuwa tofauti na gari, wao wakipata ajali ni miili yao ndiyo hujigonga na hivyo kuwa katika hatari kubwa zaidi ya kupoteza maisha au kuwa walemavu.
NINI CHA KUFANYA
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamanda Mpinga, anasema kwa mujibu wa sheria ya usalama barabarani, sura ya 168 kama iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, mtu yeyote, ili apate leseni ni lazima kwanza apate mafunzo kwenye vyuo vya udereva.
Kuhusu madereva pikipiki anasema Chuo cha Ufundi Stadi (Veta), wanaendesha programu ya mafunzo kwa madereva pikipiki, lakini kinachosikitisha wengi hawapendi kwenda kujifunza.
Anasema wengine wanaotoa mafunzo ni wadau mbalimbali wa masuala ya usalama barabarani ambao hupita kwenye maeneo ya vijiwe vya madereva wa bodaboda kwa ajili ya kufundisha matumizi ya pikipiki yanayozingatia usalama wa waendeshaji wa vyombo hivyo na abiria wao.
Kutokana na kasi ya utoaji wa mafunzo kwa sasa, kati ya waendesha pikipiki 700,000 waliopo nchini kote, asilimia 70 tayari wamepata leseni.
Injinia Mwaipopo anasema ni lazima serikali ichukue hatua madhubuti za kuwafundisha waendesha pikipiki wote ambao wanategemea kazi hiyo kama ajira yao ya kila siku katika kujiingizia kipato.
"Ukitaka kukamua jipu huwezi kulikanda. Lazima ukamue usaha wote utoke, na ndiyo pona ya mgonjwa... ajali nyingi, wengi hawajui sheria na hawataki kujifunza. Lazima tuchukue hatua mapema vinginevyo idadi ya walemavu itaongezeka siku hadi siku," anasema.
CHANZO: NIPASHE