Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JE UNAJUA KWA NINI IPTL INATESA VIGOGO WA TANZANIA NA KUWAFANYA WAKOSE USINGIZI? SOMA HAPA

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema
Wakati mbivu na mbichi kuhusu sakata la uchotaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 za Escrow akaunti iliyopo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zikitarajia kujulikana wiki hii, habari za kina zaidi zinazowafanya wakubwa serikalini wakose usingizi zimezidi kubainika.


Taarifa ambazo NIPASHE imezikusanya kwa muda mrefu kutoka vyanzo mbalimbali, zinaonyesha kuwa sakata hilo linawatesa wakubwa katika kipengele cha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), mkataba ulivyofikiwa kati ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na IPTL, kukiukwa kwa taratibu na jinsi fedha hizo zilivyotolewa BoT.

Sababu nyingine ni jinsi Tanesco na IPTL walivyoingia katika mgogoro kuhusiana na ukokotoaji wa kiwango cha malipo ya uwekezaji na hatimaye mgogoro huo kuwasilishwa katika Mahakama ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICSID).

TANESCO ILIVYOINGIA MKATABA NA IPTL
Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali zinaeleza kuwa  Mei 26,  1995 , Tanesco iliingia katika makubaliano ya ununuzi wa umeme (Power Purchase Agreement – PPA), uliokuwa unazalishwa na IPTL Tegeta, jijini Dar es Salaam.

Makubaliano haya ambayo yalikuwa ni ya miaka 20, Tanesco ilitakiwa kulipa IPTL malipo ya manunuzi ya umeme (Energy Purchase Price) na  malipo ya kiwango cha malipo ya uwekezaji (Capacity Purchase Price au Capacity Charge).

Hata hivyo, baada ya miaka kadhaa, IPTL na Tanesco waliingia katika mgogoro mkubwa kuhusiana na ukokotoaji wa kiwango cha malipo ya uwekezaji na suala hilo kuwasilishwa katika Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa (ICSID).

Uchunguzi wa NIPASHE unaonyesha kuwa kutokana na mgogoro huo kufikishwa mahakamani, Tanesco walitumia haki yao chini ya PPA kutoa notisi ya pingamizi la malipo (Invoice Dispute Notice), sambamba na kuomba kufunguliwa kwa Akaunti Maalum (Escrow Account), ili malipo yote yalipwe kwenye akaunti hiyo hadi pale migogoro hiyo itakapotatuliwa.

AKAUNTI YA ESCROW ILIVYOFUNGULIWA
Uchunguzi umebaini kuwa Julai 5, 2006, Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, IPTL na BoT waliingia katika makubaliano ya kufungua Akaunti Maalum (Escrow Account) ambayo serikali ingetekeleza Makubaliano ya Utekelezaji chini ya PPA kwa kuweka fedha katika akaunti hiyo.

Chini ya makubaliano hayo, fedha hizo zingeendelea kushikiliwa na BoT mpaka pale IPTL na serikali wangekuwa wamemaliza tofauti zao kuhusu viwango vya malipo ya uwekezaji.

 Kwa mujibu wa Kifungu 7.7 cha Makubaliano ya Ufunguzi wa Akaunti (Escrow Agreement), fedha zilizomo kwenye akaunti hiyo zingeendelea kuwapo na kuwa katika mamlaka ya “Escrow Agent” ambaye ni BoT, na zingetolewa tu kama kuna hukumu ya Mahakama inayoamuru kutolewa kwake au kama pande mbili za Makubaliano (IPTL na Serikali) zitawasilisha makubaliano yanayoridhia kutolewa kwa fedha hizo kwa upande uliotajwa katika Makubaliano hayo.

MGOGORO ULIVYOAMLIWA NA MAHAKAMA
Uchunguzi wa NIPASHE umeendelea kubaini kuwa Mahakama Kuu ya Tanzania ilitoa uamuzi Septemba 5, 2013 uliogusa umiliki wa fedha zilizopo katika Akaunti ya Escrow iliyokuwa chini ya udhibiti wa BoT.

Kutolewa kwa uamuzi kulitokana na maombi yaliyokuwa yamefanywa na mmoja wa wanahisa wa IPTL –VIP Engineering & Marketing Limited (VIP) ambaye aliiomba mahakama iridhie kufutwa kwa shauri ambalo VIP walikuwa wamelifungua Mahakamani (Misc. Civil Application No. 49/2002 & Misc. Civil Application No. 254/2003).

Maombi hayo yalitokana na makubaliano ya mauzo ya hisa za VIP katika IPTL kwenda kwa kampuni ya Pan African Power Solutions (T) Limited (PAP).

 Uchunguzi unabainisha kuwa katika uamuzi huo, Mahakama pamoja na mambo mengine iliridhia kufutwa kwa mashauri hayo na kuelekeza kwamba mali zote za IPTL, kikiwamo kiwanda cha kufua umeme zikabidhiwe kwa mmiliki mpya wa IPTL ambaye ni PAP.

Baada ya uamuzi huo, BoT ilipokea mawasiliano mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Madini (MEM) na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambao walikuwa na maoni kwamba fedha zilizopo kwenye Akaunti ya Escrow zitolewe baada ya masharti kadhaa kutekelezwa.

MASHARTI YALIYOTOLEWA KABLA KUTOLEWA FEDHA BOT
Taarifa zinaonyesha kwamba kabla ya kutolewa fedha hizo, kulitolewa masharti kadhaa kwamba utolewe ushahidi kama PAP ndiyo wamiliki wa hisa za Mechmar katika IPTL, kufikiwa kwa muafaka wa mgogoro wa ukokotoaji wa kiwango cha Malipo ya Uwekezaji kati ya IPTL na Tanesco.

Sharti jingine lililowekwa ni kwamba kuwapo na hakikisho baada ya kulipwa kwa fedha hizo, IPTL hawatadai chochote kuhusiana na tozo zinazobishaniwa.

WIZARA YA NISHATI NA MADINI ILIVYOSHIRIKI
Uchunguzi unaonyesha kuwa baada ya kuwekwa masharti hayo, Septemba 24, 2013, Wizara ya Nishati na Madini iliitisha  mkutano kwa ajili ya kujadili maombi ya Serikali ya kuruhusu kutolewa kwa fedha za Escrow. Katika mkutano huo uliomshirikisha Gavana wa BoT, Katibu Mkuu Hazina, Mwakilishi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na wawakilishi wa Tanesco, BoT ilitoa hoja tano ambazo ilitaka zizingatiwe kabla ya kutolewa ridhaa ya kutoa fedha hizo.

Hoja hizo zilikuwa ni kupata ushahidi kama hisa za Mechmar zinamilikiwa na PAP na ushahidi kwamba umiliki huo umesajiliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na ushahidi wa suluhu ya mgogoro kuhusu tozo kati ya IPTL na Tanesco.

Hoja nyingine zilizotolewa na BoT ni kujua iwapo IPTL na serikali wako tayari kusamehe riba inayotolewa kwa dhamana za Serikali ambako fedha za “Escrow” zimewekezwa; kauli ya Wizara ya Fedha na Uchumi kuhusiana na uamuzi wa kutolewa kwa fedha hizo na iwapo viongozi wa kitafa wana taarifa juu ya suala hilo.

 Nyingine ni iwapo serikali imejihami dhidi ya uwezekano wa madai yanayoweza kufunguliwa na wadai mbalimbali, wakiwamo Standard Chartered Bank (Hong Kong) ambao wanadaiwa kuidai IPTL.

 Uchunguzi zaidi unaonyesha kuwa kufuatia  hoja hizo za BoT, iliundwa timu ya wataalam ili kuzifanyia kazi hoja hizo zilizoibuliwa na kujadiliwa, na kuwasilisha ripoti kwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishatri na Madini kwa hatua zaidi.

 Taarifa zinaeleza kuwa ripoti hiyo ilikamilika na kuwasilishwa Septemba 30, 2013, ikiwa na mapendekezo yaliyohitaji kufanyiwa kazi kabla ya kutekelezwa kwa uamuzi wa mahakama kuhusu kutolewa kwa fedha. Mapendekezo hayo yalishabihiana na hoja zilizokuwa zimetolewa na BoT.

USHIRIKI WA AG  NA KATIBU MKUU NISHATI
Taarifa zinaonyesha kuwa baada ya kuwasilishwa kwa ripoti hiyo, BoT ilipokea nakala ya barua ya Oktoba 7, 2013, iliyotoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali akielezea msimamo wake kuhusiana na yale yaliyoelezwa na timu ya wataalamu.

 Katika ushauri wake, AG alishauri kwamba, baada ya kufikia muafaka kuhusu mgogoro wa tozo kati ya IPTL na Tanesco, fedha zilizomo katika Escrow Account zilipwe kwa IPTL kama uamuzi wa Mahakama ulivyoelekeza.

Aidha, Oktoba 15, 2013, BoT ilipokea nakala ya barua iliyoelekezwa kwa Katibu Mkuu Hazina, ikinukuu ushauri uliotolewa na AG na kushauri kwamba uamuzi wa Mahakama utekeleze ili kuiondolea Serikali madhila ya mashauri yanayoweza kuepukika. Barua iliandikwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini.

JINSI FEDHA ZILIVYOTOLEWA BoT
Taarifa zaidi zinaonyesha kuwa ilipofika Oktoba 21 mwaka 2013, Serikali ya Tanzania na IPTL walisaini makubaliano ya kutoa fedha zilizomo katika Escrow Account ili zilipwe kwa IPTL makubaliano yaliyojulikana kama “Agreement for Delivery of Funds to Independent Power Tanzania Limited”.

 Makubaliano hayo yaliambatana na muhtasari wa kikao cha pamoja cha uhakiki wa malipo ya tozo kati ya IPTL na Tanesco, pamoja na barua ya  Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini ikiwasilisha makubaliano hayo na kuiomba BoT iliruhusu malipo hayo kwenda IPTL kama uhakiki ulivyobainisha.

 Hata hivyo, habari zinasema kabla ya kufanyika kwa malipo hayo, BoT ilimuandikia barua Katibu Mkuu Hazina ikimuomba kuchukua hatua kadhaa kuhusiana na malipo ya IPTL. Miongoni mwa mambo yaliyoshauriwa na BoT ni ufungaji wa Escrow Account uzingatie kwamba mamlaka ya kufanya hivyo yako kwa Mlipaji Mkuu wa Serikali (Paymaster General) na kutokana na unyeti wa suala hilo na ukubwa wa malipo husika, Waziri wa Fedha apate fursa ya kuwajulisha viongozi wakuu wa kitaifa.

 Pia BoT ilitoa ushauri kuwa serikali iombe kutolewa kwa kinga itakayoikinga dhidi ya madai yanayoweza kujitokeza baada ya malipo hayo kufanyika.

Kutokana na ushauri huo, vyanzo mbalimbali vinaonyesha kwamba Oktoba 27, 2013, IPTL ilitoa hati ya Kinga (Indemnity) ambayo iliikinga BoT pamoja na serikali dhidi ya madai yote, ya sasa na ya baadaye, mashauri ya kisheria, pamoja na kuahidi kuzifidia BoT na serikali gharama na tozo zozote ambazo zitawagharimu au zitakazotokana na uamuzi wao wa kuruhusu kuchukuliwa kwa fedha za Escrow au sehemu ya fedha hizo, kwa mujibu wa Makubaliano ya Kutoa Fedha.

USHAURI WA AG ULIVYOSABABISHA SERIKALI KUKOSA KODI
Taarifa zinaonyesha kuwa Mamlaka ya Mapato (TRA) iliomba msaada wa Katibu Mkuu Hazina katika kukata kiasi cha Sh. bilioni 26.9 kama VAT kwa malipo ambayo yaliwekwa kwenye akaunti ya Escrow ambazo zilikokotolewa kutoka katika kiasi cha Sh. 176,649,195,314.00 ambazo zilikadiriwa kuwapo katika akaunti hiyo.  Hata hivyo, katika ushauri ambao ulitolewa na AG Novemba 18, 2013, ilielezwa kwamba malipo ya Capacity Charge hayakuhusisha VAT na kwamba kiasi chote kilichokuwamo katika Escrow Account kilikuwa ni malipo ya IPTL pasipo na VAT.

 Vyanzo vinaeleza kwamba ushauri huo wa AG ulitokana na barua ya BoT na ya Katibu Mkuu Hazina ambazo ziliomba ufafanuzi kuhusu suala hilo kabla ya uhamishaji wa fedha kwenda IPTL.

UTEKELEZAJI WA MAAGIZO YA KUHAMISHA FEDHA
Taarifa zinazidi kueleza kuwa utekelezaji wa maagizo ya kuhamisha fedha za capacity charge zilikuwa katika makundi mawili, ambayo ni katika fedha za Kitanzania, wakati kiasi kingine kilikuwa katika dola za Marekani.

Makundi hayo mawili ya fedha yalikuwa yamewekezwa katika uwekezaji wa ndani na wa nje, kwa kuzingatia kifungu 3.4 cha Escrow Agreement na kiasi kilichokuwa kimewekezwa nje ya nchi kilikuwa ni Dola za Marekani 22 milioni, wakati fedha za Kitanzania ziliwekezwa katika hati fungani za siku 182.

Uchunguzi huo umebaini kuwa malipo ya fedha taslimu, yaani dola za Marekani 22,198,544.60 na  Sh. 8,020,522,330.37 yalilipwa Novemba 28, 2013, uhamisho wa hati fungani ulifanywa Desemba 5, 2013, hatua ambazo zilihitimisha jukumu la BoT kama wakala wa akaunti ya Escrow.

Baada ya kuhitimishwa kwa malipo hayo Desemba 19, 2013, BoT ilimuandikia Katibu Mkuu Hazina kuomba kufungwa rasmi kwa akaunti hiyo, kwa vile madhumuni ya kufunguliwa kwake yalikuwa yamefikia tamati.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com