Walimu wawili wanaojitolea katika Shule ya Msingi Msali, Kata ya Nyakahura, wilayani Biharamulo, mkoani Kagera wanatumia vipande vya mihogo mikavu na mkaa kuandikia ubaoni baada ya kukosa chaki.
Wakizungumza shuleni hapo juzi, walimu hao walisema hawana chaki za kuandikia na kwamba wanatumia vitabu viwili vya hesabu na kiswahili kufundishia wanafunzi 200.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Evelina Jeremiah alisema shule hiyo ilianzishwa mwaka mmoja uliopita kutokana na uwapo wa watoto wengi ambao hawajaenda shule lakini haijasajiliwa.
Alisema baada ya kuwa na idadi kubwa ya watoto, wazazi walianzisha banda la kuwafundisha kusoma, kuandika na kuhesabu hali iliyosababisha kuajiri vijana waliomaliza kidato cha nne kuwafundisha.
Jeremiah alisema licha ya kukosa chaki na vitabu, kuna upungufu wa madawati na madaftari kwani wanafunzi hao hawapati mahitaji muhimu ya shule ukilinganisha na wenzao wa shule nyingine za Mzani na Nyakahura.
“Tunafundisha kwa taabu maana hata mshahara tunalipwa na wazazi Sh30,000 kwa mwezi, lakini kupatikana kwake ni kuvutana na kutufanya tuishi maisha ya ombaomba,” alisema.
Naye Mwalimu Robert Mussa alisema matatizo mengine ni kuvuja kwa jengo linalotumika kama darasa wakati wa mvua na kuathiri ufundishaji.
Diwani wa Kata ya Nyakahura ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo, Apolinary Mugarula alikiri kuwapo kwa shule hiyo na kwamba, ilianzishwa kinyemela na wafugaji wa eneo hilo bila usajili.
Mugarula alisema tayari uongozi wa kata umetoa maagizo kwa walimu wa shule hiyo kufuata chaki Shule ya Msingi Mzani na vitabu vya kufundishia, wakati utaratibu wa kuisajili ukiendelea.
Alisema matatizo ya shule hiyo ni mengi hasa madarasa, vyoo, madawati na nyumba ya walimu.
Diwani huyo wa Kata ya Nyakahura aliongeza kwamba, kubwa zaidi ni kuwaweka walimu waliopitia mafunzo chuoni badala ya vijana wasiotambua maadili ya utumishi kitaaluma.
Na Shaaban Ndyamukama-Biharamulo