KUHUSU MWANAMKE ALIYEHUKUMIWA JELA MIAKA 6 KWA KUUA KWA KISU MZAZI MWENZAKE JIJINI DAR ES SALAAM



Fatuma Seleman, mkazi wa jijini Dar es Salaam, amehukumiwa kwenda jela miezi sita baada ya kukiri mahakamani kosa la kumuua kwa kisu bila kukusudia mzazi mwenzake, Seleman Ramani.



Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Kwey Rusemwa anayesikiliza kesi za mauaji ya bila kukusudia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyopewa kibali na Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.

Fatuna alikuwa na uhuasiano ya kimapenzi na Ramani na walifanikiwa kupata mtoto mmoja.

Ilidaiwa kuwa Oktoba 27,mwaka 2012 eneo la Magomeni Makuti, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alimuua bila kukusudia Ramani.

Ilidaiwa kuwa siku ya tukio, mshtakiwa alikwenda kuomba fedha ya matibabu ya mtoto nyumbani kwa mzazi mwenzie  hakumkuta na alilazimika kumsubiri na kwamba aliporejea alimweleza shida yake, lakini aliambulia lugha ya matusi.

“Nilipoona ananitukana niliamua kuepusha shari nikaondoka kurudi nyumbani kwangu… bila kutarajia mzazi mwenzangu alikuja akaendelea kunitolea lugha ya matusi huku akinishushia kipigo katika kujihami nilichukua kisu nikamchoma” alidai na kuongeza:

“Baada ya tukio hilo nilikwenda kuwaeleza ndugu zake wakamchukue kumpeleka hospitali na baadaye nilijisalimisha polisi kwamba nimemchoma kisu mzazi mwenzangu.”

Hakimu Rusemwa alisema baada ya mshtakiwa kukiri makosa yake mahakama imemtia hatiani na inamhukumu kwenda jela miaka sita kwa kuua bila kukusudia.

Wakati huohuo, mahakama hiyo imemhukumu kwenda jela miaka mitano,  Ally Rashid baada ya kukiri kumuua bila kukusudia mpezi wake, Agnes Nyerenda.

Ilidaiwa kuwa Rashid na Nyerenda walikuwa wana uhusiano wa kimapenzi na kwamba waliishi nyumba moja kama mke na mume.

Ilidaiwa kuwa Mei 3, mwaka 2009 eneo la Mbezi jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alimpiga na kumsababishia majeraha kutokana na wivu wa mapenzi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post