Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAHABUSU KWA WANAOKWEPA KULIPA KODI SASA KUFUNGULIWA SHINYANGA


Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Annarose Nyamubi


 Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Annarose Nyamubi amesema mkoa wa Shinyanga unakusudia kufungua mahabusu kwa ajili ya wafanyabiashara wanaokwepa kulipa kodi kwani kitendo kutolipa kodi ni uhalifu na katika nchi zingine ni kosa la jinai.

Nyamubi aliyasema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa maadhimisho ya nane ya siku ya mlipa kodi mkoa wa Shinyanga yaliyofanyika katika viwanja vya Shycom mjini Shinyanga ambapo alikuwa mgeni rasmi akimwakilisha mkuu wa mkoa wa Shinyanga Ally Rufunga.

Kaimu mkuu huyo wa mkoa wa Shinyanga alisema wafanyabiashara wengi wanakwepa kulipa kodi na njia nzuri ya kuwashughulikia ni kuwafungulia mahabusu maalumu kwani kukwepa kulipa kodi ni uhalifu na hawapaswi kufumbiwa macho.

“Tumesikia mamlaka ya mapato ikilalamika kuhusu baadhi ya wafanyabiashara kukwepa kulipa kodi,hii haikubaliki,uongozi wa mkoa uko tayari kufungua mahabusu kwa wakwepa kodi,kwani katika baadhi ya nchi ni kosa la jinai”,alisema Nyamubi.

Katika hatua nyingine aliwataka wananchi kujenga tabia ya kudai risti sahihi ya bidhaa ama huduma wanayopewa na wafanyabiashara huku akiwaasa wafanyabiashara kutoa risti sahihi kwa kila mauzo na manunuzi wanayofanya.

Awali akizungumza katika maadhimisho hayo kaimu meneja wa mamlaka ya mapato mkoa wa Shinyanga Norbertus Tizibazomo alisema katika kukabiliana na changamoto ya wafanyabiashara kukwepa kulipa kodi wataanza kutangaza majina ya wakwepa kodi kwenye vyombo vya habari ili jamii iwatambue.

“Tuna mpango wa kuwatangaza kwenye vyombo vya habari wale wote wanaokwepa kulipa kodi,tunataka muwasikie na kuwatambua,tutaendelea kutoa elimu pia kwa wananchi juu ya umuhimu wa kulipa kodi kupitia vikundi mbalimbali”,aliongeza Tizibazomo.

Tizibazomo alisema bado kuna baadhi ya walipa kodi ambao hawajanunua na kuanza kutumia mashine za kielektroniki za kodi na walionunua baadhi yao wanazitumia kinyume cha sheria.

 Aidha alisema Mamlaka ya mapato itawachukulia hatua kali ikiwa ni pamoja na kuwafungia biashara na kuwafikisha makahamani wale wote wanaoonesha kukaidi wa maksudi.

Maadhimisho ya nane ya siku ya mlipa kodi mkoa wa Shinyanga yalihudhuriwa na
wafanyabiashara,wanafunzi,wadau wa mamlaka ya mapato,taasisi na idara mbalimbali zinazoshirikiana na mamlaka hiyo kufanikisha ukusanyaji wa mapato huku kauli mbiu ikiwa ni “Risti ni haki yako asiyetoa anakwepa kodi”.

Na Kadama Malunde-Shinyanga


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com