MBUNGE wa Jimbo la Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe, amemtaka Mbunge wa Kigoma Kusini kupitia NCCR Mageuzi, David Zacharia Kafulila, ambaye leo amefunga pingu za maisha na Bi.Jessica kuahirisha kwenda kula fungate (Honeymoon), badala yake warudi bungeni kumalizia sakata la Escrow.
Zitto amesema hayo katika Mji wa Uvinza, Mkoani Kigoma, wakati akitoa salaam za pongezi kwa Kafulila, mara baada ya Padri Joby Joseph kufungisha ndoa ya wawili hao katika Kanisa Katoliki Parokia ya Uvinza, Mkoani Kigoma.
Alisema kwa sasa Honeymoon ya Kafulila ni bungeni kwenda kumalizia suala la ESCROW, kwani ni lazima kuweka maslahi ya nchi mbele kwa maendeleo ya watanzania wote kwa ujumla, huku akimtaka Bi.Jessica kuwa mvumilivu katika hilo.
“Nadhani David (Kafulila), anaingia kwenye historia kwamba atakuwa amefunga ndoa bila honeymoon, kwa sababu honeymoon yake ni bungeni kwenda kumaliza suala la ESCROW,”alisema Zitto.
Kwa upande wake Kafulila amewashukuru wote waliomuunga mkono na kufanikisha suala hilo muhimu katika historia ya maisha yake, ingawa amekiri kwamba amefunga ndoa katika mazingira magumu kutokana na yeye na wabunge wenzake kukabiliwa na majukumu mazito ya kitaifa bungeni likiwemo sakata la ESCROW.
Alisema kuwa kinachoendelea bungeni kuhusu ufisadi wa zaidi ya bilioni 300, ni ufisadi wa historia na kwamba haijapata kutokea nchi ikafanya ufisadi mpaka nchi zote za Ulaya na Marekani zikakata misaada.
“Tunapita kwenye kipindi kigumu na kwa sababu mimi kwa kiasi fulani nimekuwa mstari wa mbele katika jambo hili, nikawa nawaza ndoa na wakati huo huo nawaza ESCROW,”alisema Kafulila.
Social Plugin