Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida Mgana Msindayi ambaye ni mwenyekiti wa wenyeviti nchini akizungumza kwa niaba ya wenyeviti wenzake baada ya mazishi ya mama mzazi wa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga Khamis Mgeja(Bi Halima Nchimika).Picha na Kadama Malunde
Waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa amemtumia salamu za rambirambi mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Shinyanga Khamis Mgeja baada ya kufiwa na mama yake mzazi Halima Nchimika(74) wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya Bugando jijini Mwanza.
Halima Nchimika aliyezaliwa mwaka 1940 alifariki dunia Novemba 18 mwaka huu katika hospitali ya rufaa ya Bugando baada ya kuugua kwa muda mrefu na mazishi yake yamefanyika Novemba 19,2014 katika makaburi ya Uhindini mjini Kahama mkoani Shinyanga.
Akitoa salamu za rambirambi baada ya mazishi kwa niaba ya mbunge wa Monduli Edward Lowassa(waziri mkuu mstaafu),mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Singida Mgana Msindayi ambaye pia ni mwenyekiti wa wenyeviti wa mikoa wa CCM alisema Lowassa amepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha Halima Nchimika.
Katika salamu hizo na pole Lowassa alisema alimfahamu vyema marehemu na kwamba siku za nyuma aliwahi kuishi nyumbani kwa Mgeja akabahatika kupata wosia kutoka kwa mzee huyo na kupiga naye picha mbalimbali za ukumbusho.
“Ndugu yetu Lowassa kanituma nifikishe ujumbe huu,yeye yuko nje ya nchi anawapa pole sana familia ya marehemu,Lowassa aliwahi kuishi hapa kwa Mgeja,anamjua vyema mama yetu aliyetutoka,anawaomba wanafamilia muwe na subira kwa ni mipango ya mungu”,aliongeza Msindayi.
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Kahama Mjini James Lembeli alisema Halima Nchimika alikuwa mtu mwema hivyo kumuasa mtoto wa marehemu Khamis Mgeja kuishi maisha aliyokuwa anaishi mama yake.
“Namfahamu vyema mama huyu ndiyo sababu kubwa ya mimi kufika hapa,alikuwa mtu mwema,pengine hata hii mvua iliyonyesha baada ya kumsitiri mama yetu,watumishi wa mungu mtanisamehe,hii maana yake mwenyezi mungu kampokea huyu mama”,alisema Lembeli.
“Siyo rahisi mtu anazikwa mvua ikanyesha,huyu mama mvua imenyesha,ndugu yangu Mgeja naomba uishi kama alivyoishi mama yako,umati huu siyo bure,alikuwa mama wa watu,nawashukuru viongozi wote mliofika hapa,naomba tuendelee kumwombea mama yetu ili mwenyezi mungu ampokee”,aliongeza Lembeli.
Naye Shehe wa mkoa wa Shinyanga Ismail Habib Makusanya alitaka jamii kutenda mambo mema na kusaidia na kuwapenda wazazi kwani baraka nyingi zinatoka kwa wazazi katika maisha ya mwanadamu.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya familia yake,mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga Khamis Mgeja aliwashukuru mamia ya watu waliojitokeza wakiwemo viongozi wa serikali,siasa,dini,waandishi wa habari na watu wote kutoka ndani na nje ya mkoa wa Shinyanga waliojitokeza kumfariji katika msiba huo mzito kwake.
Hata hivyo katika hali ya kushangaza wakati mwili wa marehemu ukitolewa nyumbani kwao mtaa wa Nyasubi mjini Kahama kuelekea katika msikiti mkuu wa Ijumaa kuswaliwa mvua ilianza kunyesha kisha kukatika na wakati mazishi yakimalizika katika makaburi ya Uhindini mjini Kahama ghafla mvua ilianza kunyesha ikakatika baada ya msafara kufika nyumbani.
|