Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga SACP Justus Kamugisha |
Mwanamke aliyejulikana kwa jina la Regina Salago(24) mkazi wa kitongoji cha Majimaji,kijiji cha Maganzo kata ya Songwa wilayani Kishapu mkoani Shinyanga ameuawa kwa kukatwa mapanga kichwani na mumewe aliyekuwa anamtuhumu kufanya mapenzi nje ya ndoa.
Tukio hilo linalotokana na wivu wa kimapenzi limetokea Novemba 19 mwaka huu saa moja na nusu usiku katika kitongoji cha Majimaji,kijiji cha Maganzo,kata ya Songwa wilayani Kishapu ambapo Malunde1 blog imeambiwa kuwa mwanamke huyo aliuawa kwa kukatwa panga kichwani na kusababisha kifo chake papo hapo.
Walioshuhudia tukio hilo walisema siku hiyo mume wa marehemu Kishimba Care alimfuata mkewe aliyekuwa ametengana naye na kumuomba kurudi nyumbani na alipofika nyumbani alimkata kata mapanga na kupelekea kifo chake.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga SACP Justus Kamugisha alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kutaja chanzo cha tukio hilo kuwa ni wivu wa kimapenzi kwani kulikuwa na ugomvi wa mara kwa mara huku mme akimtuhumu mkewe kufanya mapenzi nje ya ndoa.
Hata hivyo alisema jeshi la polisi linaendelea na msako wa kumtafuta mtuhumiwa wa mauaji hayo huku akitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa mhusika wa mauaji hayo.
Na Kadama Malunde-Shinyanga
Social Plugin