Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TAARIFA KAMILI KUHUSU VURUGU ALIZOFANYIWA JAJI WARIOBA JANA JIJINI DAR ES SALAAM

 

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Warioba, jana alifanyiwa vurugu kubwa zilizosababisha kuvunjika kwa kongamano la kujadili mambo ya msingi ya kuangaliwa katika Katiba inayopendekezwa.
Kongamano hilo liliandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF) na wazungumzaji wakuu walikuwa ni waliokuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Miongoni mwao ni Joseph Butiku, Profesa Mwesiga Baregu, Profesa Palamagamba Kabudi na Humphrey Polepole.

Jaji Warioba alipoanza kuzungumza, ndipo kikundi cha vijana kinachodaiwa kuwa kiliandaliwa dhidi ya kiongozi huyo kilipoanzisha vurugu hizo.

Vijana hao waliingia mapema katika ukumbi wa Ubungo Plaza, jijini Dar es Salaam, lakini baada ya Jaji Warioba kuanza kuzungumza waliibuka na mabango kisha kusogelea jukwaa alikokuwa amekaa Jaji Warioba na wajumbe wenzake.

Mabango mengi yalikuwa yakifanana kwa maudhui, aina ya wino uliotumika na pia hati ilionekana kufanana kwa kiasi kikubwa.

Mabango sita kati ya hayo, ambayo yalishikiliwa na vijana tofauti yaliandikwa kwa kalamu ya wino mzito mwekundu (marker pen) na matatu yalikuwa na ujumbe uliosomeka; "Katiba inayopendekezwa tumeipokea, tumeielewa na tunaiunga mkono."

Mengine matatu ya maandishi ya rangi ya bluu yalisomeka: "Katiba inayopendekezwa tumeipokea, na tunaiunga mkono."

Mengine yalisomeka “Fedha za Magharibi haziwezi kuibomoa nchi yetu, na Wananchi ndiyo wana maamuzi ya mwisho, Tume mnafanya kazi ya nani?”

Hali hiyo ilivunja utulivu ndani ya ukumbi kutokana waliokuwa na mabango kuendelea kuyainua juu huku kundi lingine likiwafuata kuwanyang’anya na kuyachana.

Hali hiyo pia ilisababisha watu waliokuwa ndani ya ukumbi kurushiana viti na kuwalazimisha wengine kutoka nje kuhofia usalama wao.

Kutokana na hali hiyo, Jaji Warioba na wenzake walitolewa katika ukumbi wa mikutano na kuingizwa katika chumba maalum kwa ajili ya usalama wao.

POLISI WAFYATUA MABOMU
Takribani dakika 10 baada ya kuibuka kwa vurugu hizo, polisi walifika katika eneo hilo na kufyatua mabomu ya kutoa machozi yaliyosababisha mamia ya watu waliokuwa katika eneo hilo kukimbia, kuanguka ovyo na wengine kujeruhiwa.

NIPASHE lilishuhudia polisi wakiwa wamewashikilia vijana wawili kwa kuhusishwa na vurugu hizo.

MWANDISHI APIGWA
Baadhi ya watu waliopigwa ni pamoja na Katibu wa Chipukizi na Uhamasishaji wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Paul Makonda na mwandishi wa BBC, Anold Kayanda, ambaye alijeruhiwa kichwani kutokana na vurugu za ukumbini baada ya kurushiwa kiti.

Awali, Jaji Warioba, alisema asilimia 81 ya ibara za Rasimu ya Tume yamo kwenye katiba inayopendekezwa, hata hivyo, maudhui yake yakitazamwa kwa makini mambo mengi ya msingi yametupwa. Aliyataja mambo manne ya msingi yenye kuleta mabadiliko ambayo yalipendekezwa na wananchi yaliyoondolewa kuwa ni tunu za maadili ambazo kwa mujibu wake, zilibadilishwa na kuwa urithi, madaraka ya wananchi, mgawanyo wa madaraka kutengenisha mihimili ya Serikali na Bunge na Muundo wa Muungano.

Alisema kuna baadhi ya mambo yaliyopo kwenye katiba inayopendekezwa yanatia shaka iwapo yatakuwa katika utekelezaji yakiwamo mgombea binafsi na asilimia 50 kwa 50 ya wabunge wanawake na wanaume.

Kuhusu kura ya maoni alisema ni lazima wananchi waandikishwe kwanza kwenye daftari la kupiga kura huku akiwataka kuwa makini kuyapigia kura mambo ya msingi.
Hata hivyo, mdahalo huo haukumalizika kutokana na hali hiyo na hatimaye kufungwa na Katibu Mtendaji wa MNF, Joseph Butiku.

Baadaye, Jaji Warioba alionekana akiondolewa eneo hilo kutoka chumba maalum alichokuwa amewekwa huku akiwa anasindikizwa na watu wa usalama akiwa mzima na kupanda kwenye gari lake na kuondoka eneo hilo.
CHANZO: NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com