Kigogo wa halmashauri ya wilaya ya Geita ambaye ni mtendaji
wa kata ya nkome Wilaya na mkoa wa Geita,Peter Francis Kagoma ameikimbia kata
yake baada ya kudaiwa kuuza ng’ombe wa wizi kwa thamani ya Tshs 350,000.
Kutokana na hali hiyo,jeshi la polisi Wilaya ya Geita limelazimika
kumshikilia Mashauri Magoti(54),mkazi wa kijiji cha Ihumilo kilichopo katika
kata hiyo ambaye inaelezwa alishirikiana na mtendaji huyo kumuuza ng’ombe huyo.
Kwa sasa ng’ombe huyo amekamatwa na analindwa na polisi wa
kituo kidogo cha polisi Nkome hadi hapo mtuhumiwa namba moja ambaye ni mtendaji
atakapopatikana na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Ihumilo ilipoibiwa ng’ombe hiyo
Thomas Alila alidai kuwa,desemba 13 walikuta ng’ombe huyo akiwa ametelekezwa na
mtu asiyejulikana nje ya nyumba ya Mashauri Magoti huku akiwa amefungwa kamba
kwenye mti.
Alila anasema walimchukua ng’ombe huyo hadi ofisi ya
Mtendaji wa kata ya Nkome ambako walimkabidhi kwa Weo Kagoma na mbele ya
mtendaji wa kijiji Charles Buligi kwa lengo la kumtangaza kama utaratibu wa
kisheria unavyoelekeza.
‘’Mtendaji huyo alimuomba Magoti ambaye ng’ombe huyo
alitelekezwa nyumbani kwake kuendelea kumchunga ng’ombe huyo huku wakitoa
matangazo kuona iwapo mwenyewe angepatikana nasi tuliondoka ofisini hapo
tukimuacha ng’ombe huyo baada ya kumkabidhi’’alisema Alila.
Hata hivyo katika hali isiyotarajiwa,desemba 23 mwaka huu
ofisa mtendaji huyo,alimuuza ng’ombe huyo kwa thamani ya Tshs 350,000/=,na
baadaye ng’ombe huyo alikamatwa na wananchi akiwa mbioni kuchinjwa.
‘’Baada ya wananchi kumkamata ng’ombe huyo walinitaarifu na
nilipofika eneo la tukio mnunuzi alikimbia na sisi kama viongozi tulimchukua
ng’ombe huyo na kumfikisha katika kituo cha polisi cha nkome aliko hadi sasa’’alisema
Alila.
Akizungumza na Malunde1 blog kabla ya kukamatwa,mchungaji wa
ng’ombe huyo Magoti ambaye kwa sasa anashikiliwa na polisi,alikiri mtendaji
Kagoma kumuuza ng’ombe huyo nay eye kupatiwa mgao wa Tshs 100,000 kama malipo
ya kumlinda ng’ombe huyo kuanzia alipokutwa ametelekezwa nyumbani kwake hadi
siku ya kuuzwa.
Naye Kagoma alipopigiwa simu na mwandishi wa habari hizi
simu iliita bila kupokelewa.
Mkuu wa kituo cha polisi cha Nkome OCS E 5147 D/CPL Mtawa mbali na kukiri mtendaji
huyo kukimbia na ng’ombe huyo kushikiliwa kituoni hapo alimtaka mwandishi wa
habari hizi kumtafuta kamanda wa polisi mkoa wa Geita Joseph Konyo ambaye ndiye
msemaji mkuu wa jeshi hilo.
‘’Ni kweli ng’ombe yupo kituoni na mtendaji baada ya kumuita
afike kituoni amedai amepatwa dharula ya ghafla na leo siku ya 4 kila ukimpigia
simu anadai yuko visiwa vya wilaya ya Sengerema lakini ukitaka taarifa kamili
mtafute kamanda wa polisi mkoa wa Geita huyo ndiye msemaji wetu’’alisema OCS
Mtawa.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ali
Kidwaka alikiri kupokea malalamiko hayo dhidi ya mtendaji huyo na kuahidi
kufuatilia.
Na Victor Bariety-Malunde1 blog Geita
Endapo una Habari,Picha,Video,Tangazo au Tatizo Lolote wasiliana nasi kwa namba +255 688 405 951