ASKARI POLISI ACHOMWA MKUKI NA WANANCHI HUKO MARA


Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania Ernest Mangu
Askari polisi Deogratius wa Kituo cha Polisi, Kinesi Wilayani Rorya mkoani Mara, amechomwa mkuki na wananchi waliovamia mgodi wa dhahabu wa ACACIA North Mara kwa lengo la kupora mawe.

Kamanda wa Polisi wa Tarime Rorya, ACP Lazaro Mambo, alisema jana kuwa, askari huyo alijeruhiwa na kundi la watu zaidi ya 2,000 lililovamia kwenye mgodi huo Jumanne ya wiki hii.


Alisema wavamizi hao walikuwa na silaha mbalimbali za jadi.

Alisema mara baada ya kuingia ndani ya mgodi huo, watu hao walifanya vurugu kwa kuwashambulia askari na walinzi waliokuwa wakilinda mgodi huo.

Alisema lengo la watu hao lilikuwa ni kupora mawe ya dhahabu yaliyokuwamo.


Alisema jeshi lake likishirikiana na walinzi wa mgodi huo uliopo Nyamongo Wilayani Tarime, lilifanikiwa kuwaondoa wavamizi hao kwa kutumia mabomu.


Alisema katika tukio hilo, askari huyo alijeruhiwa kwa mkuki na amelazwa katika hospitali ya Shirati kwa matibabu.


Alisema hadi sasa wanawashikilia watu sita kwa tuhuma za kuvamia na kujeruhi baadhi ya askari mgodini humo.

Alisema watu hao watawafikishwa mahakamani wakati wowote uchunguzi utakapokamilika.

 Na Samson Chacha - Mara

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post