Kamanda wa polisi mkoa wa Geita Joseph Konyo akizungumza na waendesha bodaboda mjini Geita |
Baadhi ya Askari
polisi Mjini Geita, wamelalamikiwa na waendesha pikipiki maarufu kama
bodaboda kwa kukumbatia rushwa jambo ambalo linawaumiza kiuchumi.
Wakizungumza kwenye Mkutano na kamanda wa polisi Mkoa wa
Geita Joseph Konyo, uliofanyika katika ukumbi wa bwalo la polisi uliopo mjini Geita, baadhi ya waendesha bodaboda walisema kitendo cha kukamatwa na kuombwa rushwa kimekithiri sana katika
mkoa huo.
Mkutano huo ulikuwa na lengo la kujadili kuhusu kukamatwa kwa watu 16 waendesha bodaboda, waliokuwa
katika vurugu ziliz tokea juzi baada ya kumzingira mfanyabishara mmoja Juma
Joseph maarufu (Manyama), anayetuhumiwa kuhusika kupanga mauaji na kupora pikipiki.
“Kamanda tunashukuru kwa kutuita waendesha bodaboda wote
katika ukumbi huu, ili tujadili changamoto za kuuawa kwa bodaboda wenzetu,
lakini kuna jambo ambalo sisi kama waendesha pikipiki linatukera sana la baadhi
ya askari wako wanatuomba rushwa kwa nguvu,”walisema waendesha bodaboda hao.
“Sisi tunapenda sana ushirikiano kati yetu na polisi lakini
kamanda tumekuwa tukihofia kufika kituoni kutoa ushahidi ama malalamiko yetu
kwa sababu wakati mwingine unatoa ushahidi mwisho wa siku unageukwa na kupewa
kesi kuwa wewe ni mhalifu,”alisema Joseph Iddi.
Baada ya kupokea malalamiko hayo Kamanda Konyo, alisema
atayashughulikia na ikibainika askari wake wanahusika moja kwa moja, sheria za
kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao bila kujali cheo cha mtu.
“Niwatoe wasiwasi malalamiko yenu nimeyapokea yote na
niwaahidi nitafUatilia moja baada ya jingine na yeyote atakayebainika amefanya
hayo atashughulikiwa, sisi tupo hapa kwa kushughulikia matatizo yenu, kwanza
hakuna askari yeyote katika nchi hii anayeruhusiwa kunyanyasa raia na suala la rushwa
ni matakwa ya mtu mwenyewe na jeshi letu tunapinga suala la rushwa,’’alisema
Konyo.
Katika hatua nyingine Konyo alimwagiza mpelelezi wa wilaya ya Geita Kinyunko Marlaw, kuwaachia huru waendesha bodaboda 16 waliokamatwa na polisi bila kuwekewa masharti ya aina yeyote lakini
akasisitza kuwa iwapo wataachiwa wasifanye fujo wala kuharibu mali za mtuhumiwa
bali wawe watulivu wakati wakisuburi mtuhumiwa apandishwe mahakamani.
“Jamani waendesha bodaboda nawaomba tuendelee kushirikiana
mnapobaini kuna tatizo ama uharifu tupeane taarifa ili tudhibiti hii hali na
suala la kukamatwa kwa wenzenu 16 nimeshatoa maagizo wadhaminiwe bila masharti,
lakini chonde chonde hawa watu watakapotoka wasifanye vurugu yeyote wala
kuharibu mali za mtuhumiwa hapa haki lazima itendeke hayupo atakayeonewa,”alisema
Konyo.
Social Plugin