MWAKA 2014 unafikia
tamati leo. Kwa Watanzania, kuna matukio mbalimbali yaliyojitokeza
ambayo yameacha kumbukumbu kubwa kwao. Hata hivyo, yafuatayo ndiyo mambo
yaliyotia fora zaidi.
Viungo vingi vya binadamu vikiwa vimetupwa katika machimbo ya kokoto yaliyopo Bunju, Dar.
1.VIUNGO VYA BINADAMU VYASHTUA
Jumatatu
ya Julai 21, 2014, nchi ilipatwa na mshtuko mkubwa baada ya kusambaa
kwa habari kuwa viungo vingi vya binadamu vilikutwa vikiwa vimetupwa
katika machimbo ya kokoto yaliyopo Bunju, Kinondoni jijini Dar es
Salaam.
Watu
wengi waliamini viungo hivyo vimetokana na mauaji ya halaiki, hasa
baada ya kukutwa kwa mabaki ya mikono, miguu, mafuvu, viganja na vingine
vingi. Lakini baadaye ikaja kuthibitika kuwa viungo hivyo vilitupwa
kimakosa na Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU),
ambacho pia kinaendesha hospitali.
Viungo
hivyo mbalimbali vya binadamu vilikuwa vikitumiwa kimasomo na madaktari
wanafunzi, ambavyo vilipaswa kuteketezwa baada ya matumizi. Kitendo
hicho kilisababisha serikali kukisimamisha kwa muda chuo hicho kutokana
na uzembe huo. Viungo hivyo vya binadamu, hupatikana katika maiti
mbalimbali zinazokosa ndugu wa kuwazika na hutolewa na hospitali ya
Taifa Muhimbili.
Kundi lililoitwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA),wakiongozwa na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba.
2.KUZALIWA KWA UKAWA
Baada
ya Rais Jakaya Kikwete kuridhia zoezi la uandikwaji wa Katiba Mpya,
Tume ya kukusanya maoni chini ya uenyekiti wa Jaji Joseph Warioba
ilifanya kazi yake vizuri na mwaka huu katiba hiyo ilipelekwa Bungeni
ambako Bunge Maalum la Katiba lilikutana ili kupitia vifungu vyake kabla
ya kuipeleka kwa wananchi kwa ajili ya kuipigia kura ya kuikubali au
kuikataa.
Kulitokea
malumbano makali kati ya wajumbe wa Bunge hilo juu ya vipengele kadhaa,
hasa muundo wa serikali ya Jamhuri ya Muungano. Wajumbe waliotokana na
Chama Cha Mapinduzi, walipendezwa na muundo wa serikali mbili kama
ilivyo hivi sasa, wakati wapinzani walitaka serikali tatu.
Misimamo
hiyo ilileta utengano mkali kiasi kwamba wajumbe wa upinzani
wakiongozwa na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kuamua kususia
vikao hivyo, wakipinga kile walichokiita uchakachuaji wa rasimu ya
katiba ya Jaji Warioba. Ususiaji huo ulisababisha kuanzishwa kwa kundi
lililoitwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Kuanzishwa
kwa umoja huo uliovihusisha vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na
NLD, kulisababisha kundi hilo kukubaliana kusimamisha mgombea mmoja
katika chaguzi zijazo, wakianzia na uchaguzi wa serikali za mitaa
uliofanyika katikati ya mwezi huu.
3.JAJI WARIOBA APIGWA
Baada
ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kumaliza kazi yake na kuikabidhi
katiba pendekezwa kwa Rais Jakaya Kikwete tayari kwa ajili ya kuipeleka
kwa wananchi ili kupigiwa kura ya maoni, kulikuwa na mkanganyiko
miongoni mwa watu juu ya kilichomo ndani ya katiba hiyo, baadhi
wakipinga kuondolewa kwa vifungu vingi vilivyokuwa na masilahi kwa nchi.
Miongoni
mwa wanaoongoza harakati za kupinga kuondolewa kwa baadhi ya vifungu
vilivyowasilishwa na Tume hiyo, ni Taasisi ya Mwalimu Julius Nyerere
ambayo mara kadhaa imeandaa mijadala ya wazi, lakini wakimtumia Jaji
Warioba kama msemaji wake mkuu.
Kitendo
hicho kimesababisha Warioba kuonekana kama yupo katika mgogoro na chama
chake na siku aliyofanyiwa fujo na kupigwa katika ukumbi wa mikutano wa
Ubungo Plaza, wanaodaiwa kuwa makada wa CCM wanatajwa kuhusika.
Kitendo
hicho pia kilikosolewa na wachambuzi wa habari za kisiasa wakidai
ulikuwa ni udhalilishwaji wa mtu aliyewahi kuwa Makamu wa Rais na Waziri
Mkuu wa Tanzania na hivyo kuhoji ulinzi wake.
4.MISS TANZANIA YAFUNGIWA MIAKA 2
Shindano
la Miss Tanzania limejijengea heshima kwa muda mrefu tokea lilipoanza
tena mwaka 1994. Ingawa kumekuwa na malalamiko ya chinichini juu ya
kuwepo kwa hila, safari hii lilijikuta likipata aibu kubwa, baada ya
mshindi wake wa mwaka huu, Sitti Mtemvu kudaiwa kudanganya umri hivyo
kuibua sauti zilizotaka kunyang’anywa kwa taji hilo.
Baada
ya skendo hiyo kuchachamaa, Baraza la Sanaa la Taifa liliendelea na
uchunguzi wake dhidi ya malalamiko mengi yaliyowahi kuripotiwa na katika
tukio ambalo halikutarajiwa, shindano hilo limesimamishwa kwa miaka
miwili kutofanyika na sababu nyingine iliyosababisha hatua hiyo, ni
kugundulika kuwepo kwa rushwa ya ngono katika hatua mbalimbali za
shindano hilo linaloanzia vitongojini.
5.VIFO VYA WASANII WA MUVI NA MUZIKI
NI
mwaka mwingine ambao wasanii wengi, wakiwemo wacheza filamu na
wanamuziki walifariki dunia. Mei 27 mwaka huu, msanii wa Bongo Muvi,
Rachel Haule alifariki katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Alikwenda
hospitalini kwa ajili ya kujifungua, lakini baada ya kitendo hicho hali
yake ilibadilika ghafla ambapo alihamishiwa ICU na hali yake ilizidi
kuwa mbaya kabla ya kupoteza maisha.
Recho
alifariki wiki moja baada ya muigizaji mwingine maarufu, Adam Kuambiana
kufariki ghafla. Baada ya hapo, msururu wa wasanii ulifuata akiwemo
prodyuza George Tyson, msanii mkongwe katika uchekeshaji Said Ng’amba
‘Mzee Small’, mwanamuziki wa Twanga Pepeta, Khamis Kayumbu ‘Amigolas’,
Side Mnyamwezi, Yesaya Ambilikile ‘YP’ , Maalim Gurumo, Amina Ngaluma,
Aisha Madinda na Shem Kalenga.
6. TEGETA ESCROW NA BILIONI 306
DAVID
Kafulila, mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi) alianza kama utani,
akiwatuhumu vigogo wa serikali kuhusika na wizi wa shilingi bilioni 306,
mali ya umma katika akaunti ya Tegeta Escrow. Mwanasheria Mkuu wa
serikali wakati huo, Jaji Fredrick Werema akamdhihaki kwa kumuita
Tumbili kabla ya kumtishia kumkata kichwa. Dhihaka zikaendelea kwa
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, kuziita
nyaraka alizokuwa nazo Kafulila kuwa ni makaratasi ya kufungia vitumbua.
Kadiri
muda ulivyokuwa unakwenda, ikaja kuthibitika kuwa ni kweli kulikuwa na
uchotwaji wa fedha hizo isivyo halali, kitu kilichosababisha nchi
kuingia katika kashfa nyingine ya mabilioni ya fedha, ukiacha EPA,
Richmond, Rada na Ndege ya Rais.
Mshindo
wa skendo hiyo umeondoka na vigogo watatu, waliotanguliwa na Jaji
Fredrick Werema aliyejiuzulu, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Profesa Anna Tibaijuka aliyeondolewa na Katibu Mkuu Maswi,
aliyesimamishwa ili kupisha uchunguzi dhidi yake.
7.HOMA YA DENGUE
Ni
ugonjwa mpya ambao uliingia na kumshtua kila Mtanzania, kufuatia kasi
yake ya kuua na utata wa tiba yake. Uliwafanya watu kuogopa na kuitaka
serikali kuhakikisha tiba yake inapatikana mara moja ili kuondoa hofu
miongoni mwa wananchi.
8. UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA
INGAWA
umekuwa ukifanyika kila baada ya miaka mitano, lakini uchaguzi wa
serikali za mitaa mwaka huu ulipata hamasa kubwa na kufuatiliwa kwa
karibu na watu wengi. Ingawa kama ilivyotegemewa, Chama Cha Mapinduzi
kuibuka na ushindi, lakini hata hivyo, matokeo yake yalionyesha dalili
za kuimarika kwa vyama vya upinzani baada ya kushinda viti takribani
3000 vya uenyekiti wa serikali za mitaa.
Uchaguzi
huo ambao ulisimamiwa na Tawala za Mikoa (TAMISEMI) iliyo chini ya
ofisi ya Waziri Mkuu, ulikuwa na dosari kadhaa zilizomlazimisha Waziri
wake, Hawa Ghasia, kuwasimamisha kazi Wakurugenzi, kuwafukuza na wengine
kupewa onyo, kufuatia uzembe wao katika kusimamia zoezi hilo muhimu
nchini.
DIAMOND, IDRIS WANG’ARA
Msanii
wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ mwaka 2014 aliwaongoza wenzake
kuing’arisha Tanzania kimataifa baada ya kufanikiwa kutwaa tuzo tano
barani Afrika. Hizo ni pamoja na tatu kutoka kituo cha televisheni cha
Channel O, jijini Johannesburg na The Future Awards Africa iliyofanyika
Lagos, Nigeria.
Ushindi
wake huo ulimfanya kupata mapokezi makubwa ya aina yake alipowasili
Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere na mashabiki
walimsindikiza hadi ukumbi wa Escape One kwa mi guu, umbali wa zaidi ya
km 20.
Aidha
kijana Idris Sultani alikuwa Mtanzania wa pili kushinda shindano la Big
Brother, baada ya Richard Bezuidenhout kuibuka kinara mwaka 2011.
Idris, aliyeshinda Big Brother Hotshots alijinyakulia kitita cha dola
300,000 baada ya kumbwaga Tayo Faniran wa Nigeria.
Endapo una Habari,Picha,Video,Tangazo au Tatizo Lolote wasiliana nasi kwa namba +255 688 405 951