Mahakama ya Wilaya ya Geita
mkoani Geita imetupilia mbali shauri la madai ya uchaguzi wa serikali ya mtaa wa
Nyantorotoro “A” na kuamuru mlalamikaji ambaye ni mgombea wa Chama Cha Mapinduzi(ccm) kulipa gharama za kuendesha shauri hilo.
Akisoma hukumu hiyo leo
mahakamani ,Hakimu mkazi mfawidhi wa
mahakama ya Wilaya ya Geita Desdery
Kamugisha alisema mlalamikaji amekosea madai yake kwa kuomba
mahakama ibatilishe uchaguzi wa mtaa wa Nyakagwe na kwenye maelezo ya shauri analalamikia uchaguzi wa mtaa wa
Nyantorotoro “A”.
Awali mlalamikaji ambaye
alikuwa mgombea wa mtaa huo kupitia Chama Cha Mapinduzi(ccm) Martine Lunzari alidai aondoe malalamiko yake mahakamani kwa muda ili
akafanye marekebisho kwenye hati zake za madai.
Aidha alikiri mahakamani hapo kuwa
hati zake za madai zilikosewa kwa kuandika madai ya mtaa wa Nyakagwe wakati
yeye aligombea mtaa wa Nyantorotoro “A” na kumboa mahakama iondoe hati hizo ili
akafanye marekebisho ili aandike mtaa kwa usahihi.
Akijibu hoja hizo,wakili wa
Chadema Jimbo la Geita Bernard Otieno aliambia mahakama hiyo kuwa mlalamikaji
amekosea kufungua shauri hilo na amekosea msingi wake na amefunga mikono ya
mahakama hiyo kwa kumlalamikia mgombea wa mtaa wa Nyakagwe badala ya mtaa wa
Nyantorotoro “A” na kuiomba mahakama itupiliwe mbali shauri hilo.
Otieno alisema kuwa, mahakama
itupilie mbali shauri hilo kwa sababu kuruhusu
shauri hilo
liendelee ni kukiuka sheria na taratibu hivyo mahakama imefungwa mikono na haina
budi kuifuta na kuamuru kulipa gharama za kesi hiyo.
Akitoa hukumu hiyo hakimu
Kamugisha alisema kuwa, kuruhusu mlalamikaji kufanya marekebisho katika hati
hiyo ya madai itakuwa ni kuruhusu kufuta hoja ya msingi wa shauri lenyewe,hivyo
akatupilia mbali shauri hilo na kuamuru
kulipa gharama za shauri hilo.
Akizungumza na Malunde1 blog Wakili wa Chadema Jimbo la Geita Otieno alisema kuwa shauri hilo lilikuwa na makosa makubwa na ya kisheria
na kumpongeza hakimu kwa kujielekeza vizuri kwa mujibu wa sheria.
Katibu wa Chadema Jimbo la
Geita Mutta Robert,alisema kuwa kesho asubuhi ataenda mahakamani na wakili wao
kupeleka madai ya gharama za shauri hilo.
“Kesho mapema tunaenda
mahakamani na wakili wetu kusajili madai ya gharama za shauri hilo baada ya kushinda mahakamani,pia
tunaendelea kujipanga na wakili wetu kupangua mashauri mengine mawili yaliyobaki”
Katika uchaguzi wa serikali
za mitaa uliofanyika 14 Desemba,2014 katika Halmashauri ya mji wa Geita Chadema
iliishinda vibaya CCM baada ya Chadema kuibuka mshindi katika mitaa 34 na ccm kupata 24 na
kati ya mitaa hiyo,mitaa 4 ccm waliipata kwa kuweka pingamizi na kupita bila
kupingwa.
Matokeo hayo yalionesha
kuwachanganya viongozi wengi wa ccm na kuamua kufungua madai mahakama ya
wilaya.
Mpaka sasa waliokuwa wagombea wa ccm katika mitaa 3 wamepeleka mashtaka
ya madai mahakamani.
Social Plugin