Katika hali isiyokuwa ya kawaida, mwanamume mmoja amewafyatulia
risasi watu wawili na kusababisha kifo cha mmoja kwa kile kinachodaiwa
kumletea usumbufu wakati wa mkesha wa harusi.
Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Ilala, David
Mnyambuga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ingawa hakuwa tayari
kulizungumzia kwa madai kuwa siyo msemaji na anayetakiwa kufanya hivyo
ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala ambaye hakupatikana kulizungumzia
hilo.
Majeruhi wa tukio hilo, Goodluck Madaraka
aliyejeruhiwa na risasi zilipokuwa zinapigwa hewani, alisema saa tano na
nusu usiku walipokuwa wanacheza muziki kwenye mkesha wa harusi, ghafla
jirani yao aliyefahamika kwa jina la Lucas Muhabe alikuja na panga na
kuwafukuza kwa madai kuwa wanampigia kelele.
Alisema Muhabe aliondoka na baada ya muda alirudi
na bastola na kupiga risasi ovyo na kwa bahati mbaya ikampata begani
Mahamudu Muhasi aliyekuwa anapita njia na kumpiga nyingine ya kichwa na
kumuua papo hapo.
“Muhasi alikuwa anapita njia hivyo hata vijana
walivyokimbia yeye hakukimbia na alipopigwa risasi ya bega la kushoto
alilalama kumwambia huyo baba kuwa anamwonea kwani hafahamu kitu
chochote, cha kushangaza baada ya kuambiwa hivyo aligeuka na kumpiga
nyingine ya kichwa na kufariki dunia papo hapo,” alisema Madaraka.
Madaraka alisema kuwa kwenye heka heka za kupigwa
risasi hizo moja ilimpitia kwenye shavu na kumpasua na alikwenda
Hospitali ya Amana na kushonwa nyuzi tatu.
Kaka wa marehemu, Salim Ally alisema kuwa Muhasi
alikuwa anashinda kwake na kulala kwa mjomba wake mbali kidogo kutoka
kwake, siku ya tukio baada ya kula chakula cha usiku na kuzungumza hadi
saa tano usiku, alimsindikiza.
Alisema alipohakikisha wamepita kwenye maeneo
ambayo hakuamini kama ni salama, alimwacha aende mwenyewe, njia kuu
ikiwa ni hapo palipokuwa na mkesha wa harusi na alipata taarifa ndugu
yake ameuawa kwa kupigwa risasi.
“Amekuja mwezi wa saba kutoka Malinyi Ulanga, siyo
mwenyeji na wala hashindi maeneo hayo, ndiyo maana hata wakati vijana
wanakimbia alikuwa anashangaa tu ndiyo akapigwa risasi, inauma sana hata
siamini kama sheria itachukua mkondo wake kwa jinsi ninavyoumia,”
alisema Ally.
Ally aliongeza kuwa, tunasikia mtuhumiwa amesema
marehemu ni jambazi ndiyo maana amempiga risasi, kitu ambacho siyo kweli
hana historia hiyo na ni mgeni hapa jijini.
Akizungumza na gazeti hili Mtawala Amani ambaye
nyumbani kwake ndiyo kulikuwa na mkesha wa harusi, alisema muda wa saa
tatu aliamua kujipumzisha barazani aliamshwa mnamo saa tano na nusu na
kelele zilizokuwa zinatokea nje ya nyumba yake.
Alisema baada ya kutoka nje alikuta damu na mwili
wa kijana Muhasi na kuambiwa kuwa jirani yao Lucas Muhabi ndiyo amemuua
kwa kumpiga risasi na muda siyo mrefu polisi walifika na kuuchukua mwili
kuupeleka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Mke wa Amani, Pili Miraji alisema kuwa anamfahamu marehemu kwa kuwa alikuwa akimwona anapita maeneo hayo na anakwenda kwa mjomba wake ambako siyo mbali kutoka hapo kwao.
Na Kalunde Jamal, Mwananchi
Mke wa Amani, Pili Miraji alisema kuwa anamfahamu marehemu kwa kuwa alikuwa akimwona anapita maeneo hayo na anakwenda kwa mjomba wake ambako siyo mbali kutoka hapo kwao.
Na Kalunde Jamal, Mwananchi