Mkazi wa Tarafa ya Mang’ula wilayani Kilombero mkoani Morogor, Amon Nyenja
amefariki dunia baada ya kuchomwa kwa kisu na anayedhaniwa kuwa ni
hawara wa mke wake mdogo.
Tukio hili lilitokea usiku wa Desemba 23 huko
Mang’ula na inadaiwa kuwa marehemu alirudi nyumbani saa 3.30 usiku na
kumkosa mkewe hivyo kuamua kumtafuta katika maeneo mbalimbali.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mang’ula, Shabani
Lichaula na Mkuu wa kituo cha Polisi Mang’ula, Nkilijia Lazaro walisema
polisi inamshikilia mke huyo mdogo wa marehemu huku likimtafuta
mtuhumiwa.
Lichaula alidai kuwa marehemu katika kumtafuta
mkewe huyo alimkuta akiwa amesimama mahali na mwanamume na mwanamke huyo
alikimbia na kutokomea na marehemu Nyenja aliamua kumvaa mgoni wake
lakini alizidiwa baada ya mtu huyo kumchoma kisu cha ubavuni hadi utumbo
kutoka nje.
Lichaula alisema baada ya Nyenja kuchomwa kisu
alipiga kelele za kuomba msaada na wasamaria wema walijitokeza na
kumpeleka Kituo cha Afya Mang’ula.
Mganga Mkuu wa Mang’ula, Eugen Shirima alisema
baada ya huduma ya kwanza walimpatia rufaa ya kwenda Hospitali ya
Mtakatifu Francis, Ifakara kwa matibabu lakini alifariki dunia wakiwa
njiani.
Na Lilian Lucas, Mwananchi
Na Lilian Lucas, Mwananchi
Endapo una Habari,Picha,Video,Tangazo au Tatizo Lolote wasiliana nasi kwa namba +255 688 405 951