UKATILI WA KUTISHA!! MTOTO ACHUNWA NGOZI YA USO NA BOSI WAKE,WANANCHI WAPIGWA MABOMU

 


Katika hali ya kusikitisha jamii, mtoto yatima mwenye umri wa miaka saba (jina linahifadhiwa), amejikuta ‘akisulubiwa’ kwa kufanyiwa vitendo vya kinyama baada ya kulazimishwa kufanyakazi ngumu, kupigwa na kuchunwa uso na mtu anayedaiwa kuwa mwajiri wake.
Wananchi wanaoishi eneo ambalo mtoto huyo ameajiriwa, walichukizwa na kitendo cha kumuona akiwa amejeruhiwa na kuvimba uso, hivyo kuamua kuvamia nyumba ya mwanamke aliyemuajiri kwa lengo la kumkamata.

Tukio hilo lililotokea wiki iliyopita eneo la Ruvuma Kipande, Temeke jijini Dar es Salaam, lilisababisha vurugu na kulazimisha polisi kuingilia kati kwa kurusha mabomu ya machozi.

Mwanamke anayedaiwa kufanya unyama huo aliyetambulika kwa jina la Salma Mwasha, hata hivyo, alinusurika kupigwa na wananchi baada ya polisi kuingilia kati kwa kumkamata.

Mtoto huyo kwa sasa amehifadhiwa katika kituo cha kulelea watoto baada ya kupewa huduma ya matibabu katika Hospitali ya Temeke.

MTOTO ASIMULIA
Akisimulia tukio hilo, mtoto huyo mwenyeji wa Ikungi, mkoani Singida, anasema maisha yake katika nyumba hiyo yalitawaliwa na vipigo vikali, kufanyishwa kazi ngumu na wakati mwingine kunyimwa chakula.

Alisema alichukuliwa na Salma nyumbani kwao kwa madai ya kuja jijini Dare s Salaam kumsomesha.

Alisema wakati utaratibu wa kuchukuliwa unafanyika, hakuwahi kumuona Salma, badala yake watu wawili walihusika katika majadiliano na walezi wake na kisha kumsafirisha hadi kituo cha mabasi cha Ubungo.

“Baada ya kufika Ubungo ndipo nilipomuona mama Salma, lakini toka siku hiyo nilikuwa naishi kwa mateso makubwa,” alisema mtoto huyo.

Alitaja baadhi ya kazi alizokuwa akifanya ni kufua nguo zote za familia, mashuka, nguo za ndani za watoto na bosi wake.

“Mimi siwezi kufua shuka kwa sababu ni nzito, ninaposhindwa anachukua mwiko na kunipiga huku akinifungia bafuni,” alisema.

ACHUNWA NGOZI YA USO
Aliongeza kwamba katika tukio ambalo lilisababisha wananchi kumuokoa na mateso hayo, ni baada ya tajiri wake kumpiga na kumchuna usoni kwa kutumia kucha za bandia.

Alisema alifanya unyama huo baada ya mume wa Salma kumkuta mke wake akimpiga binti huyo bila sababu.

“Siku ile mama alikuwa akinipiga kama kawaida yake, ghafla baba aliingia ndani na kuona kila kitu, ndipo alipomshika na kumuadhibu kitu ambacho kilimkasirisha na alisubiri mumewe aondoke ndipo alipoanza kunichuna kwa kutumia kucha bandia, nilitokwa na damu nyingi lakini hakujali,” alisema.

Baada ya kufanyiwa unyama huo, alifungiwa ndani ya nyumba na kunyimwa matibabu.

Hata hivyo, anamshukuru sana mzee huyo kwa kile alichosema alikuwa kama mkombozi wake kwa sababu mara kadhaa alionyesha kupinga vitendo hivyo.

WANANCHI WARUSHIWA MABOMU
Baadhi ya wananchi wanaoishi jirani na nyumba hiyo, walisema waliamua kuingilia kati baada ya kumuona binti huyo akiwa katika hali mbaya kutokana na uso wake kuvimba huku ikionekana mikwaruzo ya majeraha.

Mmoja wa majirani aliyejitambulisha kwa jina la Halima Hashim, alisema pamoja na kuwa katika hali hiyo alilazimishwa kwenda sokoni kununua mboga.

“Alipokwenda sokoni mtoto alishindwa kuongea  kutokana na uso kuvimba sana, alipobanwa sana na wauza mboga ndipo kwa shida aliongea eti kapigwa na tajiri yake,” alisema Halima.

Alisema baada ya taarifa hiyo kusambaa wananchi walijaa hasira na ndipo walipoamua kwenda kuivamia nyumba ya mwanamke huyo kwa nia ya kumkamata ili wamfikishe polisi.

Hata hivyo, katika vurugu hizo polisi waliingilia kati kwa kuwatawanya wananchi hao kwa kutumia mabomu ya machozi na kumkamata mwanamke huyo na kumfikisha polisi.

POLISI YAKIRI
Mkuu wa Polisi dawati la jinsia Wilaya ya Temeke, Mwananzige Mkayala, alikiri kumkamata mwanamke huyo na kueleza taratibu zinafanyika ili kumfikisha mahakamani.

“Mwanamke huyo ameletwa hapa polisi kwa kosa la unyanyasaji kwa mtoto, tutaendelea na uchunguzi wetu ili tuweze kumfikisha mahakamani,” alisema Mwananzige.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post