Vijana watano wanadaiwa kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 14
kwa zamu hadi kuzirai.
Mtoto huyo alikuwa akitokea Kata ya Nyamatere kusherehekea matokeo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Manispaa ya Musoma.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Phillip Kalangi
alisema tukio hilo lilitokea Desemba 20, mwaka huu saa 2.00 usiku katika
Mtaa wa Wakala.
Kamanda Kalangi alisema mtoto aliyetendewa unyama
huo ni miongoni mwa watoto wanaotarajia kujiunga na kidato cha kwanza
mwakani, baada ya kuhitimu katika Shule ya Msingi Buhare.
Kamanda huyo akielezea chanzo cha tukio hilo,
alisema mtoto huyo alikuwa njiani akienda nyumbani kwao katika Mtaa wa
Makoko Zanzibar akitokea katika ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kata
ya Nyamatare kwenye sherehe za ushindi wa chama hicho katika uchaguzi
wa Serikali za Mitaa.
Alisema njiani alikutana na kundi la vijana watano
ambao wote alikuwa akiwatambua kwa sura, ghafla vijana hao walimkamata
kwa nguvu na kumpeleka katika nyumba ambayo ujenzi wake haujakamilika na
kuanza kumbaka kwa zamu hadi mtoto huyo alipopoteza fahamu na kisha
vijana hao kutoroka.
Alisema mtoto huyo alizinduka saa nane usiku akiwa
hajiwezi, kwa msaada wa Mungu aliweza kujivuta hadi katika nyumba
zilizo jirani na nyumba hiyo na kuomba msaada, majirani hao walimfikisha
katika kituo cha polisi usiku huo na kupewa fomu namba tatu,
walimpeleka kupata matibabu katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Mara.
Kamanda alisema hali yake kwa sasa inaendelea vizuri na tayari polisi wanamshikilia mtuhumiwa mmoja ambaye jina lake linahifadhiwa, mkazi wa Mtaa wa Nyamatare mjini hapa na atafikishwa mahakamani wakati wowote baada ya upelelezi kukamilika.
Na Florence Focus, Mwananchi