Askofu
Edson Mwombeki katika picha ya pamoja na mbunge wa Jimbo la Shinyanga
mjini, Stephen Masele pamoja na mmoja wa vikongwe wanaotunzwa na kanisa
la Tanzania Field Evangelism Shinyanga.
ASKOFU wa kanisa la Tanzania Field
Evangelism la mjini Shinyanga, Edson Mwombeki amekitahadharisha Chama
cha Mapinduzi (CCM) huenda kikajikuta katika wakati mgumu kwenye
uchaguzi mkuu ujao kisipokemea tabia ya wabunge wake wanaotoa ahadi kwa
wananchi bila ya kuzitekeleza.
Askofu
Mwombeki alitoa tahadhari hiyo ofisini kwake ambapo alisema CCM inaweza
kujikuta ikipoteza majimbo ya Shinyanga mjini na Kishapu iwapo
haitawaweka kitako wabunge wake, Stephen Masele na Suleiman Nchambi kwa
lengo la kuwahimiza ili watekeleze ahadi zao kwa wananchi.
Mbali
ya tahadhari hiyo Askofu Mwombeki alisema kanisa lake halitokuwa tayari
kumpigia kampeni mbunge ye yote atakayeshindwa kutekeleza ahadi zake na
kusimamia vyema ilani ya uchaguzi ya chama chake huku akijipanga kurudi
kugombea tena ubunge akitegemea kutumia fedha kuwarubuni wapiga kura.
Alisema
iwapo CCM itashindwa kuwarekebisha wabunge hao kwa kuhakikisha
wanatimiza ahadi walizozitoa kwa wananchi kanisa lake litasimama kidete
kuwahimiza wananchi katika majimbo yao wasiwachague tena kwa vile
watakuwa wameonesha wazi kugombea kwao awali haikuwa kwa ajili ya
maslahi ya wananchi bali kutafuta maslahi yao binafsi.
Akimzungumzia
mbunge wa jimbo la Shinyanga mjini Askofu huyo alisema mara baada ya
kuchaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo alitoa ahadi nyingi ambazo kwa
sehemu kubwa ameshindwa kuzitekeleza ambapo amediriki hata kulidanganya
kanisa kitu ambacho hakina sura nzuri mbele za mungu.